Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi

Mwanafunzi Isra Hilal Mwadini akifuatiwa na mwenzake Tamima Abass Sheha wakipokea zawadi kutoka kwa mgeni rasmi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif wakati wa hafla ya Maulidi ya Jumuiya ya Chuo cha Samael Academy.Kulia ya Balozi Seif ni Rais wa Sameil Academy Sheikh Nassir Bin Said.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizindua rasmi Bara bara ya pili ya Amani hadi Mtoni baada ya kukamilika awamu ya mwisho ikiwa ni shamra shamra za maadhimisho ya kutimia miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar

Akiwa na Balozi mdogo wa India nchini Tanzania wakiangalia maonyesho yaliofanya na Msanii kutoka India, Bi Navi Madhav hapo Ngome Kongwe

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Dk. Khalid S. Mohamed

akizungumza na Wadau wa Maendeleo wa Mfuko wa TASAF, walipofika Ofisini kwake kuzungumzia maendeleo ya Mfuko wa TASAF III,na kutembelea Mradi wa Mpango wa Kunusuru Kaya masikini (PSSN) katika Jimbo la Muyuni Wilaya ya Kusini Unguja katika Kijiji cha Muyuni B

Wazir wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar

Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakifurahia jambo wakati wa semina ya siku moja kuhusu matokeo makubwa na ya haraka katika kuleta mageuzi ya kiuchumi na kuleta maendeleo nchini iliyofanyika leo katika ukumbi wa Ikulu Mjini Unguja na kufunguliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein

Friday, 20 February 2015

Balozi Seif Afungua Mkutano wa Unaozungumzia Changamoto za Ukuaji wa Mji.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiufungua Mkutano wa Siku mbili wa kanda unaozungumzia changamoto za ukuaji wa Miji pamoja na kushughulikia hali ya baadaye ya Miji ya  Afrika unaofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency Kilimanjayo Mjini Dara es salaamu.
Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa Siku mbili unaozungumzia changamoto za ukuaji wa Miji pamoja na kushughulikia hali ya baadaye ya Miji ya  Afrika.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif pamoja na Viongozi na washiriki wa Mkutano huo wakifuatilia mada inayohusu Miji inavyoweza kukuza uchumi iliyotolewa na Mtaalamu wa masuala ya Uchumi kutoka Sweden Dr. David Simon.
 Balozi Seif akiwa pamoja na Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi wa Afrika kwa Maendeleo endelevu { Uongozi Institute } Profesa Joseph Semboja wakielekea kwenye ukumbi wa Mikutano kwa ajili ya ufunguzi wa Mkutano unaozungumzia changamoto za ukuaji wa Miji pamoja na kushughulikia hali ya baadaye ya Miji ya  Afrika.(Picha na –OMPR )
Na Othman Khamis OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba ujenzi wa nyumba za Mkopo pamoja na bei nafuu na kulengwa kwa wananchi wenye kipato cha kawaida katika maeneo ya Miji na vitongoji vyake ndio njia pekee itakayosaidia mfumo mzuri katika uwekaji wa mipango Miji.
Alisema ujenzi holela usiozingatia Mipango Miji unaoendelea kukua siku hadi siku katika maeneo ya miji hasa ile ya Jumuyia ya Afrika Mashariki mara nyingi huleta athari wakati yanapotokea mafuriko au majanga ya moto.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akiufungua Mkutano wa Siku mbili wa kanda  unaozungumzia changamoto za ukuaji wa Miji pamoja na kushughulikia hali ya baadaye ya Miji ya  Afrika unaofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency Kilimanjayo Mjini Dara es salaamu.
Mkutano huo uliopewa jina la Maisha ya baadaye ya Nchi za Afrika Mashariki, jinsi gani tunataka kuishi mwaka 2050 umeandaliwa na Taasisi ya Uongozi wa Afrika kwa Maendeleo endelevu { UONGOZI INSTITUTE }.

