Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi

Mwanafunzi Isra Hilal Mwadini akifuatiwa na mwenzake Tamima Abass Sheha wakipokea zawadi kutoka kwa mgeni rasmi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif wakati wa hafla ya Maulidi ya Jumuiya ya Chuo cha Samael Academy.Kulia ya Balozi Seif ni Rais wa Sameil Academy Sheikh Nassir Bin Said.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizindua rasmi Bara bara ya pili ya Amani hadi Mtoni baada ya kukamilika awamu ya mwisho ikiwa ni shamra shamra za maadhimisho ya kutimia miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar

Akiwa na Balozi mdogo wa India nchini Tanzania wakiangalia maonyesho yaliofanya na Msanii kutoka India, Bi Navi Madhav hapo Ngome Kongwe

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Dk. Khalid S. Mohamed

akizungumza na Wadau wa Maendeleo wa Mfuko wa TASAF, walipofika Ofisini kwake kuzungumzia maendeleo ya Mfuko wa TASAF III,na kutembelea Mradi wa Mpango wa Kunusuru Kaya masikini (PSSN) katika Jimbo la Muyuni Wilaya ya Kusini Unguja katika Kijiji cha Muyuni B

Wazir wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar

Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakifurahia jambo wakati wa semina ya siku moja kuhusu matokeo makubwa na ya haraka katika kuleta mageuzi ya kiuchumi na kuleta maendeleo nchini iliyofanyika leo katika ukumbi wa Ikulu Mjini Unguja na kufunguliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein

Tuesday, 28 July 2015

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akilifungua rasmi Jengo Jipya la Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia Tanzania { COSTECH } Ofisi ya Zanzibar

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akilifungua rasmi Jengo Jipya la Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia Tanzania{ COSTECH } Ofisi ya Zanzibar liliopo ndani ya majengo ya zamani ya ilichokuwa kiwanda cha Sigara Maruhubi Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar. Picha na Hassan Issa – OMPR
Balozi Seif wa pili kutoka Kushoto akipata maelezo kutoka kwa Wataalamu  wa Chuo cha Utafiti Kizimbani  wakiongozwa na Said Suleiman Bakari jinsi zao la viazi vitamu linavyoweza kutumiwa vyema katika utengenezaji wa Juisi. Wa kwanza kutoka kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Majini Magharibi Mh. Abullah Mwinyi. Picha na Hassan Issa – OMPR
Watafiti na wawakilishi wa Vikundi vya wajasiri amali waliopata ufadhili kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia wakimpatia maelezo Balozi Seif wakati akiangalia maonyesha mara baada ya kulifungua Jengo la Tume hiyo. Picha na Hassan Issa – OMPR
Baadhi ya Wataalamu na wajasiri amali kutoka vikundi tofauti Nchini wakifuatilia matukio mbali mbali yaliyojiri kwenye hafla ya uzinduzi wa jengo Jipya la Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia { COSTECH }. Picha na Hassan Issa – OMPR
Balozi Seif akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa Jengo la Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia hapo Maruhubi akimuwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la MapinduziI Dr. Ali Mohammed Shein. Picha na Hassan Issa – OMPR





















Balozi Seif akiwa katika Picha ya pamoja na wajumbe wa Bodi ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia Tanzania { COSTECH } mara baada ya uzinduzi wa jengo la Tume hiyo hapo Maruhubi. Kulia ya Balozi Seif ni Kaimu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Ali Juma Shamuhuna, Mkurugenzi Mkuu wa Costech Dr. Hassan Mshimba, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar {SUZA} Dr. Idriss Rai. Kushoto ya Balozi Seif ni Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia Kanal Mstaafu Joseph Simba Kalia, Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mh. Abdullah Mwinyi pamoja na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Ahmad Kassim.

Picha na Hassan Issa – OMPR

                                                                Press Release:-

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein alisema wakati umefika kwa sekta binafsi kujenga Utamaduni wa kutoa ruzuku za tafiti kwa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia ili ijipatie nguvu za ziada za uwezeshaji wa kuendesha shughuli zake za utafiti kama nchi nyengine Duniani zilizofanikiwa kwa kufuata mfumo huo.
Alisema kufanya utafiti kunahitaji nguvu kubwa ya fedha kiasi kwamba Serikali pekee haiwezi kumudu kugharamia bila ya kushirikisha taasisi mbali mbali za sekta binafsi za ndani na nje ya nchi.
Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohammed Shein alisema hayo katika Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati wa ufunguzi wa Jengo la Ofisi ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia { COSTECH } liliopo Maruhubi nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Alisema Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia Tanzania imeonyesha mwanga wa kusaidia jamii kwenye tafiti za kina za Kimaendeleo zitakazomkomboa Mtanzania kutoka katika dimbwi la umaskini na kuelekea kwenye maendeleo ya kweli.
Alieleza kwamba Costech imekuwa na jitihada katika uendelezaji wa rasilmali watu ya wataalamu waliopo Zanzibar inayowagharamiwa  kimasomo kwa shahada yao ya uzamivu na uzamili katika kiwango cha Master na Udokta kwenye vyuo mbali mbali ndani na Nje ya Nchi ambao kwa sasa wapo 22 kutoka Zanzibar.
“ Tume ya Taifa ya Sayansi na Tekonolojia pia tunaishukuru kwa kuratibu na kugharamia tafiti tofauti zinazosimamiwa na vyuo mbali mbali vya Zanzibar kama SUZA, IMS, ZIFFA na Taasisi ya Utafiti Kizimbani “. Alisema Dr. Shein.
Alifahamisha kwamba Costech kwa kushirikiana na Tume ya Mipango Zanzibar pamoja na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar tayari imeshaanda agenda ya utafiti ya Zanzibar ili Serikali iweze kuitumia katika maamuzi ya vipaumbele vya Tafiti kwa maendeleo ya jumla ya Taifa.
Dr. Shein alisema hilo ni jambo zuri katika muelekeo wa kunyanua ustawi wa Umma na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa upande wake itakuwa tayari kutumia matokeo  ya tafiti zinazofanywa na Wasomi wa hapa Nchini kupitia Tume hiyo.
Hata hivyo Dr. Shein aliitanabahisha Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia kwamba yale matokeo ya utafiti yanayostahili kuwafika moja kwa moja Wananchi yatolewe ili kuwapa fursa wananchi hao kuelewa kinachoendelea kwenye maisha yao ya kila siku.
Rais wa Zanzibar ameipongeza Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia kwa uamuzi wake wa busara wa kuanzisha Ofisi ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia.
Alisema uamuzi huu unadhihirisha wazi jinsi Tume hiyo Chini ya Wizara yake ilivyopania kukuza maendeleo ya Sayansi na Teknolojia kwa pande zote mbili za Muungano ambapo Taasisi hii ndio msimamizi na mshauri Mkuu wa Serikali kwa masuala yote yanayohusu sayansi, ugunduzi na Teknolojia kwa maendeleo ya Taifa.
Dr. Shein alielezea matumaini yake  binafsi na yale ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwamba  uwepo wa Ofisi ya Tume hiyo kutaongeza kasi kwa Wasomi wa hapa Nchini kuendelea kufanya tafiti mbali mbali na kuongeza kasi ya shughuli za ubunifu katika nyanja tofauti.
Rais wa Zanzibar alitoa wito kwa Taasisi nyengine za Serikali ya Muungano wa Tanzania na zile Binafsi za Tanzania Bara mbazo hazijafungua Ofisi zao hapa Zanzibar kufanya hivyo na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itakuwa tayari kuwapatia maeneo ya kujenga Ofisi hizo kwa lengo la kuwarahisishia Wananchi kupata huduma za karibu.
Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia COSTECH  Dr. Hassan Mshimba alisema ujenzi wa Ofisi ya Tume hiyo hapa Zanzibar  ni kutekekeza ahadi iliyotoa Uongozi wa Taasisi hiyo kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mwaka 2012.
Dr. Hassan Mshimba alisema kwamba Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia kwa kuona umuhimu wa zao la Mwani kwa Serikali ya Mapinduzi ilitoa Vihori 100 vya kubebea mwani kwa lengo la kuwawezesha wakulima wa zao hilo Unguja na Pemba kukuza Kilimo hich ikiwa ni miongozi mwa miradi sita inayotekelezwa na Tume hiyo kwa Upande wa Zanzibar.
Mkurugenzi Mkuu huyo wa Costech alisisitiza kwamba katika azma ya kukuza ajira Nchini Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia imekusudia kuungana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha vitengo vya Utafiti Zanzibar kama alivyosisitiza Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohammed Shein siku ya Utafiti Tarehe 12 Disemba mwaka 2014.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia Kanal Mstaafu Joseph Simba Kalia ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  kwa ukarimu wake wa kutoa Jengo kwa ajili ya Ofisi za Tume hiyo.
Kanal Mstaafu Simba Kalia alisema kitendo hicho kilichofanywa na  SMZ ni uthibitisho wa kuthamini umuhimu wa fani ya Utafiti ambayo ndio chachu ya maendeleo ya jambo lolote lile hapa Ulimwenguni.
Ofisi ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia ilizinduliwa  rasmi mnamo Tarehe 11 Juni Mwaka 2012 katika Majengo ya Ofisi ya Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania yaliyopo Tunguu Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar na kuanza kutoa huduma zake hapa Zanzibar.
Ofisi hiyo ya  Costech iliyofanyiwa matengenezo kwa kipindi cha miezi 12 imegharimu zaidi ya shilingi za Kitanzania Milioni 185,000,000/-  ikiwa na vyumba sita vya Ofisi pamoja na ukumbi wa Mikutano ipo kwenye  majengo ya zamani ya ilichokuwa Kiwanda cha utengezezaji Sigara baridi katika eneo la Maruhubi nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.



