Mkuu wa Wilaya ya Magharibi Nd. Ayoub Moh’d Mahmoud kushoto aliyevaa kanzu na kofia ya Kiua akitoa maelezo mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wa Pili kutoka Kulia kuhusu eneo la Msitu wa Kimaumbile liliopo masingini Dole pamoja na lile ya vianzio vya maji Dole.Kushoto ya Balozi Seif ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Magharibi Nd. Yussuf Moh’f Yussuf.Kulia ya Balozi Seif ni Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Mali Asili Zanzibar Nd. Afan Othman Maalim na Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mh. Mtumwa Kheir Mbarak.Picha na – OMPR – ZNZ.
Na Othman Khamis OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameuagiza Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Magharibi pamoja na taasisi zinazosimamia masuala ya ujenzi kuhakikisha kwamba nyumba zilizojengwa na zinazoendelea kujengwa katika vianzio vya maji vya Dole zinavunjwa haraka iwezekanavyo.
Alisema hatua hiyo ya Serikali imekuja kuzingatia uharibifu unaoonekana kuendelea kufanywa katika vianzio vya maji jambo ambalo ni hatari kwa uchafuzi wa mazingira sambamba na afya za wananchi.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa agizo hilo wakati alipofanya ziara fupi ya kukagua eneo la Msitu wa Kimaumbile liliopo masingini Dole pamoja na lile ya vianzio vya maji Dole linaloonekana kuanza kuvamiwa kwa ujenzi wa nyumba licha ya amri iliyowahi kutolewa na Mamlaka ya Maji Zanzibar { ZAWA } ya kuzuia ujenzi huo.
Alisema uongozi wa Halmashauri hiyo lazima ufanye utaratibu wa kuwahamisha watu wote waliojenga kwenye vianzio hivyo vya maji ili kuendelea kuheshimu ipasavyo maeneo hayo muhimu kwa ustawi wa Jamii.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba Wataalamu wa Kilimo na mazingira wanaruhusu maeneo ya vianzio vya maji kutumika kwa vilimo vya aina mbali mbali kwani havichafui wala kuhatarisha mazingira ya vianzio hivyo.
Mapema Sheha wa Shehia ya Dole Bwana Ibrahim Shaaban Othman alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Mamlaka ya Maji Zanzibar { ZAWA } iliwahi kuweka Mabango ya matangazo kujaribu kusimamisha ujenzi wa aina yoyote kwenye eneo hilo.
Hata hivyo Sheha Ibrahimu alisema kwamba harakati za ujenzi wa nyumba hizo zilizopo mita chache kutoka kwenye kisima hicho cha Dole ziliendelea kama nyengine zikiwa katika hatua ya kukamilika.