Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiweka jiwe la msingi la Bara bara ya ndani ya
Kilomita 3.5 iliyoanzia soko la mboga
mboga Mtaa wa Mombasa hadi Skuli ya Sekondari ya Jang’ombe inayojengwa na
Uongozi wa Jimbo la Mpendae. Nyuma ya Balozi Seif ni Naibu Waziri wa Mindombinu
na Mawasiliano Zanzibar Mh. Issa Haji Gavu na Kushoto ya Balozi Seif ni
Mwakilishi wa Jimbo la Mpendae anayemaliza muda Mh. Moh’d Said Dimwa. Picha na Hassan Issa – OMPR
Wana CCM na Wananchi wa Jimbo la
Mpendae wakimpongeza Mbunge wao Mh. Salim Hassan Turky mwenye kanzu nyeupe kati kati yao kwa uamuzi
wake wa kuwapatia zawadi ya Bara bara ya ndani inayojengwa kwa kiwango cha lami
kutoka Mtaa wa Mombasa hadi Jang’ombe. Picha na Hassan Issa – OMPR
Baadhi ya Wanachama wa Chama cha
Mapinduzi na Wananchi wa Jimbo la Mpendae wakifuatilia matukio mbali mbali
yaliyojiri kwenye hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa bara bara ya
ndani kutoka Mtaa wa Mombasa kwa Mchina hadi
Skuli ya Sekondari ya Jang’ombe. Picha na Hassan Issa – OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif akimpongeza Mbunge wa Jimbo la Mpendae Mh. Salim Hassan
Turky kwa kusimamia vyema utekelezaji wa Ilani ya CCM ndani ya Jimbo lake kwa asilimia 97%. Picha na Hassan Issa – OMPR
Press Release:-
Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewatahadharisha wananchi na
wafuasi wa Vyama vya Siasa kuwa makini katika kuwachaguwa Viongozi
watakaokubali kwa dhati kuwasimamia katika kupambana na changamoto
zinazowazunguuka kwenye maeneo yao.
Alisema
wakati wa kukumbatia watu wanaojali maslahi yao binafsi kwa kukumbuka shida za
Wananchi wakati wa kuomba kura pekee kwa sasa umekwisha na unapaswa kuepukwa
kwa nguvu zote.
Balozi Seif
Ali Iddi alisema hayo wakati alipokuwa akizungumza na Wananchi
pamoja na Viongozi wa Jimbo la Mpendae baada ya kuweka jiwe la msingi la Bara
bara ya ndani iliyoanzia Soko la Mboga mboga
kwa Mchina hadi kumalizikia skuli ya Sekondari ya Jang’ombe.
Bara bara
hiyo ya Kilomita Tatu Nukta Tano
inajengwa kwa gharama zilizotolewa na
Uongozi wa Jimbo la Mpendae zinazokisiwa kufikia Shilingi za Kitanzania
Milioni 1,000,000/- katika kiwango cha Kifusi.
Balozi Seif
alisema kazi ya Mbunge, Mwakilishi na Diwani katika Majimbo na Wadi ni kusimamia utatuzi wa kero zinazoipata
Jamii katika Majimbo husika. Hivyo Wananchi wana wajibu na haki ya kuwauliza
wale wanaoomba ridhaa ya kutaka kuwaongoza watawafanyia nini watapowachagua.
Alifahamisha
kwamba wapo baadhi ya Viongozi wanaoteuliwa na Wananchi kazi yao kubwa ni kupika
majungu pamoja na kuleta malumbano yasiyo na msingi na kusababisha upotevu wa muda badala ya ile kazi
waliyoomba ya kusimamia huduma za
Kijamii.
“ Wapo
baadhi ya Viongozi Majimboni kazi yao kubwa ni kuleta fitna na majungu ndani ya
kipindi chao cha miaka mitano ambao baadaye hurudi tena kwa wananchi kuomba
ridhaa bila ya juhudi zilizoonekana za
kuwaletea maendeleo wananchi waliowachagua “. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif
ameupongeza Uongozi wa Jimbo la Mpendae kwa uamuzi wake wa kuwapatia zawadi
hiyo ya Bara bara Wananchi hao wa Mpendae.
Alisema
ujenzi wa Bara bara unaofanywa na Serikali kwa kushirikiana na washirika wa
Maendeleo wakiungwa Mkono na Viongozi wa Mjaimbo kwa zile bara bara za ndani
lengo lake kuu ni kuwarahisishia Wananchi Usafiri.
Balozi Seif
aliwataka Wananchi watakaoitumia Bara bara hiyo kuendelea kuilinda na kuitunza
ili idumu kwa muda mrefu zaidi kwa vile tayari imeshakuwa mkombozi wao katika
sekta ya mawasiliano ya usafiri wa Bara bara.
Akitoa
Taarifa za ujenzi wa Bara bara hiyo Mbunge wa Jimbo la Mpendae Mh. Salim Hassan
Turky alisema kwamba ujenzi wa Bara bara hiyo ya Mombasa hadi Jang’ombe ni
zawadi maalum iliyoamuwa kutolewa na Uongozi wa Jimbo hilo kwa Wananchi wake.
Mh.
Turky
alisema zawadi hiyo imekuja kufuatia kazi kubwa iliyofanywa kwa pamoja
kati ya Uongozi na Wananchi hao katika kutekeleza Ilani ya uchaguzi ya
CCM ya mwaka 2010 -2015
kwa njia ya amani na utulivu iliyowawezesha
kufikia kiwango kizuri cha asilimia 97%.
Mbunge huyo
wa Jimbo la Mpendae anayemaliza muda wake wa Miaka mitano alieleza kwamba
endapo Wananchi wa Jimbo hilo wataamua kumpa ridhaa tena ya kuliongoza Jimbo
hilo mkazo mkubwa utawekwa katika kubuni miradi ya amali pamoja na kuomba
kibali Serikalini cha ujenzi wa Chuo cha amali iwapo watapatiwa eneo la ardhi.
Alisema
mipango hiyo itakwenda sambamba na ujenzi wa kiwanda cha vibiriti lengo likiwa
ni kujenga fursa za ajira kwa vijana wanaomaliza masomo yao ndani ya Jimbo hilo
pamoja na Majimbo mengine hapa Nchini.
Naye Naibu
Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar Mh. Issa Ussi Gavu alisema kwamba
Serikali kupitia Wizara hiyo itaunga mkono juhudi zinazochukuliwa na Viongozi
wa Majimbo katika ujenzi wa Bara bara za ndani.
Mh. Gavu
alisema katika kuunga mkono jitihada zilizoonyeshwa na Uongozi wa Jimbo la
Mpendae Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano itasaidia kuweka Lami kwenye bara
bara hiyo licha ya kwamba bara bara za ndani zinapaswa kusimamiwa na Viongozi
wa Majimbo.
Bara bara ya
ndani iliyoanzia Soko la Mboga mboga kwa
Mchina hadi kumalizikia skuli ya Sekondari ya Jang’ombe ambayo haikuwamo ndani
ya Ilani ya Uchaguzi ya Jimbo la Mpendae ni zawadi njema, nzuri na ya faraja
iliyotolewa na Viongozi wa Jimbo hilo wanaomaliza muda wao wa utumishi wa miaka
mitano.