Monday, 27 July 2015

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiweka jiwe la msingi la Bara bara ya soko la mboga mboga Mtaa wa Mombasa hadi Skuli ya Sekondari ya Jang’ombe

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiweka jiwe la msingi la Bara bara ya ndani ya Kilomita 3.5  iliyoanzia soko la mboga mboga Mtaa wa Mombasa hadi Skuli ya Sekondari ya Jang’ombe inayojengwa na Uongozi wa Jimbo la Mpendae. Nyuma ya Balozi Seif ni Naibu Waziri wa Mindombinu na Mawasiliano Zanzibar Mh. Issa Haji Gavu na Kushoto ya Balozi Seif ni Mwakilishi wa Jimbo la Mpendae anayemaliza muda Mh. Moh’d  Said Dimwa. Picha na Hassan Issa – OMPR
Wana CCM na Wananchi wa Jimbo la Mpendae wakimpongeza Mbunge wao Mh. Salim Hassan Turky  mwenye kanzu nyeupe kati kati yao kwa uamuzi wake wa kuwapatia zawadi ya Bara bara ya ndani inayojengwa kwa kiwango cha lami kutoka Mtaa wa Mombasa hadi Jang’ombe. Picha na Hassan Issa – OMPR
Baadhi ya Wanachama wa Chama cha Mapinduzi na Wananchi wa Jimbo la Mpendae wakifuatilia matukio mbali mbali yaliyojiri kwenye hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa bara bara ya ndani kutoka Mtaa wa Mombasa  kwa Mchina hadi Skuli ya Sekondari ya Jang’ombe. Picha na Hassan Issa – OMPR





















Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akimpongeza Mbunge wa Jimbo la Mpendae Mh. Salim Hassan Turky kwa kusimamia vyema utekelezaji wa Ilani ya CCM ndani ya Jimbo lake  kwa asilimia 97%. Picha na Hassan Issa – OMPR

  Press Release:- 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewatahadharisha wananchi na wafuasi wa Vyama vya Siasa kuwa makini katika kuwachaguwa Viongozi watakaokubali kwa dhati kuwasimamia katika kupambana na changamoto zinazowazunguuka kwenye maeneo yao.
Alisema wakati wa kukumbatia watu wanaojali maslahi yao binafsi kwa kukumbuka shida za Wananchi wakati wa kuomba kura pekee kwa sasa umekwisha na unapaswa kuepukwa kwa nguvu zote.
Balozi Seif Ali Iddi alisema  hayo  wakati alipokuwa akizungumza na Wananchi pamoja na Viongozi wa Jimbo la Mpendae baada ya kuweka jiwe la msingi la Bara bara ya ndani iliyoanzia Soko la Mboga mboga  kwa Mchina hadi kumalizikia skuli ya Sekondari ya Jang’ombe.
Bara bara hiyo ya Kilomita Tatu Nukta Tano  inajengwa kwa gharama zilizotolewa na  Uongozi wa Jimbo la Mpendae zinazokisiwa kufikia Shilingi za Kitanzania Milioni 1,000,000/- katika kiwango cha Kifusi.
Balozi Seif alisema kazi ya Mbunge, Mwakilishi na Diwani katika Majimbo na Wadi  ni kusimamia utatuzi wa kero zinazoipata Jamii katika Majimbo husika. Hivyo Wananchi wana wajibu na haki ya kuwauliza wale wanaoomba ridhaa ya kutaka kuwaongoza watawafanyia nini watapowachagua.
Alifahamisha kwamba wapo baadhi ya Viongozi wanaoteuliwa na Wananchi kazi yao kubwa ni kupika majungu pamoja na kuleta malumbano yasiyo na msingi  na kusababisha upotevu wa muda badala ya ile kazi waliyoomba ya  kusimamia huduma za Kijamii.
“ Wapo baadhi ya Viongozi Majimboni kazi yao kubwa ni kuleta fitna na majungu ndani ya kipindi chao cha miaka mitano ambao baadaye hurudi tena kwa wananchi kuomba ridhaa bila ya juhudi zilizoonekana  za kuwaletea maendeleo wananchi waliowachagua “. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  Balozi Seif ameupongeza Uongozi wa Jimbo la Mpendae kwa uamuzi wake wa kuwapatia zawadi hiyo ya Bara bara Wananchi hao wa Mpendae.
Alisema ujenzi wa Bara bara unaofanywa na Serikali kwa kushirikiana na washirika wa Maendeleo wakiungwa Mkono na Viongozi wa Mjaimbo kwa zile bara bara za ndani lengo lake kuu ni kuwarahisishia Wananchi Usafiri.
Balozi Seif aliwataka Wananchi watakaoitumia Bara bara hiyo kuendelea kuilinda na kuitunza ili idumu kwa muda mrefu zaidi kwa vile tayari imeshakuwa mkombozi wao katika sekta ya mawasiliano ya usafiri wa Bara bara.
Akitoa Taarifa za ujenzi wa Bara bara hiyo Mbunge wa Jimbo la Mpendae Mh. Salim Hassan Turky alisema kwamba ujenzi wa Bara bara hiyo ya Mombasa hadi Jang’ombe ni zawadi maalum iliyoamuwa kutolewa na Uongozi wa Jimbo hilo kwa Wananchi wake.
Mh. Turky alisema zawadi hiyo imekuja kufuatia kazi kubwa iliyofanywa kwa pamoja kati ya  Uongozi na Wananchi hao katika kutekeleza  Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 -2015 kwa njia ya amani na utulivu  iliyowawezesha kufikia kiwango kizuri cha asilimia 97%.
Mbunge huyo wa Jimbo la Mpendae anayemaliza muda wake wa Miaka mitano alieleza kwamba endapo Wananchi wa Jimbo hilo wataamua kumpa ridhaa tena ya kuliongoza Jimbo hilo mkazo mkubwa utawekwa katika kubuni miradi ya amali pamoja na kuomba kibali Serikalini cha ujenzi wa Chuo cha amali iwapo watapatiwa eneo la ardhi.
Alisema mipango hiyo itakwenda sambamba na ujenzi wa kiwanda cha vibiriti lengo likiwa ni kujenga fursa za ajira kwa vijana wanaomaliza masomo yao ndani ya Jimbo hilo pamoja na Majimbo mengine hapa Nchini.
Naye Naibu Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar Mh. Issa Ussi Gavu alisema kwamba Serikali kupitia Wizara hiyo itaunga mkono juhudi zinazochukuliwa na Viongozi wa Majimbo katika ujenzi wa Bara bara za ndani.
Mh. Gavu alisema katika kuunga mkono jitihada zilizoonyeshwa na Uongozi wa Jimbo la Mpendae Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano itasaidia kuweka Lami kwenye bara bara hiyo licha ya kwamba bara bara za ndani zinapaswa kusimamiwa na Viongozi wa Majimbo.
Bara bara ya ndani iliyoanzia Soko la Mboga mboga  kwa Mchina hadi kumalizikia skuli ya Sekondari ya Jang’ombe ambayo haikuwamo ndani ya Ilani ya Uchaguzi ya Jimbo la Mpendae ni zawadi njema, nzuri na ya faraja iliyotolewa na Viongozi wa Jimbo hilo wanaomaliza muda wao wa utumishi wa miaka mitano.


