Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa na
mwenyeji wake Mrajisi wa Bodi ya Chakula, Dawa na Vipodozi Dr. Burhan Othman
Simai akikagua Maabara ya Bodi hiyo iliyopo kwenye jengo lao jipya liliopo Mtaa wa Mombasa nje kidogo ya Mji wa
Zanzibar. Picha na
Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
Meneja wa Kitengo chaMtandao wa mawasiliano ya Kompyuta cha Bodi ya Chakula na Dawa { ZFDB } Ndugu Mohamed Yahya Said aliyevaa shati rangi ya buluu akielezea mfumo wa Mradi wa MRH unaotoa fursa kwa Bodi ya Chakula na Dawa kuwa na mawasiliano ya moja kwa moja ya mamlaka za Bodi nyengine Duniani.
Press Release:-
Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameuomba Uongozi wa Bodi ya
Chakula,Dawa na Vipodozi Zanzibar { ZFDB } kuwaelimisha wananchi juu ya mfumo bora wa matumizi ya vyakula na
vinywaji ili kulinda afya zao.
Alisema afya
za jamii zitaendelea kuimarika na kuwa salama endapo vyakula na vinywaji
wanavyotumia vinakuwa salama katika kiwango kinachokubalika kwa matumizi ya mwanaadamu popote pale
Duniani.
Balozi Seif
alitoa ombi hilo wakati alipofanya ziara fupi ya kulikagua jengo jipya la Bodi ya Chakula,
Dawa na Vipodozi Zanzibar liliopo katika
Mtaa wa Mombasa Wilaya ya Magharibi nje
kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Alisema
hatua ya kuuelimisha umma kupitia vyombo mbali mbali vya Habari na mawasiliano
inafaa iongezwe kwa lengo la kuitanabaisha jamii kujiepuka na hila za baadhi ya wafanyabiashara
wanaotumia mwanya wa kusambaza bidhaa zisizostahiki kutumiwa na mlaji.
Alieleza
kwamba zipo bidhaa zinazoingizwa nchini na baadhi ya wafanyabiashara ambazo
tayari zimeshapitwa na wakati wa matumizi wakijua fika kwamba zinaweza kuleta
athari kwa umma lakini kinachowapa msukumo wa kufanya hivyo ni tamaa na utajiri
wa haraka haraka.
Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar aliushukuru Uongozi na wafanyakazi wa Bodi hiyo ya
Chakula, Dawa na Vipodozi kwa kujudi wanazochukuwa za kukabiliana na wajanja
wanaojaribu kuingiza bidhaa zisizostahiki kutumika hapa nchini bila ya kujali
afya za wananchi wenzao.
Balozi Seif
pia akaupongeza uongozi wa Bodi hiyo kwa hatua iliyofikia ya kujenga jengo
kubwa na la kisasa linalokwenda na wakati na kuuhakikishia Uongozi wa Bodi hiyo
kwamba atachukuwa juhudi katika kuona yale mafungu yao wanayopangiwa katika
Bajeti ya Wizara yao wanayapata ili kukamilisha ujenzi wao.
Mapema Mrajisi
wa Bodi ya Chakula, Dawa na Vipodozi Zanzibar Dr. Burhan Othman Simai alisema
Bodi hiyo hivi sasa imejikita zaidi katika kuongeza uwezo wa kulinda afya za
Wananachi kwa kutumia mfumo wa Taaluma.
Dr. Burhan
alisema watendaji wa bodi hiyo watajengewa mazingira mazuri ya kupatiwa mafunzo
ya kitaalamu zaidi ambayo yatakidhi
mahitaji halisi ya mfumo huo.
Mrajisi huyo
wa Bodi ya Chakula, Dawa na Vipodozi alifahamisha kwamba Taasisi hiyo kwa mujibu wa vigezo na taratibu
za Kimataifa kwa sasa inalazimika kuwa
Mamlaka inayojitegemea.
Alisema
licha ya juhudi za kwenda na vigezo hivyo iliyochukuliwa na Bodi hiyo kwa hatua
ya kuandaa rasimu ya mabadiliko ya sheria iliyoandaliwa na Taasisi hiyo lakini ufinyu wa bajeti nao
unachangia kuzorota kwa suala hilo.