Moja kati ya majengo ya Skuli mpya ya Wilaya ya Kusini
inayojengwa katika eneo la Kibuteni ambao ujenzi wake una suasua kutokana na
Mkandarasi kuchelewa kupata fedha za kuendesha mradi huo. Picha na
Hassan Issa – OMPR
Mkuu wa ujenzi wa Kampuni ya United Builders Mhandisi Hamza Najum
akimpatia maelezo Balozi Seif Ali Iddi aliyefika kukagua ujenzi wa Skuli ya
Sekondari ya Wilaya ya Kusini hapo Kibuteni. Picha na
Hassan Issa – OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif akiuagiza Uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya amali
kufuatilia ahadi aliyotoa mkandarasi wa ujenzi wa Skuli hiyo ambao umeonekana
kuchelewa kidogo kulingana na mikataba iliyofungwa kati ya pande hizo mbili. Wa mwanzo
kutoka kulia ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mh. Ali Juma Shamuhuna,
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Nd. Abdullah Mzee Abdullah na Mkuu wa Mkoa wa
Kusini Unguja Dr.Idriss Hijja. Picha na
Hassan Issa – OMPR
Press Release:-
Wizara ya
Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar
imekumbushwa kuzingatia zaidi Wahandisi wa ujenzi waliomakini katika kuzingatia
mikataba yao jambo ambalo litasaidia na kurahisisha kwa wakati miradi wanayopewa
kuitekeleza hasai ya majengo ya Taaluma.
Kumbusho
hilo limetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
alipofanya ziara fupi ya kukaguwa maendeleo ya ujenzi wa Skuli ya Sekondari ya
Wilaya ya Kusini iliyopo Kibuteni ambayo ujenzi wake unaonekana kusua sua na
kupita muda halisi uliopangiwa kukamilika kwake.
Skuli hiyo
ya Sekondari ya Wilaya inayojengwa chini ya Wahandisi wa Kampuni ya Ujenzi ya
United Builders yenye Makao Makuu yake Mjini Dar es salaam inatarajiwa
kugharimu jumla ya shilingi Milioni 223,000,000/- hadi kukamilika kwake.
Balozi Seif Ali
Iddi alisema zipo Kampuni za ujenzi zenye wahandisi na wajenzi Makini waliobobea
ambao hupenda kufanya kazi zake kwa kuzingatia mikataba na kuthamani wakati wa kazi wanzopewa na wale wanaofunga
mikataba nao kuzitekeleza.
Alisema
Serikali Kuu ina uzoefu mkubwa na Wakandarasi wazuri waliobobea katika kufanya kazi mbali mbali za
ujenzi ambao wameshawahi kupewa baadhi ya
Tenda za miradi hasa ile ya Taasisi za Umma na kuitekeleza kwa ufanisi
mkubwa.
Makamu wa Pili
wa Rais wa Zanzibar aliuagiza Uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali
kuhakikisha kwamba wanafuatilia ahadi aliyotoa mjenzi wa Skuli hiyo kwamba
inatekelezwa kwa wakati aliotoa baada ya kupita muda halisi wa Mkataba.
Akitoa
ufafanusi wa maendeleo ya ujenzi wa Skuli hiyo Mkandarasi wa ujenzi huo
Mhandisi Hamza Najim alisema kuzorota kwa muda wa ujenzi wa Skuli hiyo
kumesababishwa na ucheleweshwaji wa kupatrikana kwa fedha za kuendesha mradi
huo.
Mhandisi
Hamza alisema mfumo wa utoaji wa fedha kutoka kwenye akaunti ya Benki
waliyosajili umekuwa wa kuzorota licha ya kupata taarifa kwamba fedha hizo
zimeshaingizwa kwa ajili ya matumizi jambo ambalo huleta usumbufu kwao na hata kwa taasisi wanazotiliana
mikataba ya kuwatekelezea miradi yao.
Mhandisi
huyo wa Kampuni ya Ujenzi ya United Builders alifahamisha kwamba katika
kukabiliana na changamoto hizo Uongozi wa Kampuni hiyo umeamua kufanya uhamisho
wa Benki wanayoitumia iliyoko Tanzania Bara na kuileta Zanzibar kwa lengo la kurahisisha kazi zao.
Alieleza
kwamba kazi halisi ya ujenzi huo inatarajiwa kukamilika ndani ya miezi Minne
kuanzia sasa endapo upatikanaji wa fedha hizo utakwenda kwa wakati na hivi sasa
wajenzi wake wako katika hatua ya kukamilisha kazi za plasta pamoja na ujenzi
wa mapaa ya majengo hayo.
Mapema
Meneja wa Mradi huo kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Ndugu
Ali Juma Ali alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba mradi huo
unatazamiwa kuwa na majengo Manne makubwa yatakayokidhi mahitaji ya
wanafunzi,Walimu pamoja na utawala.
Ndugu Ali
Juma alisema Skuli hiyo itakuwa na Ofisi za wafanyakazi, madarasa ya wanafunzi,
Mabweni, nyumba za Walimu sehemu za michezo sambamba na huduma za vyakula.
Balozi Seif
alitembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa skuli hiyo ya Sekondari Wilaya ya
Kusini iliyopo Kibuteni ikiwa ni Miongoni mwa Skuli mbili za Sekondari Zanzibar pamoja na ile iliyopo Mkanyageni
Kisiwani Pemba zinazojengwa kwa ufadhili
wa Benki ya Maendeleo ya Kiarabu { Badea
}.