Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
akilifungua rasmi Jengo Jipya la Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia
Tanzania{ COSTECH } Ofisi ya Zanzibar
liliopo ndani ya majengo ya zamani ya ilichokuwa kiwanda cha Sigara Maruhubi
Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar. Picha na Hassan Issa –
OMPR
Balozi Seif wa pili
kutoka Kushoto akipata maelezo kutoka kwa Wataalamu wa Chuo cha Utafiti
Kizimbani wakiongozwa na Said Suleiman Bakari jinsi zao
la viazi vitamu linavyoweza kutumiwa vyema katika utengenezaji wa Juisi. Wa kwanza
kutoka kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Majini Magharibi Mh. Abullah Mwinyi. Picha na Hassan Issa –
OMPR
Watafiti na wawakilishi wa Vikundi vya wajasiri amali waliopata ufadhili
kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia wakimpatia maelezo Balozi Seif
wakati akiangalia maonyesha mara baada ya kulifungua Jengo la Tume hiyo. Picha na Hassan Issa –
OMPR
Baadhi ya Wataalamu na wajasiri amali kutoka vikundi tofauti Nchini
wakifuatilia matukio mbali mbali yaliyojiri kwenye hafla ya uzinduzi wa jengo
Jipya la Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia { COSTECH }. Picha na Hassan Issa –
OMPR
Balozi Seif akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa Jengo la Tume ya Taifa
ya Sayansi na Teknolojia hapo Maruhubi akimuwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa Baraza la MapinduziI Dr. Ali Mohammed Shein. Picha na Hassan Issa –
OMPR
Balozi Seif akiwa katika Picha ya pamoja na wajumbe wa Bodi ya Tume ya
Taifa ya Sayansi na Teknolojia Tanzania { COSTECH } mara baada ya uzinduzi wa
jengo la Tume hiyo hapo Maruhubi. Kulia ya
Balozi Seif ni Kaimu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Mh. Ali Juma Shamuhuna, Mkurugenzi Mkuu wa Costech Dr. Hassan Mshimba, Makamu
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar {SUZA} Dr. Idriss Rai. Kushoto ya
Balozi Seif ni Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia
Kanal Mstaafu Joseph Simba Kalia, Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mh. Abdullah
Mwinyi pamoja na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Nd. Ahmad Kassim.
Picha na Hassan Issa –
OMPR
Press Release:-
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein alisema wakati umefika kwa sekta binafsi
kujenga Utamaduni wa kutoa ruzuku za tafiti kwa Tume ya Taifa ya Sayansi na
Teknolojia ili ijipatie nguvu za ziada za uwezeshaji wa kuendesha shughuli zake
za utafiti kama nchi nyengine Duniani zilizofanikiwa kwa kufuata mfumo huo.
Alisema kufanya utafiti kunahitaji nguvu kubwa ya
fedha kiasi kwamba Serikali pekee haiwezi kumudu kugharamia bila ya
kushirikisha taasisi mbali mbali za sekta binafsi za ndani na nje ya nchi.
Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohammed Shein alisema hayo
katika Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Iddi wakati wa ufunguzi wa Jengo la Ofisi ya Tume ya Taifa ya
Sayansi na Teknolojia { COSTECH } liliopo Maruhubi nje kidogo ya Mji wa
Zanzibar.
Alisema Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia
Tanzania imeonyesha mwanga wa kusaidia jamii kwenye tafiti za kina za
Kimaendeleo zitakazomkomboa Mtanzania kutoka katika dimbwi la umaskini na
kuelekea kwenye maendeleo ya kweli.
Alieleza kwamba Costech imekuwa na jitihada katika
uendelezaji wa rasilmali watu ya wataalamu waliopo Zanzibar inayowagharamiwa kimasomo kwa shahada yao ya uzamivu na
uzamili katika kiwango cha Master na Udokta kwenye vyuo mbali mbali ndani na
Nje ya Nchi ambao kwa sasa wapo 22 kutoka Zanzibar.
“ Tume ya Taifa ya Sayansi na Tekonolojia pia
tunaishukuru kwa kuratibu na kugharamia tafiti tofauti zinazosimamiwa na vyuo
mbali mbali vya Zanzibar kama SUZA, IMS, ZIFFA na Taasisi ya Utafiti Kizimbani
“. Alisema Dr. Shein.
Alifahamisha kwamba Costech kwa kushirikiana na Tume
ya Mipango Zanzibar pamoja na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
tayari imeshaanda agenda ya utafiti ya Zanzibar ili Serikali iweze kuitumia
katika maamuzi ya vipaumbele vya Tafiti kwa maendeleo ya jumla ya Taifa.