Alisema asilimia kubwa ya wananchi wa kawaida huishi kwa kujenga makaazi yao kwenye maeneo hatarishi ambayo wakati yanapotokea maafa au mafuriko Wananchi hao wanashindwa kupata huduma muhimu za lazima kutokana na uharibifu wa mazingira na matokeo yake hukumbwa na miripuko ya maradhi yanayosababisha kupoteza idadi kubwa ya maisha ya watu.
Balozi Seif alizinasihi Taasisi, wataalamu na Viongozi wanaosimamia Mipango Miji kuelewa kwamba ili kufikia malengo ya maisha bora ya Jamii pamoja na kukuwa kwa miji bado ipo haja ya kuimarishwa miundo mbinu ya huduma muhimu za lazima katika Halmashauri za Mikoa, Wilaya na Vijiji ili kupunguza kasi ya ukuaji wa miji Mikubwa.
Mapema Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi wa Afrika kwa Maendeleo endelevu { Uongozi Institute } Profesa Joseph Semboja alisema upo uwiano mkubwa wa ongezeko la watu Barani Afrika na Dunia kwa ujumla.
Profesa Semboja alisema ongezeko hilo linasababisha msongamano wa  shinikizo la uhaba wa makaazi ya watu , ufinyu wa fursa za ajira hasa kwa vijana pamoja na huduma za Kijamii.
Alisema ukanda wa Afrika Mashariki unaendelea kukumbwa na changamoto mbali mbali za tabia nchi, mazingira sambamba na ongezeko kubwa la idadi ya wakaazi wake katika Miji ya Nchi hizo.
“ Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi { UN Habitat } hali ya Miji ya Afrika 2014, Afrika Mashariki inashika nafasi ya chini katika Miji inayokuwa Duniani lakini ndio kanda inayoongoza katika kasi ya ukuaji wa Miji yake kwa sasa “. Alisema Profesa Semboja.
Alifahamisha kwamba ifikapo mwishoni mwa muongo huu wa sasa idadi ya wakaazi waishio Mijini itaongezeka kwa asilimia 50% na jumla ya idadi ya wakaazi wa mijini ifikapo mwaka 2040 inatarajiwa kuwa mara tano ya mwaka 2012.
Profesa Semboja alieleza kwamba lengo la Mkutano huo wa kanda unaokutanisha Viongozi na watunga sera kutoka nchi za Afrika mashariki umelenga kujadili namna ya kutatua  changamoto hizo na kufikiria miji ambayo itatimiza matakwa yaliyokusudiwa.
Akitoa salamu za shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi { UN Habitat } Mwakilishi wa shirika hilo Dr. Remy Sietchiping alisema nguvu za Viongozi wa Kisiasa zitumike katika kusaidia Taaluma ya ujenzi wa Mipango Miji.
Dr. Remy alisema mipango hiyo lazima iende sambamba katika kukabiliana na ongezeko kubwa la idadi ya watu.
Alifahamisha kwamba Shirika hilo la Habitat litahakikisha kwamba linatumia nguvu na uwezo wake katika kusaidia Taaluma ya upangaji wa Miji Barani Afrika.
Washiriki wa Mkutano huo kutoka Nchi za Burundi, Ethiopia,, Kenya, Rwanda, Somalia, Sudani ya Kusini, Uganda na wenyeji Tanzania wengi wao ni watendaji wa ngazi za juu Serikalini, mshirika ya Kikanda na Kimataifa, Miji Mikubwa, wasomi, Sekta Binafsi na Taasisi za Kiraia.
 

Wednesday, 18 February 2015

Moto wadhibitiwa hifadhi ya Taifa ya msitu wa Jozani


 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akizungumza na Uongozi wa Wizara ya Kilimo na Mali Asili wakati alipotembelea eneo liloathirika kwa moto kwenye Hifadhi ya Msitu wa Jozani Mkoa wa Kusini Unguja.
Mwanzo kushoto ni Waziri wa Kilimo na Mali Asili Zanzibar Dr. Sira Ubwa Mwamboya na Katbu Mkuu wa Wizara hiyo Nd. Afan Othman Maalim.
 Baadhi ya sehemu za miti iliyoathirika kwa moto kwenye msitu wa Hifadhi ya Jozani ambao kwa sasa umedhibitiwa baada ya juhudi za vikosi vya ulinzi kwa kushirikiana na wananchi wa Mkoa wa Kusini Unguja.

 Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Mali Asili Nd. Afan Othman Maalim akimueleza Balozi Seif aliyepo kati kati yao jinsi vikosi vya ulinzi na wananchi walivyofanikiwa kuudhibiti moto ulioibuka ndani yam situ wa Jozani.
 Balozi Seif akiwapongeza askari  na Makamanda wa vikosi vya ulinzi walivyofanikiwa kuuzima moto ulioibuka ndani ya msitu wa Hifadhi ya Jozani Mkoa wa Kusini Unguja.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiwa pamoja na Waziri wa Kilimo na Mali Asili Zanzibar Dr. Sira Ubwa Mwamboya wakitembelea baadhi ya maeneo yaliyoathirika kwa moto kwenye msitu wa Hifadhi wa Jozani.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis Ame, OMPR
Vikosi vya ulinzi  na Uokozi kwa kushirikiana na wafanyakazi wa Wizara ya Kilimo na Mali Asili pamoja na wananchi wa Mkoa wa Kusini Unguja wamefanikiwa kuuzima moto katika Hifadhi ya Taifa ya Msitu wa Jozani  ulioibuka upande wa magharibi ya msitu huo maarufu Jozani Kovu.  
Hekta zipatazo 17  kati ya elfu 5,000 zilizomo ndani ya  Hifadhi ya Taifa ya Msitu huo  zimeathirika kwa moto unaodhaniwa  kuibuka  juzi jioni  kutokana na wavunaji  haramu wa Asali.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alifika eneo la tukio kuangalia athari iliyotokea kwenye msitu huo wenye hadhi ya Kimataifa kutokana na mazingira yake ya miti pamoja na wanyama adimu Duniani.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Mali Asili Zanzibar Nd. Afan Othman Maalim alimueleza Balozi Seif kwamba juhudi za vikosi vya ulinzi kwa kushirikiana na wananchi wa Vijiji Jirani imesaidia kuudhibiti moto huo usiingie kwenye msitu mkubwa.
Katibu Mkuu  Afan alisema unyevunyevu uliopo kwenye eneo hilo { Maarufu kwa jina la Kigeni Ground Water Floor } nao umechangia kuepusha athari zaidi za kuenea kwa moto huo kwa  kutoathiri  miti mikubwa.
“ Tumepata faraja kubwa baada ya kuona moto huo uliunguza majani ya chini bila ya kuathiri ile miti mikubwa. Hii inatokana na mazingira ya eneo lenyewe kuwa na unyevunyevu “. Alisema Nd. Afan  Othman Maalim.
Alifahamisha  kwamba wakulima wa Bonde la Cheju wamekuwa wakitegemea vianzio  vya maji  vilivyomo kwenye msitu wa Jozani ambavyo vinastahiki kulindwa kwa njia yoyote.
“ Hadhi ya Kimataifa iliyopo katika hifadhi ya Msitu wa Jozani inaweza kupotea iwapo uchafuzi wa mazingira katika eneo hilo hautadhibitiwa “. Alisisitiza Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Kilimo na Mali Asili Zanzibar.

