Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiufunga Mkutano wa Nne wa siku Tatu wa Mabalozi wa Tanzania kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyejkiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein uliokuwa ukifanyika katika Hoteli ya Ramada Mjini Dar es salaam. Picha Hassan Issa – OMPR – ZNZ.
Press Release:-
Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewaasa wana Habari kutumia vyema kalamu zao sambamba na kuzingatia
maadili ya jukumu lao la kazi na kuepuka utashi unaoweza kuleta sintafahamu ambayo
inaweza kuibua malumbano na hatimae
chuki kati yao na Viongozi.
Balozi Seif
ametoa nasaha hizo kufuatia Taarifa ya Gazeti moja Nchini lililochapisha
Taarifa yenye kichwa cha Habari “ Makamu
wa Rais Zanzibar amuunga mkono Membe “ wakati aliufunga Mkutano wa Nne wa
Mabalozi wa Tanzania Nchi mbali mbali Duniani uliokuwa ukifanyika katika Hoteli
ya Ramada Jijini Dar es salaam.
Balozi Seif
akionyesha mshangao na kusikitishwa kwake
kutokana na Taarifa hiyo alisema alichokitamka wakati akikaribishwa na
Waziri Membe kuufungua Mkutano huo ni kumtakia safari njema Waziri huyo ambayo
ni ngumu.
Alisema
alichowajibika na ndicho alichokifanya kwenye Mkutano huo ni kumuwakilisha Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein
kuufungua Mkutano huo wa Babalozi na si kuzungumzia siasa ambapo sio mahala
pake.
Balozi Seif
alifafanua kwamba utashi wa kuandikwa kwamba anamuunga Mkono Waziri Membe una
lengo la kutaka kumvuruga kisiasa kutokana na wadhifa wake akiwa Mmoja wa Viongozi
wa Juu wa Serikali hapa Nchini.
“ Mimi kazi
niliyokwendea pale ni kumuakilisha Bosi
wangu Rais wa Zanzibar kuufunga mkutano ule kwa niaba yake. Sasa hili la kusema
nitamuunga mkono Waziri membe bega kwa bega nimelitoa wapi na saa ngapi ? Nilimwambia namtakia safari njema lakini
nikamuasa aelewe kwamba ni safari ngumu ” .
Alifafanua Balozi Seif.
Alisema
wajibu na maadili ya Viongozi wakuu ni Kumuunga mkono Mgombea ambaye tayari ameshachaguliwa katika
ngazi ya juu ya Chama kwa ajili ya kuingia katika kinyang’anyiro cha Uchaguzi
Mkuu.
Balozi Seif
alieleza kuwa hatua hiyo imewekwa ili kuwepusha shari na mgawanyiko baina ya
viongozi hao jambo ambao linaweza kusababisha mtafaruku endapo Viongozi hao wataamua kujiingiza katika makundi
na ndivyo anavyoamini yeye katika muda wake wote.
Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar aliviomba vyombo vya Habari hasa Wahariri wa Vyombo
hivyo kuhakikisha kwamba wataendelea kubeba dhima katika kuwapasha Habari
Wananchi endapo watakuwa wakitoa Taarifa zenye muelekeo wa kusababisha vurugu
na mgawanyiko baina ya Jamii.
Alisema zipo
Nchi zilizoshuhudiwa kuingia katika migogoro ya Kisiasa na Kijamii na hatimae
kusababisha maafa na Nakama kutokana na Kalamu wa Waandishi zilivyokuwa
zikichochea shari na balaa.