Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
akisalimiana na Balozi wa Ujerumani Nchini Tanzania Bwana Egon Kochanke ofisini
kwake vuga Mjini Zanzibar. Picha na
Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
Balozi wa Ujerumani Nchini Tanzania Bwana Egon Kochanke akibadilisha mawazo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif katika jitihada za kuimarisha ushirikiano kati ya Ujerumani na Zanzibar. Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
Balozi wa Ujerumani Nchini Tanzania Bwana Egon Kochanke akibadilisha mawazo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif katika jitihada za kuimarisha ushirikiano kati ya Ujerumani na Zanzibar. Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
Balozi wa Ujerumani Nchini Tanzania Bwana Egon
Kochanke alisema amani na usalama ndio njia pekee na ya msingi itakayoyavusha
salama Mataifa mbali mbali ya Bara la
Afrika katika kuimarisha uchumi na usawi wao.
Bwana Egon alieleza hayo wakati akijitambulisha
rasmi alipokuwa na mazungumzo yake na
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Balozi Egon
Kochanke alisema mataifa mengi ya Bara la Afrika yamekosa fursa ya kuendelea na
harakati za kujiletea maendeleo kwa kukumbwa na wimbi la vurugu na vita.
Alizitolea
mfano Nchi za Somalia, Sudani ya Kusini pamoja na Nigeria ambazo zimekosa
utulivu wa kisiasa kutokana na kukumbwa na vitendo vya uvunjifu wa amani
likiwemo suala la Ugaidi linaloonekana kuitishia amani ya Dunia.
Balozi wa
Ujerumani Nchini Tanzania alipongeza na
kuridhika na mazingira mazuri ya Rasilmali na uwekezaji yaliyomo ndani ya
Visiwa vya Zanzibar jambo ambalo alisema atatumia nafasi yake ya Kidoplomasia
Kuitangaza kwa Makampuni na mashirika ya Uwekezaji vitega uchumi ya Nchini
kwake.
“
Nitachukuwa juhudi kama Balozi kujaribu kuyashawishi Makampuni na Mashirika ya
Kijerumani kulitumia Soko la Zanzibar katika kuendeleza miradi yao kiuchumi na
kibiashara “. Alisema Balozi huyo wa Ujerumani Nchini Tanzania.
Balozi Egon
alifahamisha kwamba Zanzibar inaeleweka vyema Nchini Ujerumani kutokana na
uzalishaji wake wa vyakula na bidhaa za Viungo ambavyo hupendwa na kuwa na watumiaji
wengi duniani.
Katika
kuunga mkono juhudi za Zanzibar katika kujinasua kiuchumi pamoja na kuimarisha
soko la Ajira Balozi Egon alifahamisha kwamba Serikali ya Ujerumani itaandaa
mipango maalum wa kutoa mafunzo ya kazi za amali kwa vijana wa Kizanzibari.
Alisema
mpango
huo utakaoendeshwa Nchini Ujerumani
utajengewa mazingira ya kwenda sambamba na kuwaalika wataalamu wa sekta
mbali mbali Zanzibar kupata fursa ya kutangaza mazingira na vivutio vya
uwekezaji vya Visiwa vya Zanzibar kwa taasisi na makampuni
ya Nchi hiyo.
Akitoa
shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliiomba Ujerumani kuendelea kuiunga mkono
Zanzibar na Tanzania kwa ujumla katika harakati zake za kuimarisha uchumi na
maendeleo ya ustawi wa Jamii.
Balozi Seif
alisema Serikali hivi sasa inaendelea kuimarish miundo mbinu katika sekta mbali
mbali za kiuchumi ikilenga zaidi uimarishaji wa kilimo ambacho huchukua zaidi
ya asilimia 80% ya wananchi wote Nchini
Tanzania.
Alisema ili
kufanikisha sekta hiyo zana za kisasa kama Matrekta yatahitajika katika
kuwawezesha wakulima wengi hasa vijijini kuongeza uzalishaji utaozingatia
taaluma ya kisasa kwa lengo la kuondokana na kilimo cha asili chenye mapato
madogo.
Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar kupitia Balozi huyo wa Ujerumani Nchini Tanzania
aliwaomba wawekezaji, mashirika na
Taasisi za Ujerumani kujenga viwanda mbali mbali vitakavyookoa mazao ya kilimo
mashambani.
Alisema Zanzibar
ni kituo kikubwa cha biashara ndani ya ukanda wa Bara la Afrika ambacho wawekezaji hao
wanaweza kukitumia jambo ambalo pia watapunguza wimbi la ukosefu wa ajira kwa
vijana wengi wanaomaliza masomo yao.