Alisema kuathirika kwa msitu huo mbali ya kuchafuka  kwa mazingira katika eneo hilo la hifadhi ya Taifa lakini pia kilimo cha mpunga katika Bonde la Cheju kinaweza kuwa hatarini  kutoweka kwa kukosa rasilmali ya maji.
Akitoa shukrani Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameiagiza Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na uongozi wa Serikali ya Mkoa wa Kusini Unguja kuchukuwa hatua za kukabiliana na wagemaji haramu wa asali ili kujaribu kuzuia uharibifu wa mazingira.
Balozi Seif alisema kwa niaba yake na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar amevipongeza Vikosi vya ulinzi kwa kushirikiana na wananchi  kutokana na  juhudi kubwa walizochukuwa za kufanikiwa kuuzima moto huo.
Alifahamisha kwamba Jozani ikiwa ni miongoni mwa Misitu miwili mikubwa katika Visiwa vya Zanzibar  Ukiwepo  sambamba  na ule wa Ngezi Kisiwani Pemba lazima iendelee kudhibitiwa kwa nguvu zote.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kuwa Idara ya Maafa kwa kushirikiana na Taasisi za Kimataifa  itaangalia njia za kufanya utafiti utakaosaidia kutoa taaluma kwa Jamii juu ya kuendelea kuhifadhi rasilimali hiyo ya Taifa.
Naye Mkuu wa Kikosi cha Zimamoto na Uokozi Zanzibar Mkoa wa Kusini Unguja     { SSF } Shaaban Ramadhan Ali alisema kikosi hicho bado kinaendelea kukumbwa na changamoto ya vifaa na usafiri katika utekelezaji wa majukumu yake.
SSP Shaaban Ramashan alisema yapo matukio ya maafa yanayotokea katika baadhi ya sehemu ambayo Kikosi chake kinakuwa na mazingira magumu kukabiliana nayo kutokana na miundo mbinu duni.
“ Tunapata matatizo wakati tunapokabiliana na majanga kama moto katika maeneo kama haya kwa kukosa gari zenye kiwango cha maji kinachotosheleza nguvu za kukabiliana na janga halisi “. Alifafanua SSF Shaaban Ramadhan.
Hifadhi ya Taifa ya Msitu wa Jozani imekuwa maarufu kimataifa kutokana na maumbile yake ya kuwa na viumbe mchanganyiko wakiwemo wanyama  adimu kama kima punju, Paa Nunga, nguruwe, Vipepeo na aina mchanganyiko ya ndege.

Waziri Aboud akiendelea na ziara nchini Dubai



Waheshimiwa Janet Mbene na Mohammed Aboud, leo wameendelea na ziara yao ya kikazi Dubai. Katika kikao cha leo, ujumbe huu pamoja na mwenyeji wao Mhe. Omar Mjenga, wamefanya mazungumzo ya biashara na Rais Mstaafu wa Comoro Mzee Sambi.
Pichani ni mazungumzo hayo yakiendelea.
 
 
Mawaziri Mohamed Aboud na Janet Mbene wakiwa katika picha ya pamoja na Rais mstaafu wa visiwa vya Comoro (katikati) pamoja na wenyeji wao

Sunday, 15 February 2015

Balozi Seif Awataka Wananchi Waliojenga Katika Viazio vya Maji, kuacha ujenzi maeneo hayo.


Mkuu wa Wilaya ya Magharibi Nd. Ayoub Moh’d Mahmoud kushoto aliyevaa kanzu na kofia ya Kiua akitoa maelezo mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  Ali Iddi wa Pili kutoka Kulia kuhusu eneo la Msitu wa Kimaumbile liliopo masingini Dole pamoja na lile ya vianzio vya maji Dole.Kushoto ya Balozi Seif ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Magharibi Nd. Yussuf Moh’f  Yussuf.Kulia ya Balozi Seif ni Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Mali Asili Zanzibar Nd. Afan Othman Maalim na Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mh. Mtumwa Kheir Mbarak.Picha na – OMPR – ZNZ.

                                          
Na Othman Khamis OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameuagiza Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Magharibi pamoja na taasisi zinazosimamia masuala ya ujenzi kuhakikisha kwamba nyumba zilizojengwa  na zinazoendelea kujengwa katika vianzio vya maji vya Dole zinavunjwa haraka iwezekanavyo.

Alisema hatua hiyo ya Serikali imekuja kuzingatia  uharibifu unaoonekana kuendelea kufanywa katika vianzio vya maji jambo ambalo ni hatari kwa uchafuzi wa mazingira sambamba na afya za wananchi.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa agizo hilo wakati alipofanya ziara fupi ya kukagua eneo la Msitu wa Kimaumbile liliopo masingini Dole pamoja na lile ya vianzio vya maji Dole linaloonekana kuanza kuvamiwa kwa ujenzi wa nyumba licha ya amri iliyowahi kutolewa na Mamlaka ya Maji Zanzibar { ZAWA } ya kuzuia ujenzi huo.

