Mwanzo kushoto ni Waziri wa Kilimo na Mali Asili Zanzibar Dr. Sira Ubwa Mwamboya na Katbu Mkuu wa Wizara hiyo Nd. Afan Othman Maalim.
Baadhi ya sehemu za miti iliyoathirika kwa moto kwenye msitu wa Hifadhi ya Jozani ambao kwa sasa umedhibitiwa baada ya juhudi za vikosi vya ulinzi kwa kushirikiana na wananchi wa Mkoa wa Kusini Unguja.
Balozi Seif akiwapongeza askari na Makamanda wa vikosi vya ulinzi walivyofanikiwa kuuzima moto ulioibuka ndani ya msitu wa Hifadhi ya Jozani Mkoa wa Kusini Unguja.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiwa pamoja na Waziri wa Kilimo na Mali Asili Zanzibar Dr. Sira Ubwa Mwamboya wakitembelea baadhi ya maeneo yaliyoathirika kwa moto kwenye msitu wa Hifadhi wa Jozani.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Na Othman Khamis Ame, OMPR
Vikosi vya ulinzi na Uokozi kwa kushirikiana na wafanyakazi wa Wizara ya Kilimo na Mali Asili pamoja na wananchi wa Mkoa wa Kusini Unguja wamefanikiwa kuuzima moto katika Hifadhi ya Taifa ya Msitu wa Jozani ulioibuka upande wa magharibi ya msitu huo maarufu Jozani Kovu.
Hekta zipatazo 17 kati ya elfu 5,000 zilizomo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Msitu huo zimeathirika kwa moto unaodhaniwa kuibuka juzi jioni kutokana na wavunaji haramu wa Asali.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alifika eneo la tukio kuangalia athari iliyotokea kwenye msitu huo wenye hadhi ya Kimataifa kutokana na mazingira yake ya miti pamoja na wanyama adimu Duniani.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Mali Asili Zanzibar Nd. Afan Othman Maalim alimueleza Balozi Seif kwamba juhudi za vikosi vya ulinzi kwa kushirikiana na wananchi wa Vijiji Jirani imesaidia kuudhibiti moto huo usiingie kwenye msitu mkubwa.
Katibu Mkuu Afan alisema unyevunyevu uliopo kwenye eneo hilo { Maarufu kwa jina la Kigeni Ground Water Floor } nao umechangia kuepusha athari zaidi za kuenea kwa moto huo kwa kutoathiri miti mikubwa.
“ Tumepata faraja kubwa baada ya kuona moto huo uliunguza majani ya chini bila ya kuathiri ile miti mikubwa. Hii inatokana na mazingira ya eneo lenyewe kuwa na unyevunyevu “. Alisema Nd. Afan Othman Maalim.
Alifahamisha kwamba wakulima wa Bonde la Cheju wamekuwa wakitegemea vianzio vya maji vilivyomo kwenye msitu wa Jozani ambavyo vinastahiki kulindwa kwa njia yoyote.
“ Hadhi ya Kimataifa iliyopo katika hifadhi ya Msitu wa Jozani inaweza kupotea iwapo uchafuzi wa mazingira katika eneo hilo hautadhibitiwa “. Alisisitiza Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Kilimo na Mali Asili Zanzibar.
Alisema kuathirika kwa msitu huo mbali ya kuchafuka kwa mazingira katika eneo hilo la hifadhi ya Taifa lakini pia kilimo cha mpunga katika Bonde la Cheju kinaweza kuwa hatarini kutoweka kwa kukosa rasilmali ya maji.
Akitoa shukrani Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameiagiza Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na uongozi wa Serikali ya Mkoa wa Kusini Unguja kuchukuwa hatua za kukabiliana na wagemaji haramu wa asali ili kujaribu kuzuia uharibifu wa mazingira.
Balozi Seif alisema kwa niaba yake na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar amevipongeza Vikosi vya ulinzi kwa kushirikiana na wananchi kutokana na juhudi kubwa walizochukuwa za kufanikiwa kuuzima moto huo.
Alifahamisha kwamba Jozani ikiwa ni miongoni mwa Misitu miwili mikubwa katika Visiwa vya Zanzibar Ukiwepo sambamba na ule wa Ngezi Kisiwani Pemba lazima iendelee kudhibitiwa kwa nguvu zote.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kuwa Idara ya Maafa kwa kushirikiana na Taasisi za Kimataifa itaangalia njia za kufanya utafiti utakaosaidia kutoa taaluma kwa Jamii juu ya kuendelea kuhifadhi rasilimali hiyo ya Taifa.
Naye Mkuu wa Kikosi cha Zimamoto na Uokozi Zanzibar Mkoa wa Kusini Unguja { SSF } Shaaban Ramadhan Ali alisema kikosi hicho bado kinaendelea kukumbwa na changamoto ya vifaa na usafiri katika utekelezaji wa majukumu yake.
SSP Shaaban Ramashan alisema yapo matukio ya maafa yanayotokea katika baadhi ya sehemu ambayo Kikosi chake kinakuwa na mazingira magumu kukabiliana nayo kutokana na miundo mbinu duni.
“ Tunapata matatizo wakati tunapokabiliana na majanga kama moto katika maeneo kama haya kwa kukosa gari zenye kiwango cha maji kinachotosheleza nguvu za kukabiliana na janga halisi “. Alifafanua SSF Shaaban Ramadhan.
Hifadhi ya Taifa ya Msitu wa Jozani imekuwa maarufu kimataifa kutokana na maumbile yake ya kuwa na viumbe mchanganyiko wakiwemo wanyama adimu kama kima punju, Paa Nunga, nguruwe, Vipepeo na aina mchanganyiko ya ndege.