Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif anayetembea kati kati ya
zulia jekundu akisindikizwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa Mh. Bernard Membe kulia yake na Naibu waziri wa Wizara hiyo
Mh. Mahadhi Juma kushoto yake wakiingia ndani ya Hoteli ya Ramada Dar es
salaam kwenye ufungaji wa Mkutano wa Nne wa Mabalozi wa Tanzania nchi
mbali mbali Duniani. Picha Hassan Issa – OMPR – ZNZ.
Balozi Seif kwa Niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyejkiti wa Baraza la
Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein akiufunga Mkutano wa Nne wa siku Tatu
wa Mabalozi wa Tanzania uliokuwa ukifanyika katika Hoteli ya Ramada
Mjini Dar es salaam. Picha Hassan Issa – OMPR – ZNZ.
Baadhi ya Mabalozi wa Tanzania katika Mataifa mbali mbali Duniani
walioshiriki Mkutano wao wakifuatilia Hotuba ya Ufungaji wa Mkutano huo
iliyosomwa na Balozi Seif kwa niaba ya Rais wa Zanzibar Dr. ASli
Mohammed Shein. Picha Hassan Issa – OMPR – ZNZ.
Balozi Seif akiwa katika picha ya pamoja na Mabalozi wa Tanzania Nchi
mbali mbakli Duniani mara baada ya kuufunga Mkutano wao wa Nne hapo
Ramada Hoteli Jijini Dar es salaam.
Kulia ya Balozi Seif ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania Mh. Benar
Membe, Katibu Mkuu Mpya wa Wizara hiyo Balozi Lebereta Mula mula na
kushoto ya Balozi Seif ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mh. Mhadhi Juma
Maalim. Picha Hassan Issa – OMPR – ZNZ.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akisalimiana na Balozi wa
Tanzania Nchini Jamuhuri ya Watu wa China Balozi Abrahaman Nyimbo mara
baada ya kumalizika kwa Mkutano wa Mabalozi wa Tanzania Mjini Dar es
salaam. Picha Hassan Issa – OMPR – ZNZ.
Press Release:-
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed
Shein alisema Mabalozi wanayoiwakilisha Tanzania katika Mataifa tofauti
Duniani wanapaswa kuitekeleza vilivyo Sera ya Mambo ya Nje inayolenga
katika Diplomasia ya uchumi ambayo ndiyo muongozo wao katika utekelezaji
wa jukumu lao la msingi.
Alisema Sera hiyo ni vyema ikatumika vizuri wakati huu ambao Taifa la
Tanzania linatekeleza Dira ya kuelekea uchumi wa Kati na kati ifikapo
mwaka 2020 kwa upande wa Zanzibar na Mwaka 2025 kwa Tanzania Bara.
Dr. Ali Mohammed Shein alisema hayo wakati akiufunga Mkutano wa Nne wa
siku Tatu wa Mabalozi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika Hotuba
iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi
Seif Ali Iddi hapo katika Ukumbi wa Hoteli ya Ramada Jijini Dar es
salaam.
Alisema katika kipindi cha zaidi ya miaka kumi ya utekelezaji wa Sera ya
Mambo ya Nje yenye kuweka msisitizo katika Diplomasia ya Uchumi
Tanzania imepiga hatua kubwa vikiwemo Visiwa vya Zanzibar.
Dr. Shein alifahamisha kwamba matunda ya Sera hii yanadhihirisha wazi
ukuaji wa sekta ya Utalii, miradi mengine ya kiuchumi ikiwemo pia ile
mikubwa inayotekelezwa na wahisani kwa upande wa Zanzibar.
“ Mikakati mipya ya muda mfupi na mrefu mliowekeana katika Mkutano huu
ni msingi mzuri kabisa kufuatana na mabadiliko ya uchumi yanayotokea
Duniani na kufikia malengo ya Dira ya 2020 na 2025 “. Alisema Dr. Shein.
“ Nina hakika kuwa katika Mkutano huu mmeweza kuziba nyufa zote
zilizojitokeza katika utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001
inayolenga katika Diplomasia ya Uchumi ambayo ndio muongozo wetu katika
utekelezaji wake na ni jukumu letu la msingi “. Alisisitiza Dr. Shein.
Rais wa Zanzibar alieleza kwamba licha ya mafanikio makubwa ya kiuchumi
na maendeleo yanayoendelea kushuhudiwa kwa upande wa Zanzibar lakini
bado iko haja kwa Mabalozi hao wa Tanzania kuongeza juhudi za kuitangaza
Zanzibar katika Mataifa waliyopangiwa kutekeleza majukumu yao ya
Kidiplomasia.
Alisema mafanikio ya Zanzibar katika kukuza sekta ya Utalii , uwekezaji
na utekelezaji wa mipango mengine ya maendeleo hutegemea sana juhudi za
Ofisi za Kibalozi katika kuitangaza Zanzibar nchi za Nje.
Dr. Shein alifahamisha kwamba baadhi ya wakati Serikali imekuwa ikipokea
malalamiko kutoka kwa wawekezaji, watalii na wageni wanaofika Zanzibar
juu ya ukosefu wa taarifa za kutosha kuhusu Zanzibar katika Ofisi za
Kibalozi za Tanzania.
