Balozi Seif akibadilishana mawazo na walimu wa Skuli ya Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Sekondari ya Kinyasini Mkoa wa Kaskazini Unguja
Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Kinyasini Sekondari Haroun Juma akimuonyesha Balozi Seif Vikalio vilivyotengenezwa kwa zege ndani ya madarasa ya Sekondari ya skuli hiyo.
Balozi Seif akishangaa mabadiliko makubwa ya majengo ndani ya Skuli ya Sekondari ya Kinyasini ambapo ndipo alipoanzia kupata elimu ya msingi katika miaka ya 46.
Kushoto ya Balozi Seif ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa Skuli ya Kinyasini Sekondari Nd. Simba Haji.
Balozi Seif akiangalia kisima cha Skuli hiyo ambacho kilipata hitilafu ya mafuta baada ya bomba la mafuta lka kituo cha Petroli kiliopo katibu na skuli hiyo kupasuka na kutembea katika miamba hadi eneo hilo la kisima.
Kushoto ya Balozi Seif ni Mwalimu Mkuu wa Skuli hiyo ya Kinyasini Sekondari Mwalimu Haroun Juma.
Baadhi ya wazazi , walimu na wanafunzi wa skuli ya sekondari ya Kinyasini wakimsikiliza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif baada ya kuitembelea skuli hiyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizunguma na wazazi, kamati ya skuli, walimu na wanafunzi wa skuli ya sekondario ya Kinyasini mara baada ya kukaguzwa kuona maendeleo na chngamoto zinazoikabili.
Picha na Hassan Issa wa –OMPR – ZNZ.
Na Othman Khamis Ame, OMPR
Wazazi wana wajibu na ulazima wa kuhakikisha kwamba watoto wao wanawasimamia vyema katika kupata elimu bora itakayotoa mwanga wa kimaisha katika hatma yao ya baadaye.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitoa nasaha hizo wakati akizunghumza na Uongozi wa Kamati ya Skuli, walimu, Wazazi na Wanafunzi wa Skuli ya Sekondari ya Kinyasini Wilaya ya Kaskazini “A “ mara baada ya kuikagua na kuangalia maendeleo na changamoto zinazoikabili skuli hiyo.
Balozi Seif alisema elimu ndio ufunguo pekee pekee utakaowapa njia watoto hao kukabiliana na mazingira ya kimaisha yanayokwenda kwa kasi na haraka ndani ya mfumo wa sasa wa sayansi na Teknolojia.
“ Wazee wasichoke kuwasomesha watoto wao sambamba na kuwaelekeza kuwaheshimu walimu wao ili kupata baraka na uongofu kutoka kwa walimu wao“. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliipongeza Kamati ya Uongozi ya Skuli hiyo kwa jitihada zake kubwa inazochukuwa kwa kushirikiana na walimu na kuleta maendeleo makubwa.
Alisema mabadiliko ya skuli ya Kinyasini hivi sasa ni makubwa ikilinganishwa na wakati wa enzi zake alipokuwa akisoma kwenye skuli hiyo iliyoasisiwa mwishoni mwa miaka ya 40.
Katika kuipa sifa Skuli hiyo kongwe ndani ya Mkoa wa Kaskazini Unguja Balozi Seif aliwahimiza Wafaunzi wa Skuli hiyo kuwa na dhamira ya kutafuta elimu kwa gharama yoyote ile.
Alisema wanafunzi lazima wawe na nia ya kutafuta elimu hasa ile ya sayansi ambayo bado ina mapungufu katika taasisi za kijamii kwani kuamua kusoma ni wajibu kwao ili kufanikiwa kimaisha.
Alifahamisha kwamba masomo ya sayansi yanayoonekana kupigwa chenga na wanafunzi walio wengi maskulini ndio yanayotoa fursa ya ajira katika ulimwengu huu wa sasa wa Sayansi.
Katika kuwaunga mkono walimu,wazazi na wanafunzi hao wa skuli ya Kinyasini Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliahidi kuchangia Kompyuta mbili pamoja na kuangalia uwezekano wa kusaidia vifaa vya maabara vitakavyowaongezea nguvu ya kukabiliana na masomo hayo.
Mapema Mwenyekiti wa Kamati ya Wazee wa Skuli ya Sekondari ya Kinyasini Nd. Simba Haji alisema Skuli hiyo tayari imeshapea baada ya kuzalisha skuli mbili zinazojitegemea zenyewe ile ya sekondari na ya msingi.
Mwenyekiti Simba alimuomba Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kufuatilia ahadi iliyotolewa na aliyekuwa Waziri Kiongozi wa Mwisho wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kutafuta mbinu za kulitengeneza Jengo la madarasa manne la Skuli ya Msingi ya Kinyasini ambalo liko katika hali mbaya.
Alisema jengo hilo limekuwa likitoa usumbufu kwa wanafunzi wake hasa wakati wa mvua za masika kutokana na paa lake kuwa katika hali isiyoridhisha.
Akimkaribisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuzungumza na wana Kinyasini Hao Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini “ A “ Bibi Riziki Juma Simai alielezea masikitiko yake kutokana na kiwango kidogo cha ufaulu wa wanafunzi wake wanaoingia elimu ya juu.
Bibi Riziki alisema juhudi zinazochukuliwa kila mara baina ya Uongozi wa Skuli, Kamati ya Wazee pamoja na maafisa wa Wilaya hiyo bado hazijaonyesha mafanikio jambo linaonyesha wanafunzi hao bado hawajaamua kujikita katika kutafuta elimu.
“ Mnapaswa kuzingatia zaidi kusaka elimu baada ya tabia mlizozibeza hivi sasa za kuonyesha mchanganyo wa mambo mawili kati ya elimu na starehe mambo ambayo hayaendani sambamba “. Alisema Mkuu huyo wa Wilaya ya Kaskazini “ A “ Bibi Riziki Juma Simai.
Akisoma risala ya walimu, wazazi na wanafunzi wa skuli hiyo ya Sekondari ya Kinyasini Mwalimi Mseme Hassan alisema zipo baadhi ya changamoto zinazoikabili skuli hiyo zenye kupunguza kasi ya masomo kwa wanafunzi wao.
Mwalimu Mseme Hassan alizitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na suala la uzio kwa skuli ya msingi,ukosefu wa walimu wa sekondari , vifaa vya maktaba na vikalio kwa skuli ya sekondari.
Skuli ya Kinyasini ikiwa ni miongoni mwa skuli kongwe ndani ya Mkoa wa Kaskazini Unguja iliasisiwa mnamo mwaka 1946 kwa Darasa la Quran na kuanza kwa darasa la kwanza mwaka 1947 lililoendelea hadi darasa la kumi na moja kwamba 1973.