Sunday, 26 July 2015

Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi akikabidhi msaada wa Kompyuta na Printa yake katika Skuli ya Sekondari ya Kitope, Madrasat Jamiiya Islamic ya Kijiji cha Mahonda na Skuli ya Sekondari ya Fujoni

Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi akimkabidhi msaada wa Kompyuta Tatu na Printa yake Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Sekondari ya Kitope Mwalimu Suleiman Juma Makame kwa ajili ya matumizi ya skuli hiyo. Picha na Hassan Issa – OMPR
Balozi Seif Ali Iddi akimkabidhi Msaada wa Kompyuta Moja Katibu wa Madrasat Jamiiya Islamic ya Kijiji cha Mahonda akitekeleza ahadi aliyoupa Uongozi wa Madrasa hiyo hivi karibuni. Picha na Hassan Issa – OMPR
Baadhi ya Wazazi na wajumbe wa Kamati ya Skuli ya Sekondari ya Fujoni wakifuatilia mambo mbali mbali wakati wa hafla fupi ya kukabidhiwa Skuli hiyo msaada wa Kompyuta na Prita yake kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi hayupo pichani. Picha na Hassan Issa – OMPR
Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Sekondari ya Fujoni Mwalimi Mabrouk Ishaq Daima akipokea msaada wa Kompyuta Tatu na Printa Moja kutoka kwa Mbunge wa Jimbo lao Balozi Seif Ali Iddi. Picha na Hassan Issa – OMPR

   Press Release:-

Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba Walimu Nchini bado wataendelea kuwa na dhamana kubwa ya kuwafinyanga wanafunzi katika kuelekea kwenye maadili mema yatakayowavua kutumbukia katika majanga ya migogoro na uvunjivu wa amani.
Alisema walimu ndio wahimili wakubwa wa amani kwa kuwaongoza wanafunzi wao kushinda mitego iliyoelekezwa kwao ambayo mara nyingi kuwashawishi kutumbukia katika matendo maovu.
Balozi Seif ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema hayo wakati akikabidhi Kompyuta Tatu na Printa Moja kwa Uongozi wa Skuli ya Sekondari ya Kitope pamoja na Skuli ya Sekondari ya Fujoni alizopewa msaada na Kampuni ya Kimataifa ya Mtandao wa Mawasiliano ya Kisasa ya ZTE ya Nchini China kwa ajili ya Skuli zilizomo ndani ya Jimbo lake.
Hafla hiyo fupi iliyofanyika katika skuli hizo mbili iliambatana pia na Balozi Seif kukabidhi Kompyuta Moja kwa Uongozi wa Madrasat Jamiiya Islamic ya Kijiji cha Mahonda kutekeleza ahadi aliyoupa wakati akizungumza nao.
Balozi  Seif alisema suala la amani ambalo linamuhusu kila mwana Jamii halina mbadala hasa katika kipindi hichi Taifa linakoelekea katika uchaguzi Mkuu wa Mwezi Oktoba mwaka huu.
Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope aliahidi kwamba ataendelea kuchangia maendeleo ya Wananchi hasa katika sekta ya elimu kadri fursa na uwezo utakavyomruhu.
Aliwahimiza Wanafunzi wa Skuli hizo kujitahidi kusoma kwa bidii kwa kuongeza nguvu zaidi katika masomo ya Sayansi na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano yanayoonekana kuwa na soko kubwa la ajira katika karne hii ya sayansi na Teknolojia.
Alizipongeza juhudi kubwa zinazoendelea kuchukuliwa na Walimu, Wazazi na Kamati za Skuli za Kitope na Fujoni ambazo zimesaidia kuzibadilisha Skuli hizo na kufikia katika kiwango kinachokubalika kimasomo.
“ Kitope ni moja ya Skuli inayofanya vyema kipindi hichi baada ya mikakati  imara iliyochukuliwa na Walimu na Kamati ya Skuli na mimi nikalazimika kuweka nguvu kufuatia matokeo ya wanafunzi wake kuzorota katika kipindi cha nyuma “. Alisema Balozi Seif.
“ Sekondari ya Fujoni kwa hivi sasa inatunavya uso kutokana na matokeo mazuri ya wanafunzi wake yaliyopelekea kwa sasa kuwa na madarasa ya Kidato cha Tano na Cha Sita. Hongereni Walimu na Wazazi “. Alifafanua Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope.
Akitoa Shukrani kwa niaba ya Walimu Wanafunzi, Wazazi wa Skuli hizo Mwenyekiti wa Kamati ya Skuli ya Kitope Bwana Makame Ali Mussa alisema Balozi Seif ataendelea kupata baraka za Wananachi wa Jimbo lake kutokana na moyo wake wa Kizalendo anaouchukuwa wa kuwasimamia Kimaendeleo.
Bwana Mussa alisema Jimbo la Kitope limepata mafanikio makubwa ya  Maendeleo ndani ya Kipindi cha miaka kumi ya Uongozi wa Balozi Seif hasa katika Sekta ya Mama ya Elimu ambayo ndio Mkombozi wa Jamii mahali popote pale.
Naye Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Sekondari ya Fujoni Mwalimu Mabrouk Ishaq Daima  alisema Msaada huo wa Kompyuta umefika wakati muwafaka kwa vile nusu ya zile zilizokuwa zikitumiwa na Wanafunzi zimechakaa baada ya kutoa huduma kwa muda mrefu.
Mwalimu Mabrouk  alimpongeza Balozi Seif kwa umakini wake wa kuongeza nguvu za michango na misaada katika Sekta ya Elimu inayofunza na kulea wataalamu wa fani mbali mbali.
Katika hafla hizo fupi zilizofanyika kwa nyakati tofauti kati ya Skuli ya Kitope na Skuli ya Fujoni Balozi Seif alipata fursa ya kulikagua Jengo la Darasa moja  lililkojengwakwa nguvu za Wananchi wenyewe katika Skuli ya Sekondari ya Kitope.
Akikagua Darasa na Vyoo vyake Balozi Seif Ali Iddi aliahidi kusaidia nguvu kwa kuchangia milango, madirisha, Dari pamoja na rangi  ili kukamilisha rasmi ujenzi  wa Darasa hilo.

