Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwa niaba ya Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohamed Shein akilifungua Tamasha la Sita la Kiislamu Zanzibar hapo jumba la Wananchi Forodhani Mjini Zanzibar.
Balozi Seif akimkabidhi cheti maalum Balozi wa Palestina Nchini Tanzania Bwana Nassib Abu Jesh kwa ushiriki wa Ubalozi huo kwenye kuunga mkono TYamasha la Kiislamu Zanzibar.
Balozi Seif akiwa katika picha ya pamoja na msanii maaruru aliyepata sifa kipindi kifupi kutokana na Qasida yake ya Nadu Ustadh Juma Zubeir baada ya kumkabidhi cheti maalum kutokana na ubunifu wake uliosaidia Tamaduni ya kiislamu.
Kulia yao ni Mwenyekiti wa Tamasha la Kiislamu Zanzibnar Ustadh Jabir Haidar Jabir.
Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
Na Othman Khamis Ame, OMPR
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Al-Hajj Dr. Ali Mohamed Shein ametoa wito kwa jamii kupitia Tamasha la Kiislamu kuendelea kuelimishana na kukumbushana umuhimu wa kuendeleza amani na kuepuka mifarakano baina ya waislamu wenyewe na hata wale wanaoamini Dini nyengine hapa nchini.
Alisema Walimu na Masheikh nao wasichoke kuukumbusha umma faida ya kuwepo kwa amani ya nchi kwa vile bado yapo matukio yanayothibitisha na kuashiria uwepo wa baadhi ya watu walioghafilika.
Al Hajj Dr. Ali Mohamed Shein alieleza hayo wakati wa hafla ya ufunguzi wa Tamasha la sita la Kiislamu katika Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo katika Kasri ya Kifalme Jumba la Wananchi Forodhani Mjini Zanzibar.
Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba matukio hayo maovu ni kinyume na mafundisho ya dini yenyewe sambamba na kukiukwa kwa haki za Binadaamu ambapo kwa ujumla wake Mwenyezi Muungu amekuwa akiwaasa waja wake kuacha kumwaga damu kusiko na hatia.
Alieleza kwamba wakati umefika kwa Waumini wa Dini ya Kiislamu na wananchi wote nchini kujifunza athari za kutoweka kwa hali ya amani wakishuhudia kutokea katika nchi mbali mbali Duniani.
“ Matokeo ya hali kama hii ya kusikitisha kama tunavyoshuhudia katika baadhi ya Mataifa ya Kiislamu kama vile Syria, Afghanistan na Iraq na hali wanayokabiliana nayo wananchi wa Palestina “. Alisema Dr. Sheni.
Rais wa Zanzibar alisisitiza kwamba ni wazi kuwa athari za matokeo ya kutoweka kwa hali ya amani huwafika watu wote lakini waathirika wakuu zaidi katika janga hilo ni watoto, wanawake,watu wenye ulemavu, wagonjwa pamoja na wazee wasioweza kujihami.
Al – Hajj Dr. Ali Mohamed Shein alitoa wito kwa Tamasha hilo la Kiislamu kuwa chachu ya kuelimishana na kukumbushana katika kukabiliana na vitendo vya udhalilishwaji wa wanawake na watoto ambavyo vinaonekana kuendelea kulitia doa Taifa.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi lielezea faraja yake kutokana na wazo lililoibua kuanzishwa kwa Tamasha la Kiislamu hapa Zanzibar ambalo limekuwa chem chem ya elimu na maarifa ya Kiislamu.
Alisema Tamasha hilo lina fursa pana ya kuibua vipaji katika umahiri wa kusoma na kuhifadhi Quran Tukufu, usomaji wa Maulidi, Qasida, mashairi na Kiarabu na Kiswahili pamoja na uigizaji.
Dr. Shein alisema kwamba michezo mbali mbali iliyosuniwa na Kiongozi wa Dini ya Kiislamu Mtume Muhammad { SAW } ni miongoni mwa mambo na masuala ya msingi yanayosaidia kurithisha watoto Utamaduni ya Kiislamu.
Aliwaomba wasimamizi wa Tamasha hilo la Kiislamu kuzidi kuliimarisha kwa kubuni shughuli mbali mbali zinazohusiana na utamaduni wa Kiislamu ili kuongeza maarifa na taaluma inayopatikana kupitia Tamasha hilo.
Alieleza kwamba ipo haja ya kulitanga zaidi Tamasha hilo kwa kutumia fursa mbali mbali zilizopo kwa lengo la kuliongezea umaarufu pamoja na kuongeza idadi ya wageni wanaofika Nchini wakiwemo Wazanzibari wanaoishi mataifa mbali mbali Duniani.
Mapema Mwenyekiti wa Tamasha la Kiislamu Zanzibar { Zenj Empire Islamic Festival} Ustaadh Jabir Haidar Jabir alisema tamasha hilo lililoanzishwa Tarehe 13/12/2009 limelenga kuimarisha utamaduni wa Kiislamu nchini.
Ustadh Jabir alisema wiki ya Tamasha hilo hutoa fursa kwa waumini wa Dini ya Kiislamu hasa wanafunzi wa vyuo na madrasa kujumuika pamoja kwenye usomaji Qasida, harakati za Kiislamu kama michezo na mafunzlo ya dini jambo ambalo hutoa mwanga na mafundisho kwa washiriki hao kuelewa mila na tamaduni zao.
Alisema Juhudi zinazochukuiliwa na Uongozi wa Tamasha hilo ni kusaidia kuratibu mafungamano yanayojumuisha watu wa dini na madhehebu tofauti kuishi pamoja na upendo na kushirikiana.
Tamasha la Kiislamu Zanzibar lililoasisiwa na kuanzishwa karibu miaka sita iliyopita limekuwa na utaratibu wa kushirikisha
pia
michezo mbali mbali iliyosuniwa na Mtume Muhammad { SAW } kama vile michezo ya riadha, kuogelea, Qasida, Maulidi ya Homu na usomaji wa Quran.
Wiki ya Tamasha la Kiislamu Zanzibar { Zenj Empire Islamic Festival } iliyoanza Tarehe 17 Disemba inamalizia Tarehe 21 Disemba ambapo watu wa rika mbali mbali wakiwemo Mabalozi na Maafisa wao wa Nchi za Nje waliopo Nchini Tanzania na watalii wamepata fursa ya kushiriki tamasha hilo.