Sunday, 5 October 2014

Balozi Seif Akutana na Muwekezaji kutoka Marekani na Balozi wa Heshima wa Tanzania U S A.

 Balozi wa Heshima wa Tanzania Nchini Marekani ambae pia ni Murugenzi wa Kampuni ya Ms Shimoja Dr. Robert Shumake akimtambulisha Makamu wa Rais wa Kampuni ya maendeleo ya ujkenzi ya Detroit Nchini Marekani Bw. Andrew G. McLemore kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi walipokutana kwa mazungumzo VIP ya Uwanja wa ndege wa Pemba.Aliyepo kushoto na Balozi Seif ni Afisa Ubalozi wa Tanzania Nchini Marekani Mh. Suleiman Saleh.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akizungumza na Balozi wa Heshima wa Tanzania Nchini Marekani ambae pia ni Murugenzi wa Kampuni ya Ms Shimoja Dr. Robert Shumake kwenye uwanja wa ndege wa Pemba.(Picha na Hassan Issa OMPR)


Na.AOthman Khamis Ame
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi  Seif Ali Iddi alikuwa na mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Ms Shimoja kutoka Jimbo la Michigan Nchini Marekani Dr. Robert Shumake.
Mazungumzo hayo yamefanyika katika chumba cha watu mashuhuri { VIP } kilichopo kwenye uwanja wa ndege wa Pemba ambapo Balozi Seif aliwasili akitokea Mjini Dodoma baada ya kumalizika kwa Bunge Maalum la Katiba.
Katika mazungumzo yao Mkurugenzi Mkuu huyo wa Kampuni ya Ms Shimoja Dr. Robert Shumake ambaye amepata heshima ya kuwa Balozi wa Heshima wa Tanzania Nchini Marekani alielezea kuridhika na mazingira mazuri ya uwekezaji kisiwani Pemba.
Dr. Shumake alisema Uongozi wa Kampuni yake utaangalia maeneo ambayo inaweza kuwekeza vitega uchumi kama alivyomuahidi Balozi Seif wakati wa ziara yake katika Jimbo la Seattle Nchini Marekani mwaka jana.

“ Muda wangu mfupi niliopata kutembelea maeneo tofauti ya Tanzania ikiwemo Zanzibar umenipa faraja na shauku ya kuangalia fursa zilizopo za uwekezaji na namna  uongozi wa Kampuni yangu utakavyochangamkia fursa hiyo “. Alisema Dr. Robert Shumake.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliuhakikishia Uongozi wa Kampuni hiyo ya Ms. Shimoja kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kuupa msaada wakati unaohitaji kuwekeza hapa Zanzibar.
Balozi Seif alimueleza Dr. Shumake kwamba Zanzibar tayari imetoa fursa kwa wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza miradi na vitega uchumi vyao ili kusaidia kunyanyua pato la taifa sambamba na kuongeza soko la ajira.
Alisema yapo maeneo na sekta ambazo Kampuni ya Ms Shimoja inaweza kuyatumia kuwekeza akiyataja kuwa ni patoja na upanuzi wa uwanja wa ndege wa Pemba, Bandari ya Wete, Sekta ya utalii pamoja na nyumba za mkopo nafuu.
Alifahamisha kwamba miradi ya nyumba za mikopo nafuu kwa kiasi kikubwa inaweza kuwasaidia zaidi vijana wenye ajira mpya  ili wajenge hatma bora ya maisha yao ya baadaye.
Dr. Robert Shumake Mkurugenzi wa Kampuni ya Ms. Shimoja ambae pia ni Balozi wa Heshima wa Tanzania Nchini Marekani alikuwepo Nchini Tanzania kutia saini mkataba wa uanzishwaji wa treni iendapo kwa mwendo wa kasi kati yake na Wizara ya Uchukuzi ya Tanzania.
Treni hiyo itakapokamilika itakuwa ikitoa huduma ya usafiri kati ya Dar es salaamu na pugu kwa kupitia uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Kambarage Nyerere.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
4/10/2014.