Friday, 24 July 2015

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif AlI Iddi kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein akizinduzi Tamasha la Utamaduni wa Mzanzibari


Vazi lenye asili ya watu wa Kitumbatu walilokuwa wakilitumia wakati wakielekea mashambani huku mwana Mama anatembea akisuka ukili kuashiria ufundi wa utamaduni wa asili. Picha na Hassan Issa – OMPR
Muimbaji mahiri wa Visiwa vya Comoro al anisa Shamsia Sagaf akitumbuiza kwenye uzinduzi wa Tamasha la Utamaduni wa Mzanzibari hapo Bwawani Mjini Zanzibar.
Picha na Hassan Issa – OMPR
Kikundi cha akina mama watupu wakitumbuiza ngoma ya asili ya Lelemama kwenye uzinduzi wa Tamasha la Utamaduni wa Mzanzibari Mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein. Picha na Hassan Issa – OMPR




















Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif, Waziri wa Habari,utamaduni, Utalii na Michezo Mh. Said Ali Mbarouk pamoja na washabiki wa Tamasha wakimshangiria Kiongozi wa Ngoma ya Utamaduni ya Lelemama akifanya vitu vyake wakati wa uzinduzi wa Tamasha la Utamaduni wa Mzanibari. Picha na Hassan Issa – OMPR 

  Press  Release:-

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein amewakumbusha Wananchi wote Nchini kuelewa kwamba heshima na tabia njema iliyojengeka katika nyoyo za Watu wa Zanzibar kutokana na kupenda ufafiki, amani na utulivu ni sehemu muhimu ya utamaduni wa Wazanzibari.
Alisema ni muhimu kwa kila Mwananchi kuhakikisha anatoa mchango wake katika kulinda, kuukuza na kuutangaza utamaduni wa Mzanzibari kwa kuzingatia mambo mazuri wanayoyapenda wananchi wenyewe.
Dr. Ali Mohammed Shein  alitoa kauli hiyo wakati akilizindua Tamasha la 20 la Utamaduni wa Mzanzibari katika Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo katika Ukumbi wa Salama Hoteli ya Bwawani Mjini Zanzibar.
Alisema endapo mkakati wa makusudi utawekwa wa kuwashawishi wageni kuiga mambo ya asili na utamaduni wanaoutembelea bila shaka wageni na watalii hao watavutiwa na kuyapenda na hatimae masuala hayo yatalipatia sifa Taifa hili.
Rais wa Zanzibar Alisema kwamba Zanzibar ina Historia inayowavutia wageni mbali mbali kutokana na Utamaduni wenye mchanganyiko wa mambo mengi jambo ambalo limevipatia heshima ya pekee Visiwa vya Zanzibar.
Alisisitiza jukumu la kila Mwananchi kushiriki kikamilifu katika kuvikataa na kuvipinga vitendo vinavyotia doa,Desturi, mila na Utamaduni ikiwa ni pamoja na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia ambavyo hivi sasa Serikali inaendelea na juhudi mbali mbali za kuvikomesha.
Aidha alitoa wito kwa Wananchi waendelee kuunga mkono kampeni inayofanywa na Serikali Kuu dhidi ya unyanyasaji wa Kijinsia iliyoianzisha Tarehe 6 Disemba mwaka 2014 isemayo Zanzibar bila ya udhalilishaji wa kijinsia inawezekana.
Dr. Shein aliipongeza Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo kwa kushirikiana na Kamati Maalum ya Maandalizi na Uendeshaji  wa Tamasha la Utamaduni la Mzaznzibari kwa kuongeza kasi na ubunifu katika matayarisho yake na kulifanya kuwa bora kila mwaka tokea lilipoanzishwa mwaka 1994.
Alisema nidhahiri kuwa juhudi tiofauti zinazoendelea kuchukuliwa katika kuimarisha Tamasha hilo ni hatua muhimu katika kuendeleza mila, silka, desturi na utamaduni unatotoa fursa ya kukumbuka na kufahamu mambo yaliyokuwa yakifanywa wazee wa asili.
Alifahamisha kwamba ni vyema waandaaji wa Tamasha la Utamaduni la Mzanzibari wakafanya juhudi za ziada katika kuwaalika wageni waliowasili Nchini kwa ajili ya Tamasha la Kimataifa la Filam la Nchi za Jahazi kama njia muhimu hya kuutangaza Utamaduni wa Zanzibar na kulipa hadhi Kimataifa Tamasha hilo.
Rais wa Zanzibar alikelezea matarajio yake kwa waandaaji hao ia watafanya juhudi za kutosha za kuweka matangazo katika Mahoteli, Mitandao amoja na sehemu nyengine zinazopendwa na watalii ili wapate fursa za kuona na kuufahamu zaidi Utamaduni wa Mzanzibari.
Alieleza kuwa msimu wa utalii hivi sasa umeanza, hivyo wananchi wanaweza kuyatumia Matamasha kama hayo ikiwa ni vivutio muhimu vya Utalii kama zinavyofanya Nchi mbali mbali Duniani.
Dr. Shein alisema dhana ya Utalii kwa wote inahimiza uhusiano na ushirikiano wa kisekta kwa mujibu wa shughuli za kila mdau ili juhudi za kuutangaza utalii ziendelee kufanywa na sekta zote na faida zinazopatikana ziwafikie Wananchi wote.
“ Wizara inayosimamia Utamaduni inapaswa kushirikiana na Wizara ya uwezeshaji ili wananchi katika makundi yote waweze kuzitumia na kunufaika na fursa zinazoweza kupatikana kwa kuwepo kwa Tamasha la aina hii “. Alifafanua Dr. Shein.
Rais wa Zanzibar alielezea faraja yake kutokana na uongozi wa Tamasha hilo kumualika msanii wa muziki wa asili kutoka Comoro Bibi Shamsia Sagar kutoa burdani kwenye tamasha hilo mualiko utakaosaidia kuimarisha uhusiano kati ya Comoro na Zanzibar.
Aliishauri Wizara ya Habari, Utamudni, Utalii na Michezo ifanye juhudi za kasi kwa kualika wasanii wengine mashuhuri kutoka nchi za Mwambao wa Afrika na sehemu nyengine Duniani ambao ushiriki wao utalipa umaarufu Tamasha hilo na hatimae kuwavutia wageni na  washiriki wengi zaidi.
Mapema Kaimu Kamishna wa Kamisheni ya Utamaduni na Michezo Zanzibar Nd. Suleiman Mbarouk alisema Tamasha la Utamaduni wa Mzanzibari ni muendelezo wa Agizo la Rais wa Zanzibar la Kuitaka Kamisheni ya Utamaduni na Michezo kusimamia tamasha lifanyike kuanzia Tarehe 19 hadi 25 Mwezi Julai ya kila mwaka.
Nd. Suleiman alisema Tamasha hilo limesimama kwa takriban miaka mitatu sasa kutokana na kuingiliana na Mfungol wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan ambao kwa sasa kiindi hicho tayari kimebadilika na kutoa fursa ya kuendelea na Tamasha hilo kama kawaida.
Akimkaribisha Mgeni rasmi kuzindua Tamasha hilo la Utamaduni wa Mzanzibar  Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Zanzibar Mh. Said Ali Mbarouk alisema Tamasha hilo ni muhimu katika kukirithisha kizazi kipya kuelewa Utamaduni wao wa asili.
Mh. Mbarouk alisema Taifa lisilo na Utamaduni mara nyingi kizazi chake hutumbukia katika matatizo makubwa ya mmong’onyoko wa maadili, upotevu wa mila na silka zao.
Waziri wa Habari alifahamisha kwamba Tamasha la Utamaduni wa Mzanzibar lengo lake kuu ni kuwakumbusha wazazi kurejesha malezi ya heshima kwa kikazi chao kama walivyofanikiwa wao pamoja na mafunzo ya lugha sanifu ya Kiswahili inayokubalika katika jamii pahali popote.
Ujumbe wa Mwaka huu wa Tamasha la 20 la Utamaduni wa Mzanzibar ni:-               “ Tudumishe Utamaduni wetu katika hali ya amani, utulivu na Umoja “.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akipokea msaada wa Kampyuta kutoka katika Kampuni ya Kimataifa ya Mtandao wa Mawasiliano ya Kisasa ya ZTE

