Katibu wa Jumuiya ya Wafanyakazi wastaafu Pemba Bwana Majid Moh’d akimkabidhi risala Mkamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwenye hafla ya uzinduzi wa Bodi ya Wadhamini ya Jumuiya hiyo hapo ukumbi wa Tasaf Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Chake chake Pemba.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiizindua rasmi Bodi ya wadhamini ya Jumuiya ya Wafanyakazi Wastaafu Pemba hapo ukumbi wa Tasaf uliopo Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Chake chake Pemba.
Baadhi ya Wajumbne wa Bodi ya Wadhamini ya Jumuiya ya Wafanyakazi Wastaafu Pemba akifutilia Hotuba ya Balozi Seif hayupo pichani wakati akiizindua rasmi.(Picha na Hassan Issa OMPR)
Na Othman Khamis OMPR
Wastaafu wa Taasisi za Umma za Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na zile za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wanapaswa kushirikiana kwa karibu katika kutumia ujuzi na Taaluma zao za muda mrefu ndani ya Jumuiya wanaazozianzisha baada ya kustaafu kwao ili waendelee kuchangia Maendeleo ya Taifa.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akiizindua rasmi Bodi ya wadhamini ya Jumuiya ya Wastaafu Pemba hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Tasaf uliopo katika Majengo ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar yaliyopo Chake chake Pemba.
Balozi Seif alisema mashirikiano hayo yatatoa nafasi nzuri kwa wastaafu hao kuondoa shaka ya kuendeleza maisha yao kwani baadhi yao hupata wakati mgumu kabla na baada ya kustaafu kwa vile wanakuwa bado hawajajipanga.
Alifahamisha kwamba wapo baadhi ya wafanyakazi wa Taasisi za Umma na hata zile binafsi ambao wanaogopa kustaafu wakati utaratibu wa kufanya hivyo upo wazi na sahihi kutokana na muongozo wa Utumishi Serikalini.
“ Tabia hii ya kuogopa kustaafu mara nyingi huwapa wakati mgumu wafanyakazi wanaofikia umri wa kustaafu na baadhi yao bado hawajajipanga “. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliipongeza Jumuiya ya Wastaafu Kisiwani Pemba kwa kuanzisha Bodi ya Wadhamini ambayo itakuwa kiungo muhimu cha uhimili wa Jumuiya hiyo.
Aliwakumbusha wanachama wa Jumuiya hiyo waendelee kushikamana na kuvumiliana wakati wa utekelezaji wa majukumu yao katika njia ya uadilivu, umoja na upendo.
Balozi Seif alieleza kwamba hatua hiyo itasaidia kuondosha dhana potofu zinazoweza kujengwa na baadhi ya wanachama kusingizia uendeshaji mbovu wa Jumuiya katika misingi ya ubaguzi au ubinafsi.
Akitoa Taarifa fupi Katibu wa Jumuiya ya Wastaafu Pemba Bwana Majid Moh’d alisema Jumuiya hiyo iliyoanzishwa mwishoni mwa mwezi wa Mei mwaka 2012 imelenga kuwataka wastaafu wafanye kazi badala ya kubweteka na kuanza tabia ya kuomba omba ambayo haipendezi katika Jamii.
Bwana Majid alisema wana jumuiya ya wastaafu Pemba wamepata faraja kutokana na uongozi imara wa Bodi ya Wadhamini wa Jumuiya hiyo ambao umeonyesha uoni mpana wa kufikiria kubuni mipango na miradi ya kuiendeleza Jumuiya hiyo.
Mapema Afisa Mdhamini Wizara ya Katiba na Utawala Bora Pemba Nd. Omar Khamis Juma alisema Jumuiya ya Wafanyakazi Wastaafu Pemba inafanya kazi kwa umakini kubwa na Wizara hiyo tokea kuasisiwa kwake mwaka uliopita.
Nd. Omar alisema Taasisi hiyo wa wastaafu imekuwa ikitoa msisimko mkubwa kwa wanajumiya wenyewe katika kuendeleza maisha yao wakijaribu kubuni miradi tofauti ya kiuchumi itakayooongeza mapato ya kukidhi mahitaji yao ya kila siku.
Jumuiya ya Wafanyakazi wastaafu Kisiwani Pemba imeanzishwa Tarehe 23 Mei mwaka 2012 na kusajiliwa rasmi mwezi Disemba mwaka 2012.