Kikao cha 14 cha Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 kilikutana chini ya Mwenyekiti wake Waziri Mkuu wa SMT Mh. Mizengo Pinda akiwa sambamba na Mwenyekiti Mwenza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
Kikao hicho kilichoshirikisha wajumbe wa pande zote mbili za Muungano wakiwemo mawaziri na watendaji waandamizi wa taasisi za serikali kimefanyika katika Ukumbi wa Waziri Mkuu uliopo Ikulu Jijini Dar es salaam.
Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
Na Othman Khamis, OMPR
Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 imekutana katika Kikao chake cha Kawaida cha 14 chini ya mwenyekiti wake Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Mizengo Pinda.
Kikao hicho kilichoshirikisha
pia
Mwenyekiti Mwenza wa Kamati hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, Wajumbe wa Pande zote mbili za Muungano ambao ni baadhi ya Mawaziri na watendaji wa Taasisi za Umma kilifanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu Jijini Dar es salaam.
Akiwasilisha utekelezaji wa agizo la Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa ya watu na Makazi ya mwaka 2012 la kikao cha 13 Kamishna wa Sensa Tanzania Hajat Amina Mrisho alisema kazi za usambazaji wa chapisho la tatu la Taarifa za msingi la Kidemografia, Kijamii na Kiuchumi unaendelea kusambazwa kwa watumiaji.
Kamishna wa Sensa huyo Tanzania alifahamisha kwamba warsha kama hizo zinatarajiwa kuendelea katika Mikoa mengine hapa Nchini mara uwezeshaji utakapokamilika.
Kigusia suala la uhakiki wa mipaka ambayo inastahiki kufanyika kwa uangalifu mkubwa utakaoshirikisha wadau wote wa mikapa Hajat Amina alisema kazi hiyo imepangwa kufanyika nchi nzima kulingana na uwezo wa Kifedha.
Alisema hadi sasa shughuli hiyo hadi sasa imeweza kufanyika katika Wilaya za Gairo na Chemba,Bagamoyo na hivi sasa inaendelea Wilkaya ya Kiteto kwa Tanzania Bara na Wete Visiwani Zanzibar.
Akiwasilisha Taarifa za uhakiki wa mipaka katika Wilaya ya Kiteto Afisa Takwimu wa Taifa Bwana Enest Bugambi alisema ipo changamoto nyingi zinazowakwaza wananchi hasa lile suala la kuhama hama kwa wafugaji na wakulima na kuingia ktaika maeneo ha hifadhi ya misitu.
Bwana Enest alisema uimarishaji wa usalama wa umiliki wa ardhi kwa maeneo ya kilimo na mifugo ndilo jambo la msingi litakalopunguza au kuondoa kabisa migogoro ya mipaka pamoja na umiliki wa ardhi.
Mtaalamu huyo wa Takwimu alifahamisha kwamba timu ya wataalamu wake tayari imesha hakiki vijiji vipatavyo 36 wakibakisha vijiji kumi ndani ya Wilaya ya Kiteto katika mpango mzima wa matumizi ya chapisha la Sensa ya watu na Makazi ya mwaka 2012.
Wakichangia katika Kikao hicho cha 14 cha Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 baadhi ya Wajumbe wa Kamati hiyo walisema bado suala la migogoro ya wafugaji na wakulima litaendelea kuwepo kwa vile taratibu za umiliki wa ardhi haujawa makini.
Walishauri kutumiwa kwa wataalamu wa taasisi zinazosimamia maendeleo ya jamii ili kutoa taaluma kwa umma katika maeneo mbali mbali hasa zile sehemu za migogoro ili kupunguza matokeo ya ya balaa yakiwemo yale ya mauaji.
Walisema viongozi wa kidini na kisiasa ni vyema wakashirikishwa katika kusaidia migoogoro pale inapotokea katika maeneo wanayoishi.
Akitoa nasaha zake mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012 Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Mizengo Pinda aliipongeza Timu ya wataalamu wanaosimamia uhakiki wa mipaka kwa kazi kuibwa waliyoifanya katika kipindi kifupi.
Mh. Pinda alisema kitendo cha wataalamu hao kushirikisha watendaji wa taasisi husika katika zoezi hilo imeleta uelewa na kupunguza joto la migogoro ya mipaka ambalo lilikuwa likionekana kuelekea kubaya.
“Ni mwanzo mzuri uliofanywa na wataalamu wetu unatoa mwanga mzuri wa muelekeo wa kupunguza migogoro ya mipaka ya ardhi na kustawisha jamii “. Alisema Mh. Pinda.
Mwenyekiti huyo wa Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012 aliiomba kamati hiyo ya uhakiki wa mipaka kuandaa taarifa yao katika mfumo wa kisasa wa teknolojia utakaowawezesha maafisa wa Sensa na ustawi wa jamii kuzitumia vizuri katika kutoa elimu kwa umma.