Ofisa wa Tawi la Kampuni ya Kimataifa ya Mtandao wa Mawasiliano ya Kisasa ya ZTE hapa Zanzibar yenye Makao Makuu yake Nchini  Jamuhuri ya Watu wa China Bibi Coco Wang akimpatia maelezo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kabla ya kumkabidhi msaada wa Kompyuta 10 kwa ajili ya wanafunzi wa Skuli zilizomo ndani ya Jimbo lake. Kulia ya Bibi Coco Wang ni Ofisa mwenzake wa Kampuni hiyo  Roy Chen Hafla iliyofanyika Ofisini kwa Balozi Seif hapo Mtaa wa  Vuga Mjini Zanzibar. Picha na Hassan Issa – OMPR




















Baadhi ya Kompyuta zilizotolewa msaada na Kampuni ya Kimataifa ya Mtandao wa Mawasiliano ya Kisasa ya ZTE Tawi la Zanzibar kwa ajili ya wanafunzi wa Skuli za Jimbo la Balozi Seif. Picha na Hassan Issa – OMPR 

 Press Release:-

Kampuni ya Kimataifa ya Mtandao wa Mawasiliano ya Kisasa ya ZTE yenye Makao Makuu yake Nchini  Jamuhuri ya Watu wa China imeahidi kuendelea kuunga mkono harakati za kiuchumi za Zanzibar katika kuona wananchi wake wanafaidika na mfumo wa kisasa wa mtandao wa mawasiliano.
Ofisa wa Tawi la Kampuni hiyo ya ZTE liliopo hapa Zanzibar Bibi Coco Wang alisema hayo wakati wa hafla fupi ya kumkabidhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi msaada wa  Kompyuta Kumi kwa ajili ya wanafunzi wa skuli zilizomo ndani ya Jimbo lake.
Akikabidhi msaada huo wa Kompyuta wenye thamani ya zaidi ya shilingi za Kitanzania Milioni 12,000,000/- Ofisini kwa Balozi Seif Vuga Mjini Zanzibar Bibi Coco Wang alisema Kampuni ya ZTE imejipanga kusaidia zaidi sekta ya elimu ambayo ndio msingi mkuu wa maisha ya mwanaadamu.
Bibi Coco alisema mfumo wa mafunzo katika vyuo na hata baadhi ya skuli za sekondari unaotumika katika Mataifa mbali mbali yaliyoendelea unaweza kutumika hapa Zanzibar endapo itaimarisha zaidi miundo mbinu ya mtandao wake wa  mawasiliano ya Compyuta.
Akipokea msaada huo wa Kampyuta Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliupongeza Uongozi wa Kampuni hiyo kwa moyo wake wa kujitolea katika kusaidia mtandao wa mawasiliano ya kisasa hapa Zanzibar.
Balozi Seif alisema Kampuni ya ZTE imeonyesha uungwana mkubwa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kiasi ambacho unafaa kuigwa na Makampuni mengine makubwa katika kusaidia jamii.
Kampuni ya Kimataifa ya Mtandao wa Mawasiliano ya Kisasa ya ZTE yenye Makao Makuu yake Nchini  Jamuhuri ya Watu wa China ndiyo iliyofadhili mradi wa ufungaji Kamera za  kurikodi matukio mbali mbali ya kila siku { CCTV CAMERA } katika eneo la Mji Mkongwe wa Zanzibar.
Ufadhili huo umekuja Zanzibar kufuatia ziara ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyoifanya Nchini Jamuhuri ya Watu wa China mwishoni  mwa mwaka uliopita.

Balozi Seif Ali Iddi akifanya ziara katika Kijiji cha Kinduni Wilaya ya Kaskazini “B” kukagua Kisima cha maji safi na salama kilichochimbwa na Mamlaka ya Maji Zanzibar {ZAWA }

Mkurugenzi Uzalishaji Maji wa Mamlaka ya Maji Zanzibar {ZAWA } Mhandisi Moh’d Elyas aliyenyanyua mkono akimpatia maelezo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kazi zilizobakia katika kukamilisha Miundombinu ya ujenzi wa kisima cha Maji safi katika Kijiji cha Kinduni Wilaya ya Kaskazini “B”. Picha na Hassan Issa – OMPR
Balozi Seif akizungumza na Wananchi na wana Saccos wa Kijiji cha Kinduni baada ya kukagua harakati za ujenzi wa Kibanda pamoja na Kisima cha Maji katika Kijiji hicho pamoja kutekeleza ahadi aliyotoa kwa kikundi hicho ya kusaidia matofali na saruji kwa ujenzi wa Jengo lao. Picha na Hassan Issa – OMPR



















Balozi Seif akimkabidhi Mwenyekiti wa Kikundi cha Saccos cha Kijiji cha Kinduni Nd. Abdulla Mihando mchango wa fedha kwa ajili ya ununuzi wa saruji na matofali akitekeleza ahadi aliyoitoa kwa kikundi hicho hivi karibuni. Picha na Hassan Issa – OMPR

                                          Press Release:-
Kisima cha maji safi na salama  kilichochimbwa na Mamlaka ya Maji Zanzibar {ZAWA } katika Kijiji cha Kinduni Wilaya ya Kaskazini “B” chenye uwezo wa kuzalisha Maji Lita elfu 80,000 kwa saa kinatarajiwa kuwakomboa Wananchi wa eneo hilo pamoja na Vijiji vya jirani kupata huduma hiyo muhimu.
Uchimbwaji wa Kisima hicho utaleta faraja  kwa Wananchi wa Kijiji cha Kindumi ambapo wataondokana na tatizo sugu la upatikanaji wa huduma hiyo katika muda si mrefu ujao baada  kukamilika kwa kazi ndigo ndogo zilizobakia.
Mkurugenzi wa Uzalishaji Maji wa Mamlaka ya Maji Zanzibar {ZAWA } Mhandisi Moh’d Elyas alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliyefika eneo hilo kukagua harakati za ujenzi wa Kibanda cha Maji katika Kisima hicho aliougharamia kwa lengo la kuwaondoshea tatizo la maji Wananchi hao.
Mhandisi Moh’d alisema kwamba kazi ya kukamilisha miundombinu iliyobakia katika eneo hilo inaweza kuchumuwa muda wa wiki moja mara tuu baada ya upatikanaji wa huduma za umeme katika eneo hilo.
“ Ikipatikana huduma ya Umeme katika Kibanda chetu hichi tuna uwezo wa kukamilisha kazi iliyobakia ya kuunganisha umeme na mabomba ya maji ndani ya wiki moja “. Alisema Mhandisi Elyas.
Alisema wahandisi wa Mamlaka ya Maji watalazimika  kuweka Pampu ndogo kwa wakati huu kulingana na Transfoma iliyopo jirani na eneo hilo licha ya kwamba kisima hicho kina uwezo wa kusambaza huduma za maji safi hadi katika Kijiji cha Kinyasini endapo itafungwa Mota kubwa.
Akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Kinduni pamoja na wana saccos ya Kijiji hicho Balozi Seif ambae pia ni Mbunge wa Jimbo la Kitope alisema kazi za Wawakilishi na Wabunge wakati wote ni kuwatumikia Wananchi.
Balozi Seif alisema katika kutekeleza wajibu huo aliwaahidi Wananchi hao kuchukuwa hatua za kugharamia usambazaji wa mabomba ya maji katika vitongoji vya Kijiji hicho.
Aliwashukuru Wananchi wa Kijiji cha Kinduni pamoja na Vitongoji vyake kwa ustahamilivu wao mkubwa waliouchukuwa wa kukosa huduma hiyo kwa kipndi kirefu.
Katika ziara hiyo Balozi Seif alikabidhi fedha Taslimu kutekeleza ahadi aliyoitoa hivi karibuni kwa Kikundi cha Saccos cha Kijiji cha Kinduni ya kuchangia Matofali pamoja na saruji kwa ajili ya ujenzi wa Jengo la wana saccos hao.
Mapema Diwani wa Wadi ya Mgambo Bibi Pili Said Mbonde kwa niaba ya Wananchi wa Kijji  hicho amemshukuru Balozi Seif kwa jitihada zake zilisaidia kuondosha tatizo la miaka mingi la Wananachi hao.
Bibi Pili alisema ukosefu wa huduma za maji safi na salama kwa takriban miaka Minane katika eneo hilo umechangia kuviza maendeleo na huduma zao za lazima za kila siku.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akilizindua Tamasha la 18 la Kimataifa la Filam la Nchi za Jahazi Zanzibar { ZIFF }

