Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa katika picha ya pamoja na Vongozi wa Dini mbali mbali Nchi mara baada ya kufanya mazungumzo nao Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar. Kushoto ya Balozi Seif ni Kiongozi wa Timu ya Waislamu Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Kabi na Kulia ya Balozi ni Kiongozi wa Wakristo Askofu Augustino Mweleli Shao. Picha Hassan Issa – OMPR – ZNZ.
Press Release:-
Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar inakamilisha taratibu zilizobakia na tayari
inajiandaa kuwachukulia hatua za Kisheria watu wote waliohusika kuharibu
kwa makusudi zoezi zima la Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliofanyika Tarehe
25 Mwezi Oktoba mwaka huu.
Kauli
hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi wakati akizungumza na Viongozi wa Dini mbali mbali Nchini
aliokutana nao Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar kutafakari na kutafuta
mbinu za kuendelea kujaribu kudumisha amani ya Nchi iliyotetereka na
kuleta mtafaruku katika kipindi hicho cha Uchaguzi.
Balozi
Seif alisema ina uthibitisho kamili wa vielelezo vya ushahidi wa
udanganyifu kwa maeneo yote ya Zanzibar hasa katika Majimbo ya Uchaguzi
ya Kisiwa cha Pemba.
Alisema
Afisa wa Tume ya Uchaguzi au Mtu yoyote aliyehusika na udanganyifu huo
aelewe kwamba mkondo wa sheria utamkumba kwa vile vitendo walivyofanya
wameisababishia hasara kubwa Serikali pamoja wa washirika wa maendeleo
walioamua kusaidia uchaguzi huo.
Balozi
Seif alibainisha kwamba wakati wahusika hao wanapandishwa katika
vyombo vya kisheria kujibu shutuma zinazowakabili Serikali kwa upande
wake itaweka hadharani uthibitisho kamili wa vielelezo vya ushahidi wa
udanganyifu huo ili Wananchi wapate fursa ya kuelewa dhambi hiyo mbaya
waliyofanyiwa na watu wachache kwa tamaa binafsi.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwahakikishia Viongozi hao wa Dini kwamba
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejipanga vizuri kupitia vyombo
vyake vya ulinzi kwa kupiga Doria maeneo yote katika kuona amani ya nchi
inaendelea kudumu.
Aliwapongeza
Viongozi hao wa Dini kwa jitihada zao wanazochukuwa za kutumia busara
zao kwa kukutana na Viongozi wa pande mbali mbali za Kisiasa wakilenga
kusaidia kutuliza mumkari na machungu ya waumini wao ambao takriban wote
ni wafuasi wa vyama vya Kisiasa vilivyopo hapa Nchini.
Alivilaumu
baadhi ya vyombo vya Habari hasa vile vya Nchi za Magharibi jinsi
vilivyoonyesha wazi Taarifa zao nyingi wanazotowa za zoezi zima la
uchaguzi Mkuu wa Zanzibar zikionyesha kuegemea upande mmoja tu.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar alielezea masikitiko yake juu ya wangalizi
wa Kimataifa walioamua kufuatilia uchaguzi Mkuu wa Zanzibar kwamba
hawakwenda Kisiwani Pemba muda wote wa zoezi la kupiga kura kufuatilia
changamoto zilizojitokeza katika majimbo ya Pemba.
"
Nimesikitishwa na waangalizi wa Kimataifa waliokuwepo Zanzibar kwa
karibu mwezi mmoja kufuatilia kampeni na uchaguzi wake wameshindwa
kwenda Pemba wakati wa zoezi la kupiga kura na kuonekana zaidi katika
majimbo ya Kisiwa cha Unguja.
Balozi
Seif aliishauri Idara ya Habari Maelezo kuendelea kufuatilia Taarifa
zinazotolewa na vyombo mbali mbali vya Habari ndani na nje ya Nchini na
kukemea au kutoa Taarifa dhidi ya uchochezi unaotolewa na vyombo hivyo.
Nao
Viongozi hao wa Dini mbali mbali Nchini wameishukuru na kuipongeza
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ile ya Jamuhuri ya Muungano wa
Tanzania kwa hatua iliyochukuwa katika kusimamia amani ya Nchi.
Wananchi
wa Zanzibar wamerejea katika harakati zao za kawaida za kimaisha
baada ya kutokea hitilafu tofauti ndani ya zoezi zima la upigaji kura
kwenye uchaguzi Mkuu wa Tarehe 25 Mwezi uliopita na kupelekea kuibuka
kwa mtafaruku uliotikisa amani ya Taifa.