Thursday, 8 January 2015

Balozi Seif aweka jiwe la Msingi Maktaba Kuu , Chakechake



MAKAMO wa pili wa Rais wa Zanzibar Mhe:Balozi Seif Ali Iddi, akikunjuwa kitambaa kuashiria uwekaji wa jiwe la Msingi maktaba kuu ya chake chake Pemba, ikiwa ni shamra shamra za miaka 51 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar.(Picha na Abdi Suleiman, PEMBA.)


MKUU wa makoa wa kusini Pemba, Mhe:Mwanajuma Majid Abdalla akizungumza na wanafunzi,walimu na wananchi wa Chake Chake, mara baada ya kuwekewa jiwe la msingi maktaba kuu ya Chake Chake.(Picha na Abdi Suleiman, PEMBA.)


NAIBU waziri wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe:Zahra Ali Hamad, akizungumza na wanafunzi walimu na wananchi wa Chake Chake, mara baada ya kuwekewa jiwe la msingi maktaba kuu ya Pemba.(Picha na Abdi Suleiman, PEMBA.)

MAKAMO wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe:Balozi Seif Ali Iddi, akizungumza na wananchi wa Chake Chake mara baada ya kuiwekea jiwe la msingi maktaba kuu ya Pemba .(Picha na Abdi Suleiman, PEMBA.)

Shirika la huduma za Maktaba lashauriwa kufikisha huduma vijijini


Na Othman Khamis Ame, OMPR
Shirika la huduma za Maktaba Zanzibar limetakiwa kuangalia uwezekano wa  kuzidisha kasi ya majukumu yake katika kupeleka huduma za maktaba Vijijini ili wananchi waweze kuongeza maarifa yanayokwenda sambamba na mahitaji ya maisha yao.
Wito huo umetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa Jengo la Maktaba Kuu ya Zanzibar Tawi la Pemba hapo Mtaa wa Chachaani Mjini Chake chake Pemba ikiwa ni muendelezo wa shamra shamra za maadhimisho ya kusherehekea kutimia miaka 51 ya Mapinduzi Matukufu wa Zanzibar ya Mwaka 1964.
Balozi Seif alisema anaelewa juhudi zinazochukuliwa na shirika la huduma za Maktaba Zanzibar lakini kasi hiyo ni vyema kwa hivi sasa ikaelekezwa zaidi vijijini kwa vile wananchi wengi wanaoishi katika maeneo hayo hawana fursa za kutosha za kujisomea na kujiendeleza.
Alisema hivi sasa huduma nyingi za maktaba zinapatikana zaidi katika maeneo ya miji ambako watu wengi wana maarifa pamoja na vyanzo mbadala vya kupata huduma hiyo kwa kujisomea na kuongeza maarifa yao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba Serikali imefanya juhudi za kuongeza maktaba ikifahamu kwamba eneo hilo ni muhimu kwa  kuweza kuwapatia wananchi maarifa mbali mbali ya fani tofauti.