Wasanii wa Kikundi cha Tausi Kilicho chini ya Gwiji la Sanaa Nchini Bibi Maryam Hamdan kikitoa burdani ya Maulidi ya Homu kwenye uzinduzi wa Tamasha la 18 la Filam la Nchi za Jahazi  Zanzibar { ZIFF } hapo Hoteli ya Double Tree By Hilton Shangani Mjini Zanzibar.
Picha na Hassan Issa – OMPR
Wasanii wa Kikundi cha Tausi Kilicho chini ya Gwiji la Sanaa Nchini Bibi Maryam Hamdan kikitoa burdani ya Maulidi ya Homu kwenye uzinduzi wa Tamasha la 18 la Filam la Nchi za Jahazi  Zanzibar { ZIFF } hapo Hoteli ya Double Tree By Hilton Shangani Mjini Zanzibar. Picha na Hassan Issa – OMPR
Mkurugenzi wa Tamasha la Filam la Nchi za Jahazi Zanzibar { ZIFF } Profesa Martin Mhando akitoa neneo la makaribisho kwenye uzinduzi wa Tamasha hilo hapo shangani.
Picha na Hassan Issa – OMPR
Meneja wa Taasisi ya Kimataifa inayosimamia kukuza vipaji vya wasanii katika ukanda wa Afrika Mashariki { ZUKU } Bibi Maud Roger akiahidi taasisi yake kuendelea kusaidia vipaji vya vijana katika utengenezaji wa filam zilizo bora Nchini. Picha na Hassan Issa – OMPR
Baadhi ya washirika wa Tamasha la Filam la Nchi za Jahazi  Zanzibar { ZIFF } waliohudhuria uzinduzi wake kutimia miaka 18 tokea kuasisiwa kwa Tamasha hilo hapa Nchini. Picha na Hassan Issa – OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  wa Pili kutoka Kushoto akiwa mgeni rasmi kwa Niaba ya Rais wa Zanzibar Dr Ali Mohammed Shein akijumuika pamoja na baadhi ya viongozi kwenye uzinduzi wa Tamasha la 18 la Filam la Nchi za Jahazi Zanzibar hapo Double Tree By Hilton Shangani Mjini Zanzibar. Kulia ya Balozi Seif ni Waziri wa Habari, Utamduni, Utalii na Michezo Mh. Said Ali Mbarouk, kushoto ya Balozi Seif ni Mwenyekiti wa Bodi ya ZIFF Mh. Mahmoud Thabit Kombo na msanii wa filam ya sarafina kutoka Nchini Afrika Kusini Laleta Kumalo. Picha na Hassan Issa – OMPR
Mwenyekiti wa Bodi ya Tamasha la Filam la Nchi za Jahazi  Zanzibar { ZIFF } Mahmoud Thabit Kombo akitoa neno la kumkaribisha mgeni rasmi kulizindua Tamasha hilo hapo Double Tree By Hilton Shangani. Picha na Hassan Issa – OMPR
Msanii Mkongwe wa nyimbo kutoka Johannesburg Nchini Afrika Kusini  Doroth Masuka akipongeza juhudi zinazochukuliwa  na Serikali pamoja na washirika wake katika kuimarisha vipaji vya wasanii hapa Nchini. Picha na Hassan Issa – OMPR
Balozi Seif akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Viongozi  na washirika wa Tamasha la Filam la Kimataifa la Nchi za Jahazi mara baada ya kulizindua Tamasha hilo kwa niaba ya Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohammed Shein. Picha na Hassan Issa – OMPR



















Balozi Seif akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Viongozi  na washirika wa Tamasha la Filam la Kimataifa la Nchi za Jahazi mara baada ya kulizindua Tamasha hilo kwa niaba ya Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohammed Shein. Kulia ya Balozi sdEIF NI Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mh, Said Ali Mbarouk na Meneja wa Taasisi ya Kimataifa inayosimamia kukuza vipaji vya wasanii katika ukanda wa Afrika Mashariki { ZUKU } Bibi Maud Roger. Kushoto ya Balozi Seif ni Mwenyekiti wa Bodi ya Tamasha la Filam la Nchi za Jahazi  Zanzibar { ZIFF } Mahmoud Thabit Kombo pamoja na Msanii Maarufu Duniani aliyeigiza filam Maarufu ya Mchezo wa sarafina kutoka Nchini Afrika Kusini Bibi Laleta Kumalo. Picha na Hassan Issa – OMPR
    Press Release:-

