GARI ya Kampuni ya Mecco ikimwaga lami katika mashine maalumu ya kuchawanyia lami hiyo, katika barabara ya Konde-Wete kama wanavyoonekana wafanyakazi wa kampuni hiyo wakiwa kazini.
GARI maalumu ya kutandazia lami ya kampuni ya Mecco, ikiwa kkazini katika barabara ya Konde-Wete, kama inavyoonekana kazi hiyo ikiwa inaendelea kwa kasili, ili kukamilika kwa barabara hiyo.
GARI maalumu ya kuweka sawa lami kutoka katika kampuni ya Mecco ikiweka lami hiyo, katika barabara ya Konde-Wete kama ilivyokutwa na mpiga picha.
MAKAMO wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe:Balozi Seif Ali Iddi akipata maelekezo ya hali ya uwekaji wa lami katika barabara ya Konde- Wete, kutokana kwa msimamizi wa Ujenzi wa Kampuni hiyo Abdulkadir Mohammed Bujet, wakati alipotembelea na kuangalia hali ya barabara hiyo inavyokwenda.
Na Othman Khamis Ame, OMPR
Harakati za ujenzi wa Bara bara ya Wete hadi konde ikiwa miongoni mwa mradi wa Bara bara tatu Kisiwani Pemba zinaendelea baada ya maridhiano baina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na mjenzi wa mradi huo Kampuni ya Mwananchi Contracting Company Engineering { MECCO }.
Ujenzi wa Bara bara hizo wa awamu ya kwanza wenye urefu wa Kilomita zaidi ya 30 ulioanza rasmi Tarehe 15 Mei mwaka 2009 umekuwa ukisua sua kutokana na sababu mbali mbali ikiwemo uchelewaji wa feha kutoka kwa mfadhili wa mradi huo Benki ya Maendeleo ya Kiislamu { BADEA.
Maridhiano hayo yalifiikiwa kutokana na Kamati ya Mawasiliano na Ujenzi ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar kutembelea mradi huo mapema mwezi huu na kufikiwa maazimio ya yaliyoagiza juhudi zifanywe ili madai ya mjenzi wa bara bara hizo yashughulikiwe kwa upande mwengine wa Serikali.
Maazimio hayo
pia
yalielekezwa na kumuomba mjenzi aendelee na kazi kulingana na uwezo wake alionao wakati Serikali Kuu inaendelea kushughulikia malipo ya madai yake mbali mbali.
Akitoa maelezo kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyefanya ziara ya kukagua maendeleo hya ujenzi wa bara bara kutoka Wete hadi Konde Afisa Mdhamini wa Miundo mbinu na Mawasiliano Pemba Nd.Hamad Ahmed Baucha alisema Uongozi wa usimamizi wa kazi hiyo umeishukuru Kamati hiyo ya Baraza la Wawakilishi kwa uamuzi wake wa kuingilia kati suala hilo.
Nd. Baucha alisema hatua hiyo mbali ya kunusuru hasara nyengine lakini pia imetia moyo na chachu kwa wananchi pamoja na wawekezaji kufanya shughuli zao kwa uhakika baada ya kukamilika kwa miundo mbinu ya mawasiliano ya bara bara.
Alisema kazi ya uwekaji lami kwenye bara bara hiyo ya Wete hado Konde ilianza mnamo Tarehe 19 mwezi huu na kuendelea kwa kasi ikileta matumaini ya kuwa kazi hiyo inaweza kukamilika kwa wakati uliopangwa.
Mwakilishi wa Kampuni ya Mwananchi Contracting Company Engineering { MECCO } Bwana Abdullkadir Mohammed Bujet alimuhakikisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wahandisi wa kazi hiyo watajitahidi kutekeleza mradi huo katika kiwango bora kinachokubalika.
Bwana Bujet alisema ujenzi huo wa lami hivi sasa unafanyika kwa masafa ya mita mia tato kwa siku kiwango kinacholeta faraja kwa kukamilika kazi hiyo katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia Januari mwakani.
Alifahamisha kwamba hivi sasa tayari kilo mita 14.2 za bara bara hiyo itokayo Wete hadi Konde imeshawekewa lami zikibakia kilo mita 12 tu kukamilisha awamu hiyo.
Mradi huo wa awamu ya kwanza wa ujenzi wa kilo mita 30 unahusisha kufumua bara bara, kujenga tuta la bara bara,ujenzi wa madaraja mdogo madogo { pipe culvert } pamoja na madaraja saba sehemu mbali mbali ya bara bara zote mbili za Wete Gando na Wete Konde.
Kuchelewa kukamilika kwa wakati mradi huo wa bara bara tatu za Pemba uliokuwa wa gharama ya shilingi Bilioni 23,389,551,848.75 umesabisha kuongezeka na kufikia gharama ya shilingi Bilioni 30,176,874,854/- hadi utakapokamilika.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akikamilisha ziara yake ya siku tatu Kisiwani Pemba kutembelea miradi mbali mbali ya maendeleo aliutembelea msikiti mkongwe kabisa ndani ya Ukanda wa Afrika Mashriki uliopo Micheweni Mjini Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Akisalimiana na uongozi wa Kamati ya msikiti huo pamoja na baadhi ya waazi wake Balozi Seif aliwakumbusha waumini wa Dini ya Kiislamu kuendelea kushikamana kama maamrisho ya dini yao yanavyoelekeza.
Alisema Dini ya kiislamu imekuwa ikisisitiza suala la amani jambo ambalo likifuatwa na kutekelezwa ipasavyo husaidia kuwapa utulivu pamoja na wananchi kufanya ibada za shughuli zao kama kawaida.
Aliwaasa kuwa na hadhari ya kuchanganya dini na siasa kama baadhi ya watu nhasa wanasiasa kujaribu kushawishi watu kufanya hivyo matokeo yake ni kuanzisha cheche za uhasama na wasi wasi katika jamii.
Msikiti wa Ijumaa wa Micheweni Mjini unakisiwa kujengwa tokea karne ya 14 kipindi ambacho kilikuwa na harakati za kueneza kwa Dini ya Kiislamu katika mwambao wa Afrika Mashariki.