Mkurugenzi Uzalishaji Maji wa Mamlaka ya Maji Zanzibar {ZAWA }
Mhandisi Moh’d Elyas aliyenyanyua mkono akimpatia maelezo Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Balozi Seif kazi zilizobakia katika kukamilisha Miundombinu ya
ujenzi wa kisima cha Maji safi katika Kijiji cha Kinduni Wilaya ya Kaskazini
“B”. Picha na Hassan Issa –
OMPR
Balozi Seif akizungumza na Wananchi na wana Saccos wa Kijiji cha
Kinduni baada ya kukagua harakati za ujenzi wa Kibanda pamoja na Kisima cha
Maji katika Kijiji hicho pamoja kutekeleza ahadi aliyotoa kwa kikundi hicho ya
kusaidia matofali na saruji kwa ujenzi wa Jengo lao. Picha na Hassan Issa –
OMPR
Balozi Seif akimkabidhi Mwenyekiti wa Kikundi cha Saccos cha Kijiji cha Kinduni Nd. Abdulla Mihando mchango wa fedha kwa ajili ya ununuzi wa saruji na matofali akitekeleza ahadi aliyoitoa kwa kikundi hicho hivi karibuni. Picha na Hassan Issa – OMPR
Press Release:-
Kisima cha
maji safi na salama kilichochimbwa na
Mamlaka ya Maji Zanzibar {ZAWA } katika Kijiji cha Kinduni Wilaya ya Kaskazini
“B” chenye uwezo wa kuzalisha Maji Lita elfu 80,000 kwa saa kinatarajiwa kuwakomboa
Wananchi wa eneo hilo pamoja na Vijiji vya jirani kupata huduma hiyo muhimu.
Uchimbwaji
wa Kisima hicho utaleta faraja kwa
Wananchi wa Kijiji cha Kindumi ambapo wataondokana na tatizo sugu la
upatikanaji wa huduma hiyo katika muda si mrefu ujao baada kukamilika kwa kazi ndigo ndogo zilizobakia.
Mkurugenzi
wa Uzalishaji Maji wa Mamlaka ya Maji Zanzibar {ZAWA } Mhandisi Moh’d Elyas
alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliyefika eneo hilo
kukagua harakati za ujenzi wa Kibanda cha Maji katika Kisima hicho
aliougharamia kwa lengo la kuwaondoshea tatizo la maji Wananchi hao.
Mhandisi
Moh’d alisema kwamba kazi ya kukamilisha miundombinu iliyobakia katika eneo
hilo inaweza kuchumuwa muda wa wiki moja mara tuu baada ya upatikanaji wa
huduma za umeme katika eneo hilo.
“
Ikipatikana huduma ya Umeme katika Kibanda chetu hichi tuna uwezo wa
kukamilisha kazi iliyobakia ya kuunganisha umeme na mabomba ya maji ndani ya
wiki moja “. Alisema Mhandisi Elyas.
Alisema
wahandisi wa Mamlaka ya Maji watalazimika
kuweka Pampu ndogo kwa wakati huu kulingana na Transfoma iliyopo jirani
na eneo hilo licha ya kwamba kisima hicho kina uwezo wa kusambaza huduma za
maji safi hadi katika Kijiji cha Kinyasini endapo itafungwa Mota kubwa.
Akizungumza
na Wananchi wa Kijiji cha Kinduni pamoja na wana saccos ya Kijiji hicho Balozi
Seif ambae pia ni Mbunge wa Jimbo la Kitope alisema kazi za Wawakilishi na
Wabunge wakati wote ni kuwatumikia Wananchi.
Balozi Seif
alisema katika kutekeleza wajibu huo aliwaahidi Wananchi hao kuchukuwa hatua za
kugharamia usambazaji wa mabomba ya maji katika vitongoji vya Kijiji hicho.
Aliwashukuru
Wananchi wa Kijiji cha Kinduni pamoja na Vitongoji vyake kwa ustahamilivu wao
mkubwa waliouchukuwa wa kukosa huduma hiyo kwa kipndi kirefu.
Katika ziara
hiyo Balozi Seif alikabidhi fedha Taslimu kutekeleza ahadi aliyoitoa hivi
karibuni kwa Kikundi cha Saccos cha Kijiji cha Kinduni ya kuchangia Matofali
pamoja na saruji kwa ajili ya ujenzi wa Jengo la wana saccos hao.
Mapema
Diwani wa Wadi ya Mgambo Bibi Pili Said Mbonde kwa niaba ya Wananchi wa
Kijji hicho amemshukuru Balozi Seif kwa
jitihada zake zilisaidia kuondosha tatizo la miaka mingi la Wananachi hao.
Bibi Pili
alisema ukosefu wa huduma za maji safi na salama kwa takriban miaka Minane katika
eneo hilo umechangia kuviza maendeleo na huduma zao za lazima za kila siku.