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuunga mkono  juhudi zinazochukuliwa na Uongizi wa Tamasha la Kimataifa la Filam la Nchi za Jahazi  Zanzibar { ZIFF } katika azma yake ya kuijengea nguvu tasnia ya Filam Nchini inayoonekana kusaidia ukuaji wa uchumi kupitia sekta ya Utalii.
Kauli hiyo imetolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar Dr. Ali Mohammed Shein katika Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati  akilizindua Tamasha la 18 la Kimataifa la Filam la Nchi za Jahazi Zanzibar { ZIFF } hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Double Tree By Hilton Shangani Mjini Zanzibar.
Dr. Shein  alisema kwamba Tamasha la Nchi za jahazi limekuwa na mchango mkubwa katika kuitangaza Zanzibar Kimataifa hali ambayo imetoa ushawishi kwa wageni na watalii wengi kuamua kuvitembelea Visiwa vya Zanzibar kujionea mazingira na rasilmali zilizopo.
Alisema kupitia Tasnia ya filam zinazotayarishwa na wasanii mbali mbali kwa kushirikiana na wadau wa Fani hiyo chini ya Wataalamu wa Ziff wageni na watalii mbali mbali Duniani wamekuwa wakivutiwa na fukwe pamoja na Utamaduni  uliojaa ukarimu wa Watu wa Visiwa vya Zanzibar.
Rais wa Zanzibar aliushauri Uongozi wa Tamasha la Kimataifa la Filam la Nchi za Jahazi Zanzibar { ZIFF } kuendelea kufanya juhudi zaidi za kuwashawishi wasanii wa Kimataifa kuzitumia Fukwe na Tamaduni za Zanzibar katika kutengeneza Filam mbali mbali kwa lengo la kuitangaza zaidi Zanzibar Kimataifa.
“ Zanzibar  ni Visiwa vya maumbile ya Utamaduni ya Ukarimu pamoja na fukwe za kuvutia mambo ambayo yakitangazwa vyema wasanii wa Kimataifa wanaweza kushawishika kuyatumia katika kutengeneza Filamu zao “. Alifafanua Dr. Shein.
Alifahamisha kwamba Tamasha la Kimataifa la Filam la Nchi za Jahazi, Tamasha la Iddi, Tamasha la Mzanzibari pamoja na  Sherehe za Mwaka Kogwa zinazofanyika Makunduchi ni Mambo muhimu yanayopaswa kuimarishwa katika kukuza na kusimamia Utamaduni na Historia ya Zanzibar na Watu wake.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi amewapongeza Wasanii wa Maigizo pamoja na Filam Nchini  kutokana na kazi kubwa wanayoendelea kuifanya ya kuelimisha Jamii sambamba na kuwapatia Burdani.
Alisema mbali ya Tasnia hiyo kutoa ajira pana kwa kundi kubwa hasa Vijana Nchini lakini pia imepanua soko la filam za nyumbani na kuleta unafuu kwa kila mtu kumudu kununua na kuangalia kazi za wasanii wa hapa Nchini hali iliyopelekea kufikia asilimi 80% ya filamu za Kiswahili zinazoangaliwa tofauti na miaka iliyopita nyuma.
Mapema Meneja wa Taasisi ya Kimataifa inayosimamia kukuza vipaji vya wasanii katika ukanda wa Afrika Mashariki { ZUKU } Bibi Maud Roger aliahidi kwamba Taasisi yake itaendelea kukuza vipaji vya wasanii kwa lengo la kufikia kiwango kinachokubalika Kimataifa.
Bibi Roger alisema hatua hiyo muhimu itaweza kuwajengea uwezo wa kiajira badala ya kusubiri kutegemea zile za Serikali ambazo kwa sasa upo upungufu mkubwa hata katika Mataifa yaliyoendelea.
Meneja wa Taasisi hiyo ya Zuku alifahamisha kwamba mpango maalum umeandaliwa na Uongozi wa Taasisi hiyo baina ya miaka sita na kumi kwa kuwadhamini Vijana wapatao Kumi wanaopata Mafunzo ya msingi kuweza kutengeneza Filam zitazokubalika Kimataifa.
Wakitoa salamu zao kwenye uzinduzi wa Tamasha hilo la 18 la Kimataifa la Filam la Nchi za Jahazi Msanii Gwiji  Duniani kutoka Nchini Afrika Kusini Laleta Kumalo aliyeigiza filam Maarufu ya sarafina pamoja na Msanii Mkongwe wa Nchi Hiyo Doroth Masuka wameelezea faraja yao kutokana na Serikali kupitia taasisi za kijamii zilivyojikita katika kusaidia vijana kwenye fani ya sanaa.
Akimkaribisha mgeni rasmi katika uzinduzi wa Tamasha la 18 la Ziff Mwenyekiti wa Bondi ya Tamasha hilo Mahmoud Thabit Kombo alisema Ziff itaendelea kushirikiana na wadau wote wa ndani na nje ya nchi katika kuona Taasisi hiyo muhimu inazidi kuimarika.
Mahmoud Thabit Kombo alisema uimarikaji huo utawapa nguvu na ari Vijana walioamua kujiajiri kupitia Tasnia ya Filam inayoonekana kupata umaarufu siku hadi siku hapa Duniani.
Uzinduzi wa Tamasha hilo la 18 la Kimataifa la Filam la Nchi  za Jahazi Zanzibar       { ZIFF } limekwenda sambamba na siku yake lililoasisiwa rasmi Tarehe 18 Julai Mwaka 1997 likitimiza umri wa miaka 18 sasa.

Thursday, 23 July 2015

Balozi Seif Ali Iddi akitoa nasaha katika hafla fupi ya Kukabidhi Boti kwa Vijana Sita wa Kijiji cha Fujoni Wilaya ya Kaskazini “ B “ walioamua kuacha matumizi ya Dawa za kulevya

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimkamilishia Fedha zake Fundi Omar Makame Juma wa Boti aliyochonga kwa ajili ya Vijana Sita wa Kijiji cha  Fujoni walioamua kuacha matumizi ya Dawa za kulevya. Picha na Hassan Issa – OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliyevaa shati rangi ya Kijani akimkabidhi Boti na Mshine yake Kiongozi wa Vijana Sita wa Kijiji cha Fujoni walioamua kuacha matumizi ya Dawa za kulevya. Picha na Hassan Issa – OMPR
Boti iliyonunuliwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwa ajili ya Vijana Sita wa Kijiji cha Fujoni walioamua kuacha matumizi ya Dawa za kulevya. Picha na Hassan Issa – OMPR
Balozi Seif akirejesha Fomu  na kumkabidhi Katibu wa CCM Wilaya ya Kaskazini “ B” Bibi Subira Mohammed za kuwania nafasi ya kugombea Uwakilishi kwa Tiketi ya CCM Katika Jimbo Jipya la Mahonda. Kushoto ya Balozi Seif Ali Iddi ni Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi. Picha na Hassan Issa – OMPR




















Balozi Seif akitoka nje ya Ofisi ya CCM Wilaya ya Kaksaini B iliyopo Mhonda baada ya kurejesha Fomu za kuomba nafsi ya kugombea uwakilishi Jimbo la Mhonda. Kulia ya Balozi Seif akishindikizwa na Mwenyekiti wa CCM Wilayaya Kaskazini B Nd. Hilika Fadhil Khamis. Picha na Hassan Issa – OMPR