Alisema uongozi wa Halmashauri hiyo lazima ufanye utaratibu wa kuwahamisha watu wote waliojenga kwenye vianzio hivyo vya maji ili kuendelea kuheshimu ipasavyo maeneo hayo muhimu kwa ustawi wa Jamii.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba Wataalamu wa Kilimo na mazingira wanaruhusu maeneo ya vianzio vya maji kutumika kwa vilimo vya aina mbali mbali kwani havichafui wala kuhatarisha  mazingira ya vianzio hivyo.


Mapema Sheha wa Shehia ya Dole Bwana Ibrahim Shaaban Othman alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Mamlaka ya Maji Zanzibar { ZAWA } iliwahi kuweka  Mabango ya matangazo   kujaribu  kusimamisha ujenzi wa aina yoyote kwenye eneo hilo.
Hata hivyo Sheha Ibrahimu alisema kwamba harakati za ujenzi  wa nyumba hizo  zilizopo mita chache kutoka kwenye kisima hicho cha Dole ziliendelea kama nyengine zikiwa katika hatua ya kukamilika.

Balozi Seif Atembelea hoteli ilioungua kwa moto Nungwi Kendwa.



Baadhi ya Sehemu za jengo la Jiko la Hoteli ya Kendwa Rocks iliyoko Mkoa wa Kaskazini Unguja ambalo iliuungua moto ulisababishwa na hitilafu za umeme.

Wahandisi wa Hoteli ya Kendwa wakijaribu kurejesha miundo mbinu ya umeme iliyoathirika kutokana na moto mkubwa uliotokea kwenye Hoteli hiyo.
Jengo la Jiko la Hoteli ya Kendwa Rocks lililoungua vibaya mwa moto uliosababishwa na hitilafu ya umeme.
  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimfariji Mwakilishi wa Hoteli ya Gold Zanzibar iliyopo Nungwi  Mkoa wa Kaskazini Unguja Bwana Andrea Azzala baada ya paa la jengo lao kuungua moto.
Balozi Seif akikaguzwa kuangalia maeneo yaliathirikia kutokana na moto kwenye Hoteli ya Kendwa Rocks Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Kulia ya Balozi Seif ni  Msaidizi Menja Mkuu wa Kendwa Rocks Bwana Omar Ibrahim Kilupi, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Kanal Mstaafu Juma Kassim Tindwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Moh’d Aboud Moh’d.
Balozi Seif akiwafariji wamiliki wa Kendwa Rocks Bwana Ali Ibrahim Kilupi aliyepo mwnzo kushto na msaidizi wake Omar Ibrahim Kilupi baada ya jengo la jiko la hoteli yao kuungua moto.Kati kati ni Waziuri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Moh’d Aboud Moh’d na kushoto kwa Balozi Seif ni Mkuu wa Mkoa Kaskazini Unguja Kanal Mstaafu Juma Kassin Tindwa.
Picha na – OMPR – ZNZ.
                                                                                                                                                                          