Balozi Seif alitoa wito kwa wananchi wa Kisiwa cha Pemba kujenga utamaduni wa kujisomea vitabu, magazeti na majarida tofauti kwa lengo la kuongeza maarifa mapya yatakayowasaidia katika maisha yao lakini 
pia
 ni sehemu ya kujiburudisha.
Alisisitiza kwamba elimu bora haipatikani madarasani tu bali pia maktaba ina mchango mkubwa katika kuwawezesha kupata elimu iliyo bora. Hivyo amewahimiza wanafunzi kuitumia fursa waliyoipata ya kuitumia maktaba ili kupata maarifa za ziada.
Alieleleza kwamba kupanuka kwa huduma za elimu hakuna budi kwenda sambamba na upatikanaji wa miundombinu na nyenzo mbali mbali za elimu ikiwemo huduma za maktaba za kisasa.
Alisema pamoja na wanafunzi kwenda skuli na kujifunza lakini bado kuna haja kubwa sana kwa wao kupata taaluma zaidi ya ziada kwa lengo la kujiongezea maarifa ili kukuza kiwango chao cha elimu.
Alieleza kwamba Serikali imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kueneza huduma za elimu katika maeneo mbali mbali Unguja na Pemba mijini na vijijini na hili linadhihirika wazi kutokana na ongezeko kubwa la Skuli 279 za maandalizi, msingi 250, msingi na kati 109 na sekondari 147.
“ Mwaka 1964  wa Serikali ya Mapinduzi ya  Zanzibar wakati inaanza kuongoza baada ya kufanya Mapinduzi ilikuwa na skuli 62 tu za msingi na skuli 4 tu za sekondari wakati elimu ya vyuo vikuu wanafunzi walilazimika kuvuka maji kwenda Tanzania bara au nchi za Ulaya “. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaasa wananchi na watu wote watakaotumia maktaba hiyo kuhakikisha kwamba wanaitunza pamoja na vifaa vyake vyote ili lengo la kuwepo kwake  lifikiwe na kuchangia maendeleo ya elimu.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliipongeza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali pamoja na Bodi ya huduma za Maktaba kwa juhudi za kufikishia huduma za maktaba karibu na wananchi na kuwashauri waongeze nguvu za kuweka mataba kila Wilaya Unguja na Pemba.
Mapema akisoma risala yenye mnasaba na shughuli hiyo ya Maktaba Kuu ya Zanzibar Tawi la Pemba Msaidizi Mkutubi Mkuu wa Maktaba hiyo Bibi Mwache Moh’d alisema ujenzi wa jengo la Maktaba hiyo ulioanza mwezi Septemba mwaka 2013 tayari umeshafikia asilimia 90%.
Bibi Mwache alisema ujenzi huo unaotarajiwa kukamilika na kutoa huduma za Maktaba kwa wanafunzi, wataalamu na wananchi  mwezi ujao umezingatia pia mahitaji ya watu maalum kama wale wenye ulemavu, watoto wadogo pamoja na watu wazima.
Msaidi Mkutubi Mkuu huyo wa Huduma za Maktaba Tawi la Pemba ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  kwa kugharamia ujenzi huo utaofikia jumla ya shilingi Milioni 655,000,000/- ambapo huduma za kijamii zitakuwa zimesogezwa kwa Wananchi.
Hata hivyo Bibi Mwache Moh’d alisema bado Shirika la Huduma za Maktaba Kuu Zanzibar Tawi la Pemba linaendelea kukabiliwa na baadhi ya changamoto akiitaja sugu zaidi kuwa ni suala la usafiri.
Alisema Watendaji wa Shirika hilo wanashindwa kutekeleza vyema majukumu yao kutokana na ukosefu wa huduma za usafiri jambo ambalo linawanyima fursa za kutoa na kufuatilia huduma za Maktaba katika Wilaya na Maskuli mbali mbali Kisiwani humo.
Naye Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Zahra Hamad alisema Wizara hiyo hivi sasa imejikita kuelekeza nguvu zake katika ujenzi wa Maktaba za Wilaya ili kuwajengea utamaduni wa kupenda kusoma Wanafunzi na  Wananchi wa maeneo yote Mjini na Vijijini.
Mh. Zahra alisema ujenzi huo ulio chini ya mradi wa I.G.P utakwenda sambamba na ununuzi wa Mabasi yatakayoliwezesha shirika la Huduma za Maktaba kutoa huduma za Maktaba hadi Vijijini.
Alisema Wizara  ya Elimu hivi sasa inaendelea na juhudi za kusomesha wakutubi kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar {SUZA } pamoja na Shirika la Huduma za Maktaba ili kukabiliana na uhaba wa wakutubi  uliopo katika Wilaya na Skuli mbali mbali za Zanzibar.
Mh. Zarha alifahamisha kwamba shirika hilo kwa kushirikiana na Wizara na SUZA tayari limeshawapatia mafunzo  tofauti wakutubi mia mbili na ishirini na saba ngazi ya Stashahada, 75 ngazi ya Cheti pamoja na 25 kushiriki  semina mbali mbali.