Haiba ya eneo la mbele la Kituo cha Mafunzo ya Aamali kiliopo
Mkokotoni Mkoa wa Kaskazini Unguja ambacho hufundisha vijana waliomaliza masomo
yao ya Kidatu cha Nne katika fani mbali mbali za ujasiri amali. Picha na Hassan Issa –
OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa
pamoja na Uongozi wa Wizara ya Elimu akitembelea majengo ya Kituo cha Mafunzo
ya Amali kilichopata vifaa vipya vya
kufundishia vilivyotolewa msaada na Serikali ya Jamuhuri ya Kiislamu ya Iran. Picha na Hassan Issa –
OMPR
Mkuu wa Kituo cha Mafunzo ya Amali Mkokotoni Maalim Mkubwa Khamis Ibrahim
wa mwanzo kutoka kushoto akimtembeza Balozi Seif aliyepo kati kati kwenye
maeneo tofauti ya Kituo hicho baada ya kupata vifaa vipya vya kufundishia. Picha na Hassan Issa –
OMPR
Mkuu wa Kituo cha Amali Mkokotoni Maalim Mkubwa akimpatia maelezo Balozi
Seif jinsi chuo hicho kitakavyokuwa na uwezo wa kutengeneza vyombo vya moto kwa
mfumo wa kisasa wa Kompyuta. Picha na Hassan Issa –
OMPR
Balozi Seif akionekana kufarajika
baada ya kuonamashine za kisasa za kutengenezea thamani za ofisini na
majumbani zilizomo ndani ya Kituo cha Amali Mkokotoni. Picha na Hassan Issa –
OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiwapongeza walimu wa
Kituo cha Amali Mkokotoni kwa kazi kubwa ya kuwafinyanga vijana katika
mazingira ya muelekeo wa kuweza kijitegemea wenyewe badala ya kusibiri ajira za
Serikali. Kulia ya
Balozi Seif ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mheshimiwa Ali Juma
Shamuhuna.
Picha na Hassan Issa – OMPR
Picha na Hassan Issa – OMPR
Press
Release:-
Ile dhamira ya Serikali ya Mapin duzi ya Zanzibar
kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali
Zanzibar ya kuanzisha mafunzo ya
Amali ili kuwapa fursa ya uhakika Vijana kupambana na changamoto zinazowakabili
za ajira Nchini imeanza kuonyesha muelekeo wa matumaini.
Muelekeo huo wa matumaini unafuatia Kituo cha
Mafunzo ya Amali kiliopo Mkokotoni Mkoa wa Kaskazini Unguja kupokea Vifaa mbali mbali vya kisasa vya masomo vilivyotolewa
msaada ya Serikali ya Jamuhuri ya Kiislamu ya Iran.
Vifaa hivyo vikiwemo vile vya Ufundi wa Magari,
Fanicha cha Maofisini, Mafriji,
Televisheni na Matrekta vinakadiriwa kugharimu Dola
Laki Tano { 500,000 } za Kimarekani sawa na zaidi ya shilingi Bilioni
Moja za Kitanzania.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi alipata fursa ya kufanya ziara fupi kuangalia vifaa hivyo ambavyo baadhi
yake tayari vimeshaanza kutumiwa na Wanafunzi wa Kituo hicho.
Mkuu wa Kituo cha Mafunzo ya Amali Mkokotoni Maalim
Mkubwa Khamis Ibrahim alimueleza Balozi Seif kwamba Uongozi wa Kituo hicho kwa
Kushirikiana na Wizara ya Elimu unafanya juhudi za kuwapata wataalamu
waliobobea watakaosaidia kutoa mafunzo kwa walimu wa Kituo hicho waweze kudumu
kuvitumia kwa kuwafundisha Wanafunzi wao.
Maalim Mkubwa alisema vipo vifaa vya kutengenezea
vyombo vya moto vinavyotumia mfumo wa Kisasa wa Komyuta ambavyo watumiaji wake
watalazimika kupata taaluma ya kina.
Akitoa Taarifa kamili ya Kituo hicho baada ya ziara
hiyo Maalim Mkubwa Khamis Ibrahim alisema lengo la kuanzishwa Kituo hicho
karibu miaka mitatu iliyopita ni kuwapatia mafunzo ya Amali Vijana baada ya
kukosa kuendelea na mafunzo yao ya Sekondari.
