Mwakilishi wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania {
RED CROSS } Bwana Shaaban Ali Iddi akikabidhi msaada wa Viatu Pair 90 kwa
Katibu wa Kamati ya Taifa ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar Dr. Khalid Salum
Moh’d kwa ajili ya watoto wa familia zilizopata maafa ambao wapo Kambini Skuli ya mwanakwerekwe “C” .
Katibu wa Kamati ya Taifa ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar Dr.
Khalid Salum Moh’d akiushukuru Uongozi wa Red Cross kwa misaada yao ya Kibinaadamu
waliyotoa kwa ajili ya familia zilizopatwa na maafa wiki iliyopita. Wanaoshuhuria
kutoka kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa
Red Cross Tanzania Bwana Salum Juma na Mjumbe wa Red Cross Mkoa Mjini Magharibi
Bwana Mwinyi Khamis Hamad.
Uongozi wa Chama cha Msalaba mwekundu Tanzania ukimsikiliza Katibu wa
Kamati ya Taifa ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar Dr. Khalid Salum Moh’d hayupo
pichani akitoa nasaha zake baada ya kupokea msaada uliotolewa na Uongozi huo. Kutoka Kulia
ni Mwakilishi wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania { RED
CROSS } Bwana Shaaban Ali Iddi, Mjumbe wa Red Cross Mkoa Mjini Magharibi Bwana
Mwinyi Khamis Hamad na Makamu Mwenyekiti wa Red Cross Tanzania Bwana Salum
Juma.
Picha Hassan Issa–OMPR – ZNZ.
Press Release:-
Chama cha
Msalaba mwekundu Tanzania { red Cross } kimekabidhi msaada wa viatu Pair 90 kwa
ajili ya watoto wa familia zilizowekwa
Kambini katika Skuli ya Sekondari ya Mwanakwerekwe
“C” baada ya Nyumba zao kujaa maji ya mvua.
Msaada huo
umefuatia Mvua za Masika zilizotokea usiku wa kuamkia Tarehe 3 Mei mwaka huu na
kuleta maafa makubwa yaliyosababisha zaidi ya
Nyumba 700 kuathirika ndani ya
Mkoa wa Mjini Magharibi na kuzikosesha makaazi Familia zilizokuwa zikiishi
katika nyumba hizo.
Ujumbe wa Red Cross Mkoa wa Mjini Magharibi
ukiongozwa na Mwakilishi wa Mkutano Mkuu wa Chama hicho Bwana Shaaban Ali Iddi
umekabidhiwa msaada huo kwa Katibu wa Kamati ya Taifa ya Kukabiliana na Maafa
Zanzibar ambae pia ni Katibu Mkuu Ofisi
ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Dr. Khalid Salim Moh’d hapo Ofisini kwake
Vuga Mjini Zanzibar.
Akizungumza
katika hafla hiyo fupi Bwana Shaaban Ali Iddi alisema Uongozi wa Red Cross
ulifikia hatua ya kutoa msaada huo baada ya kugundua kwamba idadi kubwa ya watu waliohifadhiwa kwenye
kambi ya dharura ya Mwanakwerekwe “C” ni Watoto wadogo.
Alisema Red
Cross imeguswa na tukio hilo la mafuriko hivyo licha ya juhudi wanazochukuwa za
kutoa misaada mbali mbali ya huduma lakini pia ikawajibika kuongeza msaada huo
wa Viatu ambao kwa kiasi kikubwa utawasaidia watoto hao.
Mwakilishi
huyo wa Mkutano Mkuu wa Red Cross Taifa aliyaomba Mashirika na Taasisi nyengine
za Kitaifa na Kimataifa kuendelea kuguswa na Tukio hilo na kutoa misaada kwa
jukumu hilo si vyema ikaachiwa pekee Serikali Kuu.
Akipokea
Msaada huo Katibu wa Kamatio ya Taifa ya
Kukabiliana na Maafa Zanzibar ambae pia ni Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili
wa Rsis wa Zanzibar Dr. Khalid Salum Moh’d aliipongeza Red Cross kwa jitihada
zake inazoendelea kuchukuwa katika kusaidia huduma za Kijamii.
Dr. Khalid
alisema Viongozi na Wanachama wa Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania muda wote
wamekuwa karibu na Serikali hasa wakati yanapotokea matukio ya majanga na
maafa.
Katibu huyo
wa Kamati ya Taifa ya kukabiliana na Maafa Zanzibar aliupongeza Uongozi wa Red
Cross kwa hatua yake hiyo ambayo itasaidia kupunguza machungu ya Watoto hao,
wengi kati yao wamepoteza vitu vyao vyote zikiwemo nguo na hata madaftari ya
Skuli.
Alisema
Kambi ya dharura ya Mwanakwerekwe “ C “ hivi sasa ina zaidi ya watoto 74 walio
chini ya umri wa miaka 14 wanaoendelea
kuhifadhiwa ambao watafaidika na msaada huo wa viatu.
“ Asilimia
kubwa ya Watoto hao waliopo Kambini wamepoteza Vitu vingi ikiwemo Madaftari ya
Skuli, Nguo, Viatu na vitu vyengine muhimu wanavyotumia ambavyo vingi kati yao
tayari Idara ya Maafa kupitia Taasisi na Mshirika hisani wameshapatiwa “.
Alifafanua Da. Khalid Salum Moh’d.
Pia aliyashukuru na kuyapongeza Mashirika na
Taasisi za Umma na hata zile Binafsi zilizojitolea kutoa misaada mbali mbali ya
Kibinaadamu na kuziomba zisichoke kwa vile bado mahitaji zaidi kwa waathirika
hao yanahitajika.
Katibu huyo
wa Kamati ya Taifa ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar alieleza kwamba Serikali
imeandaa mpango maalum wa usafiri kwa
watoto wote waliopo Kwenye Kambi ya dharura Mwanakwerekwe “C” kuendelea na
masomo yao kwenye skuli mbali mbali wanazotoka.
Dr. Khalid
aliwatoa hofu Wazazi wa Watoto hao kwamba Gari zilizoandaliwa zimepangwa kuwachukuwa watoto hao na kuwapeleka kwenye Skuli zao
waanze masomo kama kawaida na kuwarejesha Kambini baada ya kumaliza masomo yao kwa kila kipindi
watachokuwapo kambini hapo..