Friday, 16 January 2015

Balozi Seif Achangia saruji mifuko 200 kwa Ujenzi wa Skuli ya Sekondari ya Donge Unguja.

Balozi Seif akimkabidhi mifuko ya saruji 200 Mlezi wa Jumuiya ya Maendeleo Donge Nd. Moh’d Abdulla Khamis akitekeleza ahadi yake hapo skuli ya Sekondari Donge Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akizungumza na Uongozi wa Jumuiya ya Maendeleo Donge pamoja na Wananchi wa Kijiji hicho kwenye hafla kukabidhi mifuko 200 ya Saruji akitekeleza ahadi aliyotoa mwezi mmoja uliopita.kushoto ya Balozi ni Mbunge wa Jimbo la Donge Mh. Sadifa Juma Khamis na kulia yake ni Mlezi wa Jumuiya ya Maendeleo Donge Nd. Moh’d Abdulla Khamis na Mke wa Balozi Seif Mama Asha Suleiman Iddi.
 Mbunge wa Jimbo la Donge Mh. Sadifa Juma Khamis akitoa mchango wa papo kwa papo wa shilingi Milioni 1,000,000/-.Mchango huo ni kuongeza nguvu za upigaji plasta wa madarasa ya Skuli ya Sekondari ya Donge kwenye hafla ya makabidhiano ya saruji iliyotolewa  na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
 Baadhi ya Wzee na Viongozi wa Jumuiya ya Maendeleo Donge  wakimsikiliza Balozi Seif hayupo pichani wakati wa hafla ya kukabidhi saruji kwa uendelezaji wa skuli ya sekondari ya Donge.(Picha na Hassan Issa OMPR)

     
Na Othman Khamis 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewaasa Vijana kuzitumia fursa  nzuri zinazoandaliwa na wazazi wao katika kuwajengea  miundombinu na mazingira bora ya kupata elimu ambayo ndio mzingi pekee utakaowapa manufaa  katika hatma yao ya baadaye.

Alisema elimu ndio rasilmali muhimu kwa vijana katika wakati huu wa mabadilio yanayokwenda na wakati wa  sayansi na teknolojia ulimwenguni kote.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa wasia huo wakati akikabidhi mifuko 200 ya Saruji kwa ajili ya uendelezaji wa ujenzi wa Skuli ya Sekondari ya Donge akitekeleza ahadi aliyoitoa mwezi uliopita wakati akiuzindua Uongozi wa Jumuiya ya Maendeleo Donge.

Akiahidi kuchangia tena shilingi Milioni 2,000,000/- kuunga mkono uendelezaji wa  Jengo hilo katika kazi za upigaji plasta Balozi Seif aliwataka wanafunzi kuacha mchezo na badala yake wapende masomo yao na kuwaheshimu walimu wao ili kupata maendeleo yenye mafanikio.   

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  alisema ameamua kutekeleza ahadi hiyo katika kipindi kifupi  kwa kuthamini umuhimu wa elimu pamoja na kuunga mkono juhudi zinazochukuliwa na  wazazi katika kuekeza kwenye sekta ya taaluma.


Balozi Seif alifahamisha kwamba karne ya sasa imebadilisha mfumo mzima wa elimu ambao kwa njia ye yote mwanafunzi analazimika kufanya jitihada za zaiada katika kutafuta elimu itakayomuwezesha kujijengea mazingira bora ya ajira wakati amalizapo masomo.

“ Karne ya sasa imebadilika kutokana na Darasa la 12 kukosa thamani kwa zaidi ya miaka 20 ambayo inamlazimu kijana kusoma elimu ya ziada  kama anahitaji kuwa na ajira nzuri  “. Alisema Balozi Seif.

Aliwakumbusha vijana kuangalia mambo yatakayowafaa katika maisha yao ya baadaye badala ya kuamua kufuatilia upuuzi unaopenda kuenezwa na watu wajiojikubalisha kupigania ubinafsi.

Balozi Seif alisema wakati umefika kwa jamii kuwatenga watu wanaopita mitaani kushawishi vijana kuwachukia viongozi wao waliojikubalisha kuwaletea maendeo kwenye maeneo yao.

“ Hawa Watu wanaopita pita na kushawishi vijana kuwachukia viongozi wao wanaowasaidia katika harakati zao za kimaendeleo wanafaa kutengwa na Jamii “. Alisema Balozi Seif.

Aliwakumbusha Wazazi na Walezi wa Kijiji cha Donge kuendelea kushirikiana, kupendana pamoja na kushikamana ili kupata nguvu za pamoja katika kujiletea maendeleo yao na vizazi vyao vya baadae.

Mapema Mlezi wa Jumuiya ya Maendeleo Donge Bwana Moh’d Abdulla Khamis amesema wananchi wa Jimbo la Donge wameelezea faraja yao kutokana na kauli ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif ya kutekeleza ahadi yake katika muda mfupi.

Bwana Moh’d Abdulla alisema ahadi ya Balozi Seif ndani ya kipindi cha mwezi mmoja uliopita ameifanya kama Kiongozi anayekereketwa na maendeleo yanayaopatikana katika sekta ya elimu.

“ Si wepesi kwa Viongozi  wengi hapa nchini kuahidi au kutenda jambo la kutaka kusaidia jamii na kulitekeleza kwa muda mfupi “. Alisema Mlezi huyo wa Jumiya ya Maendeleo ya Donge.

Alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Donge Mh. Sadifa Juma Khamis   kwa wepesi wa maamuzi yake katika kusaidia harakati za Wananchi hasa katika sekta muhimu ya Elimu.

Akitoa shukrani kwa niaba ya Wana jumuiya ya Maendeleo Donge pamoja na Wananchi wa Jimbo hilo Mzee Moh’d Rafii alimtaja Balozi Seif kama mfano wa Kiongozi anayetekeleza  agizo la Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete la kuwataka viongozi kufuatilia kero za Wananchi badala ya kukaa maofisini.

Katika makabidhiano hayo ya saruji kwa ajili ya upigaji plasta madarasa ya skuli ya Sekondari ya Donge Mbunge wa Jimbo hilo Mh. Sadifa Juma Khamis alikabidhi mchango wa shilingi Milioni 1,000,000/-  papo hapo kusaidia kazi hiyo.

Mh. Sadifa ambaye tayari ameshakabidhi matofali  Elfu 10,000 kutekeleza ahadi aliyoitoa kwenye Skuli hiyo pia akaahidi kuchangia shilingi Milioni tano zitakazoongeza nguvu za kazi hiyo ya upigaji plasta kwenye skuli hiyo.