Thursday, 6 August 2015

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akitekeleza Ahadi ya Serikali aliyoitoa Dole na Ndunduke

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akikabidhi Hati  ya umiliki wa eneo la Kilimo kwa Bwana Yuweni Kibwana Nzukwi  Mmoja miongoni mwa wakulima wa Vijiji vya Dole, Ndunduke na Kijichi  baada ya upatikanaji wa ufumbuzi wa mgogoro wa maeneo hayo. Picha na Hassan Issa - OMPR
Mkulima Ana Nyaka Buluju wa Dole    akikabidhiwa hati ya umiliki wa eneo la kilimo kutoka kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  hapo Skuli ya Wazazi Dole Wilaya ya Magharibi  “A “. Picha na Hassan Issa - OMPR





















Baadhi ya wakulima wa  Vijiji vya Dole, Ndunduke na Kijichi wakifuatilia zoezi la kukabidhiwa hati zao za umiliki wa maeneo ya kilimo kwenye Vijiji vyao lililafanywa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi. Picha na Hassan Issa - OMPR 
  
Press Release:-

Hatma ya Mgogoro wa maeneo ya Kilimo unaowahusisha Wakulima wa Vijiji vya Dole, Ndunduke, Kijichi na Nguruweni dhidi ya baadhi ya watu wanaovamia  maeneo hayo hivi sasa umeshafikia ukingoni baada ya kurindima kwa takriban miaka 12.
Mgogoro huo ulizuka kufuatia baadhi ya watu wenye uwezo wa kifedha pamoja na marafiki na familia za maafisa wa taasisi za Kilimo kuvamia maeneo hayo wakati wakielewa kwamba wakulima wa asili wa maeneo hayo walikuwa wakiyatumia kuendeleza shughuli zao za kilimo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akitekeleza Ahadi ya Serikali aliyoitoa Tarehe 14 Disemba mwaka 2012 ya kuwamilikisha Wakulima hao alikabidhi Hati za umiliki huo kwa Wakulima 145 wa Dole, Ndunduke na Kijichi hapo katika maeneo ya skuli ya Wazazi Dole.
Wakulima hao 145 ni miongoni mwa wote Mia 222 wa Vijiji hivyo ambao walipata hati hizo baada ya kuyatumia maeneo hayo ya Serikali  yaliyokuwa chini ya Wizara ya Kilimo wanayolimwa kwa kipindi kirefu cha maisha yao.
Akizungumza na Wakulima na Wananchi wa Vijiji hivyo vya Dole, Ndunduke na Kijichi Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeamuwa kufanya hivyo ili kuwapa fursa ya umiliki wakulima hao waendeleze shughuli zao za Kilimo kwa utulivu zaidi.
Balozi Seif aliwatanabahisha wakulima hao  kuelewa kwamba maeneo waliyopewa ni kwa ajili ya kilimo kama walivyofanyiwa wenzao wa Kijiji cha Nguruweni .
 Alisema maeneo hayo tokea asili kutokana na mazingira yake yamekuwa ni vianzio vya maji, hivyo Serikali Kuu haitoruhusu kamwe watu wakaamua kubadilisha utaratibu na kuanza kujenga nyumba za kudumu za kuishi.
“ Wananchi wa Nguruweni bado bado wanafuata utaratibu waliopewa kama Hati zao zinavyoelekeza. Na Nyinyi wakulima wa Dole, Ndunduke pamoja na Kijichiinafaa muige mfano wa wenzenu wa Nguruweni “. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwashukuru na kuwapongeza Wananchi na Wakulima wa Dole, Ndunduke, Nguruweni na Kijichi kwa ustahamilivu wao mkubwa waliouonyesha ambao umeipa faraja Serikali na kufikia hatua njema na ya mafanikio.
Balozi Seif aliwashauri Wakulima hao mbali ya kuendeleza shughuli za kilimo mchanganyiko lakini pia wana fursa ya kuimarisha miti ya mishoki shoki  kwa nia ya kuongeza  mapato yao na kujikimu kimaisha katika azma ya kupunguza umaskini.
Akitoa Taarifa fupi katika mkutano  huo wa makabidhiano ya hati ya umiliki wa maeneo ya kilimo, Mwenyekkiti wa Wakulima wa Dole, na Ndunduke Dr. Daudi Silas Mukaka alisema Serikali Kuu imeonyesha nia thabiti ya kuwajali Wananchi wake.
Dr. Mukaka alisema Wananchi pamoja na Wakulima wa Dole na Ndunduke wamefarajika sana kutokana na kazi kubwa iliyochukuliwa na Serikali  Kuu chini ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwa kushirikiana na baadhi ya Viongozi wa Taasisi za Kilimo na Ardhi katika kulipatia ufumbuzi wa kudumu suala hilo la mgogoro wa maeneo ya kilimo.
Alifahamisha kwamba mgogoro huo wa miaka 12 ulianza hatua za kuchukuliwa  ufumbuzi katika kikao cha Tarehe 14 Disemba Mwaka 2012 chini ya Mwenyekiti wa Kamati iliyoundwa Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mh. Abdullah Mwinyi ambapo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitoa ahadi ya kupatiwa ufumbuzi tatizo hilo.
Mapema Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mh. Abdullah Mwinyi  alisema licha ya Wananchi wa Vijiji hivyo kuonyesha ishara ya hasira lakini alifarajika kuona kwamba busara ilitawala katika kulishughulikia tatizo hilo.
Mheshimiwa Abdullah alisema Wananchi hao wanapaswa kuendelea kumpongeza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kutokana na Uongozi wake wa busara wa kuweka ahadi na akawa makini kuitekeleza.
“ Kiongozi mzuri ni yule anayeweka ahadi akaitekeleza. Balozi Seif anastahiki kupongezwa na kushukuriwa kwa suala hili ambalo sote tunaelewa lilivyokuwa na ugumu wake “. Alisema Mkuu huyo wa Mkoa wa Mjini Magharibi.
Migogoro ya ardhi katika maeneo mbali mbali ya Visiwa vya Zanzibar hivi sasa inaonekana kuchukuwa sura mpya ya kuanza kuchukuliwa hatua za ufumbuzi kutokana na uamuzi wake wa kusajili ardhi yote ya Zanzibar.