Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akifunga Mkutano wa 17 wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar
uliokuwa ukiendelea katika Ukumbi wa Baraza hilo uliiopo Mbweni Nje kidogo ya
Mji wa Zanzibar. Picha na Hassan Issa wa
– OMPR – ZNZ.
Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanbzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
imekusudia kuendeleza utafiti pamoja na utoaji wa huduma za ufuatiliaji kwa wazalishaji
wa sekta za mifugo na uvuvi, ili wazalishaji
hao wawe na uwezo wa kupata faida kubwa,
jambo ambalo litawafanya wananchi wengine hasa vijana kuendelea kujiajiri
katika sekta hizo muhimu.
Alisema dira ya
Serikali kuhusu Sekta ya Mifugo na Uvuvi ni kuibadililisha Sekta hiyo kutoka
katika mfumo wa uzalishaji wa kujikimu hadi kufikia kilimo cha biashara ifikapo
mwaka 2020.
Balozi Seif alisema
hayo wakati akifunga Mkutano wa 17 wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar uliokuwa
ukiendelea katika Ukumbi wa Baraza hilo uliiopo Mbweni Nje kidogo ya Mji wa
Zanzibar.
Alisema azma hiyo itafikiwa kwa mkakati wa kuimarisha hali ya
uchumi na kijamii kwa wazalishaji wa mifugo na wavuvi kuwekewa mazingira mazuri
ya utekelezaji, kupatiwa huduma za kitaalamupamoja
na kuongeza thamani na upatikanaji wa
taarifa za masoko ili kuongeza uzalishaji na kipato.
Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar alifahamisha kwamba ongezeko kubwa la mahitaji ya soko la utalii
nchini ambalo ni mtumiaji mkubwa wa bidhaa za mifugo na samaki, sambamba na
ongezeko la watu mijini limesaidia kukua kwa sekta ya mifugo na uvuvi nchini kulikosababisha
kuimarika kwa soko la ndani.
“ Suala la utafiti ni
kikwazo kwa sekta zetu hizi, kuanzishwa kwa idara ambayo pia inasimamia suala
la utafiti haitoshi, bali kuwepo kwa taasisi zinazojitegemea kushughulikia
utafiti kisekta ndio njia pekee ya kuweka mazingira mazuri katika masuala ya utafiti “. Alisema Balozi Seif.
Alifahamisha kwamba Serikali tayari imo katika mpango wa kufanikisha suala zima
la vituo vya utafiti kwa kuanzia na sekta ya uvuvi kwa kushirikiana na Serikali
ya Jamuhuri ya Watu wa China pamoja na Kampuni ya KOICA kutoka Japani.
Alisema Serikali imo katika kuandaa mpango wa kuanzisha Chuo cha Uvuvi hapa
Zanzibar kitakachosaidia taaluma kwa vijana kwa lengo la kupata ajira kupitia
shughuli za uzalishaji mifugo na uvuvi licha ya kwamba sekta hizo zimekuwa
muajiri mkubwa wa vijana
Balozi Seif alieleza kwamba mazingira mazuri ya kisera, sheria, kanuni na
miongozo yataandaliwa ili kuifanya sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika
kuendeleza sekta endelevu, ufugaji wa ng’ombe pamoja na uwekezaji wa viwanda
vya usarifu wa samaki na mifugo bila kuathiri mazingira.
Akigusia Kilimo
Balozi Seif alisema SDekta hiyo inaendelea kuwa ni muhimili
mkuu wa uchumi wa Zanzibar ambapo inatoa mchango wa moja kwa moja katika
kujikimu kimaisha, kuwa na uhakika wa chakula, lishe na afya za wananchi walio
wengi vijijini na mijini.
Alisema takriban zaidi ya asilimia 70 ya wananchi wote hapa nchini wanategemea
sekta ya Kilimo kwa kuendeleza maisha yao ambapo takwimu zinaleza wazi kwamba kwa
mwaka wa fedha 2012/2013 sekta hii
ilichangia wastani wa asilimia 30 ya Pato la Taifa.
Balozi Seif alisema kwa Msimu wa Kilimo cha Mpunga cha Masika 2013/2014, jumla ya ekari 30,444 Unguja na Pemba
zililimwa katika maeneo ya juu, sawa na
asilimia 87 na ekari 1,736
zililimwa katika maeneo ya umwagiliaji maji sawa na asilimia 88 ya lengo
lililowekwa.
Kuhusu suala la
amani Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Serikali itaendelea kwa juhudi
zake zote kusimamia amani na utulivu iliyopo na ni vyema viongozi na wananchi wakaongeza
ushirikiano katika kufanikisha azma hii.
Alisema Taifa
linajivunia
hazina kubwa iliyojaliwa na Mwenyezi Mungu ya amani na utulivu ambayo ni nyenzo
kubwa kwa ustawi na maendeleo ya nchi nchi hii. Hivyo, hakuna budi kwa kila
mmoja kuilinda na kuidumisha hazina hiyo kwani ikivurugika hakuna hata mmoja
miongoni mwetu mwa jamii atakaebaki salama.
Aliwahakikishia Waheshimiwa Wajumbe kwamba Serikali chini ya uongozi mahiri
wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt. Ali
Mohamed Shein itajitahidi kuhakikisha kwamba inaimarisha utendaji na
uwajibikaji katika Serikali na kuendelea kudumisha amani na utulivu.
Miswada minne ya Sheria katika
Mkutano wa 17 wa Baraza hilko la Wawakilishi Zanzibar na
kujadiliwa yakiwemo mawasli 48 ya wajumbe wa Baraza hilo yalijibiwa yakifuatiwa
na maswali mengine 100 ya nyongeza.
Miswaada hiyo ni ule Mswada
wa Sheria ya kufuta Sheria ya Wauguzi na Wakunga (uanzishwaji wa Baraza la
Usajili wa Wauguzi na Wakunga) Nam. 9 ya mwaka 1986 na kuanzisha badala yake
Sheria mpya ya Wauguzi na Wakunga na Mambo Yanayohusiana na Hayo.
Mwengine ni Mswada wa Sheria ya
Kuanzisha Shirika la Nyumba la Zanzibar, Mswaada wa Sheria ya Baraza la
Manispaa Nam. 3 ya mwaka 1995 na Halmashauri za Wilaya na Mabaraza ya Miji Nam.
4 ya mwaka 1995 na kuanzishwa upya Sheria ya Mamlaka za Serikali za Mitaa ya
mwaka 2014 kwa madhumuni ya kuanzisha Serikali za Mitaa, uwezo wake, kazi na
wajibu, muundo, mpangilio, fedha na Mambo Mengine Yanayohusiana na Hayo.
Mswada wa Nne uliowasilishwa
unahusu kufuta Sheria Nam. 1 ya Tawala za Mikoa ya Mwaka 1998 na kuanzisha
Sheria mpya ya Tawala za Mikoa ya Mwaka 2014 na Mambo Mengine yanayohusiana na
Hayo.
Baraza la
Wawakilishi Zanzibar limeahirishwa hadi
siku ya Jumatano, tarehe 21 Januari, 2015 saa 3.00 asubuhi.