Alisema Kituo hicho hivi sasa kinafundisha Fani 11
zinazomjengea uwezo wa kujiajiri mwenyewe Mwanafunzi baada ya kumaliza mafunzo
yake ya miaka Mitatu akizitaja baadhi ya fani hizo kuwa ni pamoja na Ufundi
Magari, Uashi, Uchongaji, Friji,umeme, bomba, uchoraji pamoja na Mapishi.
Maalim Mkubwa alifahamisha kwamba wakati Kituo kiko mbioni kufunga vifaa vya
mawasiliano ili kwenda katika mfumo wa kisasa mkakati mkubwa wa miaka Mitano
umeandaliwa katika kuwawezesha wanafunzi wanaomaliza mafunzo yao kufanya
Mtihani wa Veta ili kuwajengea uwezo wa elimu wanayoipata ikubalike Kitaifa.
Alifahamisha kwamba mkakati huo umeshasaidia Vijana
kadhaa waliopitia Kituo hicho ambao kwa
sasa idadi yao imefikia 180 na wengi kati yao wameshaajiriwa katika Taasisi
mbali mbali za Umma na hata zile binafsi za ndani ya nje ya Nchi.
Akizungumzia mtazamo wa baadae wa Kituo hicho cha
Mafunzo ya Amali Mkokotoni Mkuu wa Kituo hicho Maalim Mkubwa alisema kwamba
mpango unaandaliwa wa kuwapatia mafunzo Kituoni hapo wanafunzi wanaomaliza
Kidato cha Pili.
Alisema mkazo utawekwa wa kuwapatia mafunzo Vijana hao
ya jinsi ya kuendesha Biashara chini ya Shirika la Kazi la Umoja wa Mataifa {
ILO } kwa Vile Vijana hao wapatao 6,000
wanaomaliza masomo kila mwaka hivi sasa hawaajiriki.
Akitoa shukrani zake kwa juhudi kubwa inayochukuliwa
na walimu wa Kituo hicho katika kuwafinyanga wanafunzi hao Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema wakati umefika kwa kila mwana jamii
kujifunza kazi yoyote ya amali itakayomuwezesha kuongeza mapato yake na
kujikimu Kimaisha.
Alisema hatua hiyo kwa uande mwengine itasaidia pia kuipunguzia
mzigo Serikali Kuu kwa kuagiza baadhi ya vifaa nje ya Nchini ambavyo kama jamii
itajipanga vyema vinaweza kutengenezwa hapa hapa Nchini.
Makamu wa ili wa Rais wa Zanzibar alilipongeza wazo
la busara la Uongozi wa Kituo hicho cha Mafunzo ya Amali la kuwaandalia mafunzo
Wanafunzi wanaomaliza Kidato cha Pili.
Balozi Seif aliushauri Uongozi wa Kituo hicho kwa
Kushirikiana na Wizara ya Elimu kwamba ni vyema wanafunzi wanaomaliza mafunzo
yao kusaidiwa vifaa vitakavyowapa hamasa ya kuipenda kazi yao wakati watapoamua
kujiajiri katika maeneo yao.
Alisema Serikali Kuu inaweza kusaidia kukiwezesha
Kituo hicho kununua vifaa hivyo ikiwa kama zawadi kwa kufanikisha vyema
mafunzo yao na kianzio kizuri cha mwanzo wa maisha yao.
Mapema Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar
Mheshimiwa Ali Juma Shamuhuna alisema vifaa hivyo ni ahadi iliyotolewa na Serikali ya Jamuhuri
ya Kjiislamu ya Irani karibu Miaka mitatu iliyopita.
Waziri Shamuhuna alisema Kituo cha Mafunzo ya Amali
Mkokotoni kilikuwa na upungufu wa vifaa vya mafunzo tokea kilipoanzishwa miaka
Mitatu iliyopita ambapo zile ndoto
zilizokuwa zikiotwa na Walimu na Wanafunzi wa Kituo hicho sasa zimetimia.
Alisema
Walimu wa Kituo hicho sasa watakuwa na uwezo na shauku kubwa ya
kusomesha kwa juhudi na maarifa baada ya kupata vifaa tofauti vitakavyokuwa
chachu ya matumaini katika siku zijazo.