Dr. Shein alisema hilo ni jambo zuri katika muelekeo
wa kunyanua ustawi wa Umma na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa upande wake
itakuwa tayari kutumia matokeo ya tafiti
zinazofanywa na Wasomi wa hapa Nchini kupitia Tume hiyo.
Hata hivyo Dr. Shein aliitanabahisha Tume ya Taifa
ya Sayansi na Teknolojia kwamba yale matokeo ya utafiti yanayostahili kuwafika moja
kwa moja Wananchi yatolewe ili kuwapa fursa wananchi hao kuelewa kinachoendelea
kwenye maisha yao ya kila siku.
Rais wa Zanzibar ameipongeza Serikali ya Jamuhuri ya
Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia kwa
uamuzi wake wa busara wa kuanzisha Ofisi ya Tume ya Taifa ya Sayansi na
Teknolojia.
Alisema uamuzi huu unadhihirisha wazi jinsi Tume
hiyo Chini ya Wizara yake ilivyopania kukuza maendeleo ya Sayansi na Teknolojia
kwa pande zote mbili za Muungano ambapo Taasisi hii ndio msimamizi na mshauri
Mkuu wa Serikali kwa masuala yote yanayohusu sayansi, ugunduzi na Teknolojia
kwa maendeleo ya Taifa.
Dr. Shein alielezea matumaini yake binafsi na yale ya Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar kwamba uwepo wa Ofisi ya Tume
hiyo kutaongeza kasi kwa Wasomi wa hapa Nchini kuendelea kufanya tafiti mbali
mbali na kuongeza kasi ya shughuli za ubunifu katika nyanja tofauti.
Rais wa Zanzibar alitoa wito kwa Taasisi nyengine za
Serikali ya Muungano wa Tanzania na zile Binafsi za Tanzania Bara mbazo
hazijafungua Ofisi zao hapa Zanzibar kufanya hivyo na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar itakuwa tayari kuwapatia maeneo ya kujenga Ofisi hizo kwa lengo la
kuwarahisishia Wananchi kupata huduma za karibu.
Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi
na Teknolojia COSTECH Dr. Hassan Mshimba
alisema ujenzi wa Ofisi ya Tume hiyo hapa Zanzibar ni kutekekeza ahadi iliyotoa Uongozi wa
Taasisi hiyo kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mwaka 2012.
Dr. Hassan Mshimba alisema kwamba Tume ya Taifa ya
Sayansi na Teknolojia kwa kuona umuhimu wa zao la Mwani kwa Serikali ya Mapinduzi
ilitoa Vihori 100 vya kubebea mwani kwa lengo la kuwawezesha wakulima wa zao
hilo Unguja na Pemba kukuza Kilimo hich ikiwa ni miongozi mwa miradi sita
inayotekelezwa na Tume hiyo kwa Upande wa Zanzibar.
Mkurugenzi Mkuu huyo wa Costech alisisitiza kwamba katika
azma ya kukuza ajira Nchini Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia imekusudia
kuungana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha vitengo vya
Utafiti Zanzibar kama alivyosisitiza Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohammed Shein
siku ya Utafiti Tarehe 12 Disemba mwaka 2014.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Taifa ya Sayansi
na Teknolojia Kanal Mstaafu Joseph Simba Kalia ameipongeza Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar kwa ukarimu wake wa kutoa
Jengo kwa ajili ya Ofisi za Tume hiyo.
Kanal Mstaafu Simba Kalia alisema kitendo hicho
kilichofanywa na SMZ ni uthibitisho wa
kuthamini umuhimu wa fani ya Utafiti ambayo ndio chachu ya maendeleo ya jambo
lolote lile hapa Ulimwenguni.
Ofisi ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia ilizinduliwa rasmi mnamo Tarehe 11 Juni Mwaka 2012 katika
Majengo ya Ofisi ya Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa
Tanzania yaliyopo Tunguu Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar na kuanza kutoa huduma
zake hapa Zanzibar.
Ofisi hiyo ya
Costech iliyofanyiwa matengenezo kwa kipindi cha miezi 12 imegharimu zaidi
ya shilingi za Kitanzania Milioni 185,000,000/- ikiwa na vyumba sita vya Ofisi pamoja na
ukumbi wa Mikutano ipo kwenye majengo ya
zamani ya ilichokuwa Kiwanda cha utengezezaji Sigara baridi katika eneo la
Maruhubi nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.