Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya
Ushauri wa Uhandisi katika miundombinu ya ujenzi, usarifu wa Miji, Majengo ya
Kisasa pamoja na Vituo vya Kimataifa vya Biashara { ECG } ya Nchini Misri
Mhandisi Amri Alouba akimuonyesha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
michoro iliyotengenezwa na Wataalamu wa
ECG ya jinsi linavyoweza kujengwa eneo la Darajani na kuwa katika mazingira ya
Biashara ya Kimataifa. Picha na Hassan Issa –
OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na
Wafanyabiashara pamoja na wataalamu wa ushauri wa Uhandisi kutoka Nchini Misri
waliopo Tanzania kuangalia maeneo ambayo wanaweza kuwekeza miradi ya Kiuchumi. Picha na Hassan Issa –
OMPR
Meneja wa Biashara wa Kampuni ya
Kimataifa ya AIKAN ya Nchini Misri Bwana
Mohammed Alef Sherief wa kwanza
kutoka kushoto akimfahamisha Balozi Seif hayupo pichani fursa zinazotolewa na
Taasisi yake katika kuwajengea Vijana uwezo wa kufanya Biashara. Picha na Hassan Issa –
OMPR
Balozi Seif katika Picha ya pamoja na Wafanyabiashara na wataalamu
wa ushauri wa Uhandisi kutoka Nchini Misri mara baada ya kufanya mazungumzo nao
Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar. Kushoto ya
Balozi Seif ni Makamu Mwenyekiti wa
Taasisi ya Ushauri wa Uhandisi katika miundombinu ya ujenzi, usarifu wa Miji,
Majengo ya Kisasa pamoja na Vituo vya Kimataifa vya Biashara { ECG } ya Nchini
Misri Mhandisi Amri Alouba na Balozi wa
Tanzania Nchini Misri Balozi Mohammed Hamza. Kulia ya
Balozi Seif ni Mtaalamu wa Taasisi ya Ushauri wa Uhandisi katika miundombinu ya
ujenzi, usarifu wa Miji ya ECG Mhandisi Sherif Meurad pamoja na Meneja wa
Biashara wa Kampuni ya Kimataifa ya
AIKAN ya Nchini Misri Bwana Mohammed
Alef Sherief. Picha na Hassan Issa –
OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akizungumza na Balozi
Mdogo wa Oman aliyepo Zanzibar Bwana Ali Abdullah Ofisini kwake Mtaa wa Vuga
Mjini Zanzibar. Picha na Hassan Issa –
OMPR
Press Release:-
Taasisi ya
Ushauri wa Uhandisi katika miundombinu ya ujenzi, usarifu wa Miji, Majengo ya
Kisasa pamoja na Vituo vya Kimataifa vya Biashara { ECG } ya Nchini Misri
imeamua kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika azma yake ya
kusaidia Uchumi wa Zanzibar na ustawi wa Wananchi wake.
Kiongozi wa
Ujumbe wa Wafanyabiashara wa Misri wanaotembelea Tanzania kuangalia maeneo
wanayoweza kushirikiana na Serikali katika uwekezaji Mhandisi Amr Allouba
alisema hayo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi
Seif Ali Iddi Ofisi kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Mhandisi
Amri Allouba ambae pia ni Makamu
Mwenyekiti wa Taasisi hiyo ya
uhandisi ya { ECG } alisema Wataalamu wa Taasisi hizo wako tayari
kuelekeza nguvu zao ndani ya ukanda wa Afrika ya Mashariki, Zanzibar ikiwa
miongoni mwake kutokana na mazingira mazuri ya rasilmali pamoja na uwekezaji.
Makamu
Mwenyekiti huyo wa Taasisi ya Uhandisi ya ECG alisema Wataalamu wa Taasisi hiyo
tayari wameshaandaa michoro ya jinsi linavyoweza kujengwa eneo la Darajani na kubadilishwa
kuwa katika mazingira ya kisasa ya Biashara
ya Kimataifa.
