Tuesday, 19 May 2015

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akieleza wakati alipofanya ziara fupi ya kukagua Nyumba zilizoathirika na Mvua Kubwa

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akifanya ziara ya kukagua Nyumba zilizoathirika na Mvua Mkubwa ya Hivi Karibuni ambazo zimeanguka baadhi ya Kuta zake. Picha na Hassan Issa  OPMR – ZNZ
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja Haji Juma Haji aliyevaa shati ya Drafti na Kofia kati kati akimfahamisha Balozi Seif Kulia yake kadhia iliyowapata baadhi ya wananachi waliangukiwa na kuta za nyumba zao ndani ya Mkoa huo. Picha na Hassan Issa  OPMR – ZNZ.
Balozi Seif akimkabidhi Saruji, Matofali na Mchanga Bwana Khamis Haji Machano ikiwa ni mchango utakaomsaidia kuanza matengenezo mengine ya nyumba yake. Picha na Hassan Issa  OPMR – ZNZ.

Balozi Seif akimfariji na kumpa Pole Mzee Tanzilu Waziri Muharizo wa Kijiji cha Pitanazako Geuni Kikombe Tele baada ya ukuta wa Nyumba yake kubomoka kutokana na Mvua kubwa za hivi karibuni.  Picha na Hassan Issa  OPMR – ZNZ.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akimkabidhi mchango wa Fedha Taslim Bibi Tatu Simai Ali wa Kijiji cha Upenja baada ya kuta za nyumba yake kubomoka kufuatia Mvua kubwa za Masika. Picha na Hassan Issa  OPMR – ZNZ
Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi akikabidhi Mchango wa shilingi Milioni 1,000,000/- Taslim zilizotolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi na Utumishi wa Umma Mh. Haroun Ali Suleiman kutekeleza ahadi aliyoitoa kwa Kikundi cha Ushirika cha Saccos cha Kijiji cha Upenja. Picha na Hassan Issa  OPMR – ZNZ





















Baadhi ya Wanachama wa Saccos ya Kijiji cha Upenja wakisikiliza nasaha za Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif hayupo pichani wakati akikabidhi ahadi ya fedha zilizotolewa na Waziri Haruon Ali Suleiman. Picha na Hassan Issa  OPMR – ZNZ.

 Press Release:-

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Wananchi wake katika kuona changamoto na matatizo yanayowakumba Wananchi hao ikiwemo majanga na Maafa  yanapatiwa ufumbuzi wa uhakika kadri hali ya uwezeshaji itakavyoruhusu.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  Ali Iddi alieleza hayo wakati alipofanya ziara fupi ya kukagua Nyumba zilizopata athari kutokana na kuanguka kwa baadhi ya kuta zake kufuatia Mvua kubwa za Masika zilizonyesha hivi karibuni.
Balozi Seif Ali Iddi akifuatana na Uongozi wa Serikali pamoja na wa  Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Kaskazini Unguja alikabidhi mchango wa Matofali, Saruji, Mchanga na fedha taslimu ikiwa ni hatua ya kutoa mkono wa pole kwa Wananchi waliopatwa na maafa ya kubomokewa kwa Nyumba zao.
Akikabidhi michango hiyo kwa Bwana Khamis Haji Machano wa Kijiji cha Pitanazao Kizimbani,Bwana Tanzilu Waziri muharizo wa Kijiji cha Pitanazako Geuni Kikombe Tele, Bibi Tatu Faki Ali wa Pita nazako pamoja na Bibi Tatu Simai Ali wa Kijiji cha Upenja Balozi Seif alisema Serikali imeshtushwa na Mtihani uliowapata wananchi wake hao.
Alisema kwa vile mtihani huo ni kazi ya Muungu Wananchi hao wanapaswa kujitahidi kufanya matengenezo au kujenga tena nyumba zao kwa lengo la kupata hifadhi na kuendelea na maisha yao ya kawaida.
Balozi Seif aliwashauri Wananchi hao kuanza na hatua za awali za marekebisho hayo kutokana na kianzio cha msaada huo ukijumuishwa na ule uliotolewa na Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Sheni, Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi kwa kushirikiana na Mfanyabiashara maarufu ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mh. Moh’d Raza.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif mbae pia ni Mbunge wa Jimbo la Kitope alikabidhi mchango wa Shilingi Milioni Moja taslim                 { 1,000,000/- } zilizotolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi na Utumishi wa Umma  Mh. Haroun Ali Suleiman kutekeleza ahadi aliyoitoa kwa Kikundi cha Ushirika cha Saccos cha Kijiji cha Upenja wakati alipokuwa Waziri wa Uwezeshaji Wananchi.
Balozi Seif na yeye akiwaahidi Wanachama wa Saccos hiyo ya Upenja kuwapatia  mchango wa Shilingi Laki 500,000/- kuendeleza Ushirika wao aliwapongeza wana saccos hao kwa  umahiri wao wa kuendelea kuilea Saccos hiyo.
Alifahamisha kwamba umahiri huo umewezesha kuzishinda changamoto mbali mbali walizokumbana nazo jambo ambalo limekwenda sambamba na Ilani na sera ya Chama cha Mapinduzi ya Kuimarisha Vikundi vya Ushirika nchini ambavyo ni mkombozi kwa Wananchi walio wengi hasa Vijijini.
Aliwataka wajitahidi zaidi katika kuimarisha miradi yao ya kilimo cha mboga mboga pamoja na biashara ya kukopesha huku wakihakikisha kwamba mwanachama anayepoka analipa kwa wakati.
Balozi Seif alitahadharisha kwamba Vikundi vingi vya Ushirika hapa nchini vilianzishwa kwa mitaji mikubwa lakini vimeshindwa kuendelea ndani ya kipindi kifupi kutokana na ukosefu wa uwazi na uaminifu.
Mapema Katibu wa Ushirika wa Saccos wa Kijiji cha Upenja Bwana Khamis Mussa Kwaza alisema Saccos yao imeanzishwa mwaka 2007 ikiwa na wanachama 33 wa Kike na Kiume.
Bwana Khamis Mussa alisema Ushirika wao unaendeshwa kupitia mradi wa Kibiashara kwa kutumia hisa pamoja na kilimo cha mboga mboga mambo ambayo yamewapatia mafanikio makubwa tokea kubuniwa kwa saccos hiyo karibu miaka Minane iliyopita.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Meja Mstaafu Juma Kassim Tindwa aliwatanabahisha wananchi wa Mkoa huo kuwaangalia Viongozi wenye nia thabiti ya kutaka kuwahudumia kikweli.
Meja Mstaafu Tindwa aliwakumbusha wananchi hao kwamba Kiongozi mkweli ni yule mwenye kukubali kubeba dhima ya kutaka kusaidia miradi ya wananchi pamoja na kutafuta mbinu za kuwaondoshea changamoto zinazowakabili katika harakati zao za kujitafutia maendeleo kwa ustawi wa familia zao.