                                                        Press Release:-

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewanasihi Vijana kuwacha mawazo ya kufikiria kwamba ajira pekee itakayowasaidia kuendesha maisha yao ni ile ya Ofisini pamoja na vikosi vya ulinzi ambazo kutokana na wingi wa idadi yao hazitaweza kukidhi mahitaji yao.
Alisema wakati umefika kwa vijana wanaomaliza masomo yao kuanzisha vikundi vya ushirika vinavyojumuisha kazi za amali na Serikali Kuu itakuwa tayari kusaidia nguvu vijana hao katika kuwapatia vitendea kazi.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa nasaha hizo katika hafla fupi ya Kukabidhi Boti kwa Vijana Sita wa Kijiji cha Fujoni Wilaya ya Kaskazini “ B “ walioamua kuacha matumizi ya Dawa za kulevya baada ya kupata mafunzo ya wiki sita katika nyumba ya kurekebisha watu walioathirika na matumizi ya Dawa hizo.
Boti hiyo pamoja na Mashine yake aliyowakabidhi  Vijana hao pembezoni mwa Bahari ya Kijiji cha Mangapwani na kushuhudiwa na baadhi ya wananchi wa Vijiji Jirani vimegharimu jumla ya shilingi Milioni 11,000,000/-, kati ya fedha hizo boti ilichongwa kwa shilingi Milioni 7,000,000/- wakati mashine yake imetumia shilingi milioni 4,000,000/-.
Balozi Seif ambae alikuwa akitekeleza ahadi aliyowapa Vijana hao wakati alipowapokea Tarehe 16 Juni 2015 baada ya kumaliza mafunzo yao alisema chombo hicho kwa kiasi kikubwa kitawapa nafasi nzuri vijana hao kuendesha maisha pamoja na Familia zao.
“ Tafadhalini jitahidini kukitunza chombo hicho. Na iwapo kama kitakushindeni basi naomba  ni vyema mkanirejeshea kwa kuniuzia mwenyewe “. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaomba na kuwakumbusha vijana hao kujiepusha na uvuvi haramu uliopigwa marufuku na Serikali ambao unaweza kuharibu mazingira na hatimae lile lengo walilolikusudia kulifanya kwa kutafuta riziki ya halali litakosekana.
Akipokea msaada huo wa Boti pamoja na Mshine yake Mmoja wa Viongozi wa Vijana hao Ndugu Kombo Iddi Juma alimshukuru na kumpongeza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwa jitihada zake anazochukuwa za kusaidia makundi ya jamii hapa Nchini.
Ndugu Kombo alisema msaada huo wa Balozi Seif alioutoa katika kipindi cha mwezi Mmoja tu baada ya ahadi yake umeleta faraja kwao, Familia na hata wana Kijiji cha Fujoni.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi amerejesha Fomu akijiandaa kuomba fursa ya kuwania nafasi ya Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar katika Jimbo Jipya la Mahonda ndani ya Wilaya ya Kaskazini “B” Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Balozi Seif Ali Iddi ni Miongoni mwa Wanachama 11 wa CCM waliorejesha Fomu hizo hadi sasa tokea kuanza kwa zoezi hilo Tarehe 15 Mwezi huu katika kuomba nafasi za Uwakilishi  na Ubunge kwenye  Majimbo  Manne yaliyomo ndani ya Wilaya ya Kaskazini “B”.
Akipokea Fomu hizo Katibu wa Chama cha Mapinduzi wa Wilaya ya Kaskazini “B” Bibi Subira Mohammed alimtakia Balozi Seif Safari njema kwenye mchakato wa Uchaguzi Mkuu ujao kwa nafasi aliyoomba endapo atapata ridhaa ya Chama.
Kutokana na mabadiliko yaliyofanywa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar hivi karibuni Wilaya ya Kaskazini “B” hivi sasa ina Majimbo Manne ambayo ni Mahonda, Bumbwini, Donge na Kiwengwa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiipongeza Serikali ya Cuba kwa juhudi inayoendelea kuchukuwa katika kuunga mkono harakati za maendeleo ya Kijamii ya Zanzibar hasa katika Sekta ya huduma za Afya.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na Madaktari wa Cuba wanaomaliza muda wao wa utumishi hapa Zanzibar ambao aliwaandali chakula cha Jioni nyumbani kwake Mazizini nje kidogo ya Mji wa Zanzibar. Picha Hassan Issa – OMPR – ZNZ.
Balozi Seif akisalimiana na Mkuu wa Mafunzo wa  Madaktari Wazalendo wa Zanzibar  waliopata taaluma chini ya Madaktari Mabingwa wa Cuba Dr. Daisy Batlle kabla ya chakula cha jioni alichowaandalia Madaktari mabingwa wa Cuba. Picha Hassan Issa – OMPR – ZNZ.
BaloziSeif akibadilishana mawazo na Kiongozi wa Madaktari wa Cuba Profesa Ulpiano hapo nyumbani kwake Mazizini nje kidogo ya Mji wa Zanzibar. Picha Hassan Issa – OMPR – ZNZ.
Kiongozi wa Madaktari Mabingwa wa Cuba Profesa Ulpiano wa kwaza kutoka kulia akiwa pamoja na Mwenyeji wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar wakipata mlo kwenye hafla fupi waliyoandaliwa Madaktari hao. Picha Hassan Issa – OMPR – ZNZ.
Baadhi ya Madaktari Mabingwa wa Cuba wanaomaliza muda wao wa kazi hapa Zanzibar wakipata mlo  wa jioni nyumbani kwake  Balozi Seif Ali Iddi hapo Mazizini.Picha Hassan Issa – OMPR – ZNZ. 
Balozi Seif akimzawadia Kasha Kiongozi wa Madaktari wa Cuba Profesa Ulpiano mara baada yam lo wa jioni kama ishara ya kumbukumbu ya uwepo wao hapa Zanzibar. Picha Hassan Issa – OMPR – ZNZ.
Mkuu wa Mafunzo wa  Madaktari Wazalendo wa Zanzibar  waliopata Taaluma chini ya Madaktari Mabingwa wa Cuba Dr. Daisy Batlle akipokea zawadi kutoka kwa Balozi Seif. Picha Hassan Issa – OMPR – ZNZ.





















Balozi Seif Ali Iddi kati kati ya waliokaa kwenye viti akiwa katika picha ya pamoja na Madaktari Mabingwa wa Cuba wanaomaliza muda wao wa kutoa huduma za Afya hapa Zanzibar. Picha Hassan Issa – OMPR – ZNZ.

 Press Release:-

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeipongeza Serikali ya Cuba kwa juhudi inayoendelea kuchukuwa katika kuunga mkono harakati za maendeleo ya Kijamii ya Zanzibar hasa katika Sekta ya huduma za Afya.
Pongezi hizo zimetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi katika hafla Maalum ya chakula cha Jioni aliyowaandalia Madaktari Mabingwa wa Cuba wanaotoa huduma za Afya pamoja na kutoa mafunzo kwa Madaktari wazalendo wa Zanzibar.
Hafla hiyo iliyofanyika katika Makazi ya Balozi Seif yaliyopo Mazizini nje kidogo ya Mji wa Zanzibar imetayarishwa ili kuwaaga rasmi Madaktari hao baada ya kukamilisha muda wao wa kutoa huduma za Afya wa miaka miwili ambapo wanatarajiwa kurejea nyumbani Cuba Mwezi Septemba Mwaka huu.
Balozi Seif alisema kwamba huduma za afya zilizokuwa zikitolewa na Madaktari Mabingwa hao wa Cuba zimeweza kuleta faraja kubwa kwa Wananchi walio wengi hapa Zanzibar.
Alieleza kuwa yapo mafanikio makubwa yaliyopatikana kutokana na uimarishwaji wa mfumo wa huduma za afya uliopekelea kuongezeka kwa Madaktari wazalendo Nchini kasi ambayo imekwenda sambamba na ile azma ya Serikali ya kulenga kuwa na huduma za Afya katika maeneo yasiyozidi kilomita Tano.
Balozi Seif alisisitiza kwamba bado Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inahitaji kuongeza nguvu zaidi katika Sekta hiyo muhimu kwa ustawi wa Jamii ili kufikia kiwango bora cha utoaji wa huduma za afya kilichowekwa na shirika la Afya Duniani { WHO }.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliwatakia maisha ya furaha na upendo Madaktari hao wa Jamuhuri ya Cuba wakati watakaporejea Nyumbani kwao mnamo Mwezi Septemba mwaka huu wa 2015.
Katika hafla hiyo fupi ya chakula cha jioni Balozi Seif aliwazawadia Madaktari hao Makasha Maalum kama ishara ya ukumbusho wao wakati walipokuwepo hapa Zanzibar wakitoa huduma za Afya pamoja na kutoa mafunzo kwa Madaktari Wazalendo.
Akitoa shukrani kwa niaba wenzake Kiongozi wa Madaktari hao Profesa Ulpiano alisema wakati wa utumishi wao hapa Zanzibar walilazimika kufanya kazi kwa juhudi, bidii na maarifa kutokana na ukarimu walioupokea kutoka kwa Wananchi wa Zanzibar.
Profesa Ulpiano alisema kwamba Madaktari hao wa Cuba wataendelea kukumbuka maisha ya Zanzibar ambayo yaliwapa fursa ya kujihisi kwamba wanaishi katika maisha ya kifamilia kama wapo Nyumbani kwao Cuba.
Zanzibar imekuwa na uhusiano wa muda mrefu na Nchi za  Jamuhuri ya Cuba pamoja na Jamuhuri ya Watu wa China ambapo Mataifa hayo mawili yamekuwa yakiendeleza ushirikiano huo na Zanzibar kwa kusaidia kitaaluma huduma za Afya hapa Zanzibar tokea miaka ya 60 mara baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964.