Mhandisi Amr
alifahamisha kwamba eneo hilo la Darajani upande wa iliyokuwa kituo cha Dala
dala pamoja na Makontena linaweza kujengwa Vituo vya Biashara bila ya kuathiri
mipango Miji iliyowekwa katika Mji Mkongwe wa Zanzibar ambao umo katika urithi
wa Kimataifa.
Alieleza
kwamba mradi huo endapo unaweza kukubalika na Serikali ujenzi wake unaweza kuchukuwa miezi 12 hadi 18 baada ya
kukamilika kwa michoro husika itayozingatia taratibu za Shirika la Umoja wa
Mataifa linalosimamia masuala ya
Sayansi, Elimu na Utamaduni { Unesco } linalohusika na hifadhi ya Mji
Mkongwe wa Zanzibar.
Naye Meneja wa Biashara wa Kampuni ya Kimataifa ya AIKAN ya Nchini Misri
Bwana Mohammed Alef Sherief alimueleza
Balozi Seif kwamba Taasisi yake imekuwa ikitoa mafunzo ya biashara ili kuwajengea
uwezo vijana kujimudu kimaisha baaada kumaliza masomo yao.
Bwana Sherief
alisema mpango huo unaohusisha wataalamu waliobobea katika fani ya Biashara huandaliwa katika mazingira bora yanayotoa
ushawishi kwa vijana kupenda kujiunga badala ya kubakia kuzurura mitaani na hatimae kujiingiza katika
vikundi viovu.
Akitoa
Shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliupongeza Ujumbe huo wa Wafanyabiashara na
wahandisi kutoka Nchini Misri kwa uwamuzi wake wa kutaka kusaidia taaluma
katika sekta ya uwekezaji vitega uchumi hapa Zanzibar.
Balozi Seif
alisema Zanzibar hivi sasa imo katika mipango ya kuimarisha uchumi wake kupitia
sekta ya viwanda, uvuvi, vituo vya biashara pamoja na maeneo mengine jambo
ambalo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itazingatia Michoro iliyotayarishwa na
Wataalamu hao katika azma ya kufanikisha mipango yake.
Taasisi ya
Ushauri wa Uhandisi katika miundombinu ya ujenzi, usarifu wa Miji, Majengo ya
Kisasa pamoja na Vituo vya Kimataifa vya Biashara { ECG } ya Nchini Misri
tayari imeshajenga Vituo Sita vya Kimataifa vya Kiabiashara katika Nchi za
Qatar, Kuweit, Sudan, Kenya, Tanzania Bara na wenyeji Misri.
Mhandisi Amr
Allouba amekuwa mshauri muelekezi aliyesimamia kujengwa kwa Kijiji cha Kisasa
cha Kibiashara cha Kimataifa kikiopo katika vitongoji vya Mtaa wa Kadizani ndani
ya Mji wa Cairo Nchini Misri.
Wakati huo
huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikutana na Balozi
Mdogo wa Oman aliyepo Zanzibar Bwana Ali Abdulla Ofisini kwake Vuga Mjini
Zanzibar.
Katika
mazungumzo yao Balozi Seif kupitia Balozi Mdogo huyo wa Oman aliishukuru
Serikali ya Nchi hiyo kwa jitihada inazochukuwa katika kusaidia harakati za
Maendeleo ya Wananchi wa Zanzibar.
Balozi Seif
alisema kwamba Oman yenye uhusiano wa kidugu na kidamu na Zanzibar imekuwa
mshirika mkubwa kwa Zanzibar hasa katika masuala ya kusaidia fursa za Elimu ya
Juu kwa wanafunzi wa Visiwa vya Zanzibar.
Mapema
Balozi Mdogo wa Oman aliyepo Zanzibar Bwana Ali Abdulla alimuhakikishia Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Nchi yake itaendelea kuiunga mkono Zanzibar
katika harakati zake za kuelekea kwenye maendeleo.
Balozi Ali
Abdulla alisema uhusiano wa Kihistoria wa muda mrefu wa Wananchi wa Oman na
Zanzibar unatokana na maingiliano ya kidamu yaliyopo kwa karne nyingi zilizopita kati ya watu wa pande hizo mbili.