Na Othman Khamis OMPR
Hitilafu ya umeme iliyotokea mapema  asubuhi imesababisha moto mkubwa   ulioteketeza jengo la jiko, Duka ,sehemu ya burdani ya Hoteli Kendwa Rocks pamoja na Hoteli ya Gold Zanzibar zilizopo katika Kijiji cha Nungwi Mkoa wa kaskazini Unguja.
Moto huo ulioripuka kwa kusaidiwa na upepo mkali uliokuwa ukivuma majira ya saa nne za asubuhi umeteketeza vitu na vifaa mbali  vilivyokuwemo ndani ya majengo hayo na kusabisha hasara inayokisiwa kufikia shilingi za Kitanzania Bilioni Moja { 1,000,000,000/- }.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiambatana pamoja na Waziri wa  Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  Mh. Moh’d Aboud Moh’d walifika eneo la tukio kuwafariji wamiliki wa Hoteli hizo.
Meneja wa Kendwa Rocks Bwana Ali Ibrahim Kilupi alimueleza Balozi Seif kwamba wafanyakazi  kwa kushirikiana na wananchi wanaozizunguuka Hoteli hizo walijaribu kuuzima moto huo uliokuwa ukiwaka kwa kasi kutokana na upepo mkali uliovuma wakati huo.
Bwana Ali alifahamisha kwamba Uongozi wa Hoteli hiyo ulijaribu kuwasiliana na Kikosi cha Zima moto na Uokozi  Zanzibar kujaribu kusaidia uokozi huo lakini wakati huduma hizo zinakaribi kufika kasi ya moto huo iliyochukuwa baina ya dakika 15 na 20 tayari ilikuwa imeshateketeza vifaa na vitu vyote.
Alieleza kwamba licha ya wageni wengi kuvutiwa na mazingira ya nyumba zinazoezekwa makuti lakini Uongozi wa Hoteli hiyo umeamua kubadilisha mfumo huo kwa kutumia vitage ili kujaribu kujikinga na majanga kama hayo.
Naye Mwakilishi wa Hoteli ya Gold Zanzibar Bwana Andrea Azzala alisema kwa kwa hivi sasa  ni mapema mno kujua hasara iliyopatikana kutokana na kuungua kwa paa la jengo lao moja.
Bwana Andrea aliwashukuru wafanyakazi na baadhi ya wananchi wa vijiji jirani vilivyozuunguka Hoteli hizo kwa jitihada zao zilizosaidia kukabiliana na moto huo uliovumba ghafla mapema asubuhi.
Akitoa pole kwa wamiliki wa miradi hiyo ya Hoteli Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesikitishwa kutokea kwa janga hilo la moto litakalorejesha nyuma malengo ya wamiliki wa hoteli hizo.
Hata hivyo Balozi Seif amefurahishwa na Uongozi wa Hoteli hiyo kwa uamuzi wake wa kuuwekea  bima ya moto mradi wao  kwani itasaidia kupunguza machungu ya hasara iliyotokea.
Alisema maafisa wa Idara ya Maafa Zanzibar ambayo iko chini ya Ofisi yake  itafanya tathmini kujuwa harasa kamili iliyotokea ya janga hilo na kuripoti Serikalini ili kuangalia namna ya kusaidia wawekezaji hao wazalendo.
Akitoa shukrani kwa niaba ya Uongozi wa hoteli ya Kendwa Rocks Msaidizi meneja Mkuu wa Hoteli hiyo Bwana Omar  Ibrahim Kilupi ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibaf kwa  kuwa karibu na Wananchi wake.
Majanga ya miripuko ya moto yamekuwa yakitokea mara kwa mara katika kipindi cha kiangazi na kusababisha hasara kubwa inayochukuwa muda mrefu hasa kwenye miradi ya hotel.

Thursday, 5 February 2015

Balozi Seif Azungumza na Mwakilishi wa Kampuni ya Ms Shimoja. ya Marekani


Balozi wa Heshima wa Tanzania Nchini Marekani ambae pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Ms Shimoja ya Nchini Marekani Dr. Robert Shumake akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini kwake iliyopo katika Jengo la Msekwa ndani ya Viunga vya Bunge la Jamuhuri nya Muungano wa Tanzania Mjini Dodoma.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akibadilishana mawazo na Balozi wa Heshima wa Tanzania Nchini Marekani ambae pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Ms Shimoja  ya Nchini Marekani Dr. Robert Shumake Bungeni Mjini Dodoma.(Picha na – OPMR)
Na Othman Khamis. OMPR 
Kampuni ya Ms Shimoja  yenye Makao Makuu yake katika Jimbo la Michigan  Nchini Marekani iko mbioni kutaka kuanzisha kituo cha Matangazo ya Televisheni Mjini Dar es salaam Nchini Tanzania kitakachotoa huduma ndani ya Ukanda wa Afrika Mashariki.
Mkurugenzi wa Kampuni hiyo ambae pia ni Balozi wa Heshima wa Tanzania Nchini Marekani Dr. Robert Shumake alieleza hayo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini kwake katika Jengo la Msekwa ndani ya viunga vya Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mjini Dodoma.
Dr. Shumake alisema licha ya kwamba matangazo ya Televisheni yanachukuwa sehemu kubwa ya burdani lakini Kituo hicho kitalenga zaidi kutoa vipindi wa Elimu vitakavyowasaidia wananchi na hasa wanafunzi wa elimu ya msingi, sekondari na vyuo vikuu Afrika Mashariki.
Alisema mipango inaandaliwa na Kampuni hiyo katika kuyashirikisha Makampuni ya Mitandao ya Mawasiliano Duniani ya Google na Microsoft ili kuona Elimu inayokusudiwa kufikishwa kwa umma kupitia matangazo ya Kituo hicho yanafanikiwa kwa kiwango kikubwa.