Aliwakumbusha Mabalozi hao kwamba katika kutekeleza majukumu yao ni
vyema kila wakati wakazingatia kuwa Ofisi zao zinaweka taarifa za
kutosha juu ya sekta zote muhimu za kiuchumi na kijamii za pande zote
mbili za Jamuhuri hasa zile fursa za uwekezaji vivutio vya utalii.
“ Suala hili nimekuwa nikilikumbusha kila ninapopata fursa ya kuzungumza
nanyi, hasa wakatia mbao Mabalozi huja kunitembelea na kuniaga kabla ya
kuripoti katika vituo vyao vya kazi “. Alifafanua Dr. Shein.
Alifahamisha kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kupokea
mawazo ya Mabalozi hao ili kupata fursa nzuri ya nini Wanadipomasia hao
wakitangaze kuhusu Zanzibar.
Rais wa Zanzibar alihimiza kwamba katika kipindi hichi ambapo Nchi mbali
mbali Duniani zimekumbwa na misukosuko ya kutetereka kwa hali ya amani
na utulivu Mbalozi hao wanapaswa kuzitangaza fursa ya kiuchumi zilizopo
Nchini na kuzihusisha na hali ya amani na utulivu uliopo Nchini
Tanzania.
Alieleza kuwa amani na utulivu ni miongoni mwa vigezo muhimu vya awali
vinavyozingatiwa na wawekezaji pamoja na wageni wanaotaka kwenda nje ya
nchi zao kwa nia ya kuwekeza na kufanya biashara.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr Ali Moh’d Shein
amezipongeza juhudi kubwa zinazoendelea kuchukuliwa na Ofisi za
Kibalozi za Tanzania kwa kufanya kazi kwa karibu na Wizara ya Nchi,
Ofisi ya Rais, Ikulu na Utawala Bora Zanzibar katika masuala yanayohusu
Diaspora.
Alisema Wananchi wameshuhudia mafanikio makubwa yaliyopatikana katika
kipindi kifupi tokea kuanzishwa kwa Idara inayohusika na Diaspora ambapo
imeweza kushajiisha ushiriki wa Wanadiaspora katika utekelezaji wa
mipango ya Maendeleo hasa katika sekta ya Elimu, Afya, Utalii na
Uwekezaji.
Dr. Shein alionyesha faraja yake kutokana na Washiriki wa Mkutano huo wa
Nne wa Mabalozi wa Tanzania kujadili matarajio ya Diaspora kwa Serikali
na Balozi hizo kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo.
Alisema Mada hiyo imekuja wakati muwafaka ambapo Serikali zote mbili
zimekuwa zikitunga sera na sheria mbali mbali zenye malengo ya
kuimarisha ushiriki wa Wanadiaspora katiika harakati za maendeleo na
masuala mengine ya kiuchumi pamoja na kijamii.
Mkutano huo wa Nne wa Mabalozi wa Tanzania uliofunguliwa na Rais wa
Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete umejadili
mada tofauti ikiwemo Mwenendo wa Uchumi wa Tanzania, Mwelekeo wa
utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo pamoja na Utangamano wa
Kikanda na fursa zilizopo kwa Tanzania.
Mapema Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania
Mh. Bernard Membe alisema utekelezaji wa sera ya mambo ya nje inayolenga
katika Diplomasia ya Uchumi umeleta faida kubwa katika uchumi wa Taifa
ndani ya kipindi cha miaka kumi iliyopita.
Waziri Membe alisema ipo miradi kadhaa ya kiuchumi iliyotokana na sera
hiyo kufuatiwa kutanganzwa na Ofisi za Kibalozi za Tanzania akiitaja
kuwa ni pamoja na misaada ya maendeleo iliyofadhiliwa na mpango wa
Milenia wa Marekani MCC na mradi wa chuma wa Mchuchuma.
Mh. Membe alisisitiza pia kuwa ipo miradi ya ujenzi wa Bandari ya
Bagamoyo, Tanzania kusamehewa mikopo tofauti kutoka kwa baadhi ya
wafadhii, mradi wa huduma za maji safi unafadhiiwa na Serikali ya Japan
pamoja na mradi wa Kilimo kwa upande wa Visiwa vya Zanzibar.
Alisisitiza kwamba Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia
Wizara ya Mambo ya nje itahakikisha kwamba inaendelea kuchangia vikosi
vya kulinda amani Barani Afrika.
Akitoa shukrani kwa niaba ya washiriki wa Mkutano huo wa Nne wa Mabalozi
wa Tanzania Nchi Mbali mbali Duniani Dini wa Mabalozi hao Balozi
Kijazi alisema Maalozi hao wakirudi vituoni mwao watakuwa na kazi moja
tu ya kutekeleza yale waliyoyajadili na kukuibaliana katika Mkutano huo.
Balozi Kijazi alilihakikishia Taifa kwamba Mabalozi hao wana nia safi ya
kutekeleza majukumu yao kwa ufasini uliotukuka, lakini lakuzingatia
zaidi ni uwezeshwaji wao ili kutekeleza vyema kazi yao hiyo ya
Kidiplomasia.