Dr. Shumake alifahamisha kwamba mpango huo unakusudiwa kwenda sambamba na ule utakaoandaliwa na Kampuni hiyo wa kuwapatia mafunzo vijana wapatao 50,000 kutoka Bara la Afrika katika Jimbo la Michigan Nchini Marekani.
Alisema hatua hiyo inakusudia kuwajengea uwezo wa ajira vijana hao katika fani ya  ujasiri amali utakaowapa fursa nzuri ya kufanya kazi katika taasisi na mashirikia yoyote ya Kitaifa na Kimataifa.
“ Tumejipanga kuwapatia mafunzo maalum viiana wa Bara la Afrika ili kusaidia kupunguza wimbi la vijana wasio na ajira ndani ya Bara hili “. Alifafanua Balozi huyo wa Heshima wa Tanzania Nchini Marekani Dr. Shumake.
Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alimshukuru Dr. Robert  Shumake pamoja na Kampuni yake kwa uamuzi huo wa busara utakaowezesha kuisaidia pia Serikali katika mapambano dhidi ya uhaba wa ajira Nchini.
 Balozi Seif alisema Serikali zote mbili ile ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Mapinduzi ya Zanzibar zimeweka milango wazi kwa taasisi na mashirika ya Kitaifa na Kimataifa kuwekeza miradi yao kwa kutumia rasilmali zilizopo nchini ili kusaidia nguvu za kiuchumi na kupunguza ukali wa maisha.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimshauri Mkurugenzi huyo wa Kampuni ya Ms Shimoja ya Nchini Marekani kuangalia fursa nyingi zaidi  za uwekezaji zilizopo Nchini Tanzania ambazo Kampuni yake inaweza kuongeza uwekezaji zaidi.

Tuesday, 3 February 2015

Matayarisho ya ujio wa Rais wa shirikisho la Ujerumani

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akitembelea Bandari ya Malindi kuangalia matayarisho ya ujio wa  Rais wa shirikisho la Ujerumani Bwana Joachik Gauck.


Kushoto ya Balozi Seif ni Mshauri wa Rais anaesimamia Uchumi, Uwekezaji na Ushirikiano wa Kimataifa Balozi Moh’d Ramia na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar Nd. Abdulla Juma Abdulla.
  Balozi Seif akiwa na Viongozi wa Kamati ya kuratibu Mapokezi ya Rais wa Ujerumani wakirudi kukagua eneo la kushukia boti  ziendazo kwa kasi katika Bandari ya Malindi.


Kushoto yake ni  Mshauri wa Rais Balozi Moh’d Ramia, Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Nje Zanzibar Balozi Silima Kombo Haji pamoja na Mkurugenzi Bandari Nd. Abdulla Juma.


 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiwa pamoja na Balozi Mdogo wa Heshima wa Shirikisho la Ujerumani hapa Zanzibar Balozi Has –Dieter Allgaier wakielekea kukagua chum,baa cha watu Mashuhuri { VIP }  kiliopo Bandari ya Malindi ambacho kimewekwa hakiba kwa ujio wa Rais wa Shirikisho la Ujerumani Bwana Joachim Gauck.
Mshauri wa Rais anayesimamia Uchumi,Uwekezaji na Ushirikiano wa Kimataifa Balozi Moh’ d Ramia akimuelezea Balozi Seif hatua zilizochukuliwa katika matayarisho ya ujio wa Rais wa Ujerumani.


Kati kati yao ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Moh’d Aboud Moh’d na kulia ya Balozi Ramia ni Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Nje Zanzibar Balozi Silima Kombo Haji.