Vazi lenye asili ya watu wa Kitumbatu walilokuwa wakilitumia wakati
wakielekea mashambani huku mwana Mama anatembea akisuka ukili kuashiria ufundi
wa utamaduni wa asili. Picha na Hassan Issa – OMPR
Muimbaji mahiri wa Visiwa vya Comoro al anisa Shamsia Sagaf akitumbuiza
kwenye uzinduzi wa Tamasha la Utamaduni wa Mzanzibari hapo Bwawani Mjini
Zanzibar.
Picha na Hassan Issa – OMPR
Picha na Hassan Issa – OMPR
Kikundi cha akina mama watupu wakitumbuiza ngoma ya asili ya Lelemama
kwenye uzinduzi wa Tamasha la Utamaduni wa Mzanzibari Mgeni rasmi alikuwa
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwa niaba ya Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein. Picha na Hassan Issa – OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif, Waziri wa
Habari,utamaduni, Utalii na Michezo Mh. Said Ali Mbarouk pamoja na washabiki wa
Tamasha wakimshangiria Kiongozi wa Ngoma ya Utamaduni ya Lelemama akifanya vitu
vyake wakati wa uzinduzi wa Tamasha la Utamaduni wa Mzanibari. Picha na Hassan Issa – OMPR
Press Release:-
Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein
amewakumbusha Wananchi wote Nchini kuelewa kwamba heshima na tabia njema
iliyojengeka katika nyoyo za Watu wa Zanzibar kutokana na kupenda ufafiki,
amani na utulivu ni sehemu muhimu ya utamaduni wa Wazanzibari.
Alisema ni
muhimu kwa kila Mwananchi kuhakikisha anatoa mchango wake katika kulinda,
kuukuza na kuutangaza utamaduni wa Mzanzibari kwa kuzingatia mambo mazuri
wanayoyapenda wananchi wenyewe.
Dr. Ali
Mohammed Shein alitoa kauli hiyo wakati
akilizindua Tamasha la 20 la Utamaduni wa Mzanzibari katika Hotuba iliyosomwa
kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo
katika Ukumbi wa Salama Hoteli ya Bwawani Mjini Zanzibar.
Alisema endapo
mkakati wa makusudi utawekwa wa kuwashawishi wageni kuiga mambo ya asili na
utamaduni wanaoutembelea bila shaka wageni na watalii hao watavutiwa na
kuyapenda na hatimae masuala hayo yatalipatia sifa Taifa hili.
Rais wa
Zanzibar Alisema kwamba Zanzibar ina Historia inayowavutia wageni mbali mbali
kutokana na Utamaduni wenye mchanganyiko wa mambo mengi jambo ambalo limevipatia
heshima ya pekee Visiwa vya Zanzibar.
Alisisitiza
jukumu la kila Mwananchi kushiriki kikamilifu katika kuvikataa na kuvipinga
vitendo vinavyotia doa,Desturi, mila na Utamaduni ikiwa ni pamoja na vitendo
vya unyanyasaji wa kijinsia ambavyo hivi sasa Serikali inaendelea na juhudi
mbali mbali za kuvikomesha.
Aidha alitoa
wito kwa Wananchi waendelee kuunga mkono kampeni inayofanywa na Serikali Kuu
dhidi ya unyanyasaji wa Kijinsia iliyoianzisha Tarehe 6 Disemba mwaka 2014
isemayo Zanzibar bila ya udhalilishaji wa kijinsia inawezekana.
Dr. Shein
aliipongeza Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo kwa kushirikiana na
Kamati Maalum ya Maandalizi na Uendeshaji wa Tamasha la Utamaduni la Mzaznzibari kwa
kuongeza kasi na ubunifu katika matayarisho yake na kulifanya kuwa bora kila
mwaka tokea lilipoanzishwa mwaka 1994.
Alisema
nidhahiri kuwa juhudi tiofauti zinazoendelea kuchukuliwa katika kuimarisha
Tamasha hilo ni hatua muhimu katika kuendeleza mila, silka, desturi na
utamaduni unatotoa fursa ya kukumbuka na kufahamu mambo yaliyokuwa yakifanywa
wazee wa asili.
Alifahamisha
kwamba ni vyema waandaaji wa Tamasha la Utamaduni la Mzanzibari wakafanya
juhudi za ziada katika kuwaalika wageni waliowasili Nchini kwa ajili ya Tamasha
la Kimataifa la Filam la Nchi za Jahazi kama njia muhimu hya kuutangaza
Utamaduni wa Zanzibar na kulipa hadhi Kimataifa Tamasha hilo.
Rais wa
Zanzibar alikelezea matarajio yake kwa waandaaji hao ia watafanya juhudi za
kutosha za kuweka matangazo katika Mahoteli, Mitandao amoja na sehemu nyengine
zinazopendwa na watalii ili wapate fursa za kuona na kuufahamu zaidi Utamaduni
wa Mzanzibari.
Alieleza
kuwa msimu wa utalii hivi sasa umeanza, hivyo wananchi wanaweza kuyatumia
Matamasha kama hayo ikiwa ni vivutio muhimu vya Utalii kama zinavyofanya Nchi
mbali mbali Duniani.
Dr. Shein
alisema dhana ya Utalii kwa wote inahimiza uhusiano na ushirikiano wa kisekta
kwa mujibu wa shughuli za kila mdau ili juhudi za kuutangaza utalii ziendelee
kufanywa na sekta zote na faida zinazopatikana ziwafikie Wananchi wote.
“ Wizara
inayosimamia Utamaduni inapaswa kushirikiana na Wizara ya uwezeshaji ili
wananchi katika makundi yote waweze kuzitumia na kunufaika na fursa zinazoweza
kupatikana kwa kuwepo kwa Tamasha la aina hii “. Alifafanua Dr. Shein.
Rais wa
Zanzibar alielezea faraja yake kutokana na uongozi wa Tamasha hilo kumualika
msanii wa muziki wa asili kutoka Comoro Bibi Shamsia Sagar kutoa burdani kwenye
tamasha hilo mualiko utakaosaidia kuimarisha uhusiano kati ya Comoro na
Zanzibar.
Aliishauri
Wizara ya Habari, Utamudni, Utalii na Michezo ifanye juhudi za kasi kwa kualika
wasanii wengine mashuhuri kutoka nchi za Mwambao wa Afrika na sehemu nyengine
Duniani ambao ushiriki wao utalipa umaarufu Tamasha hilo na hatimae kuwavutia
wageni na washiriki wengi zaidi.
Mapema Kaimu
Kamishna wa Kamisheni ya Utamaduni na Michezo Zanzibar Nd. Suleiman Mbarouk
alisema Tamasha la Utamaduni wa Mzanzibari ni muendelezo wa Agizo la Rais wa
Zanzibar la Kuitaka Kamisheni ya Utamaduni na Michezo kusimamia tamasha
lifanyike kuanzia Tarehe 19 hadi 25 Mwezi Julai ya kila mwaka.
Nd. Suleiman
alisema Tamasha hilo limesimama kwa takriban miaka mitatu sasa kutokana na
kuingiliana na Mfungol wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan ambao kwa sasa kiindi hicho
tayari kimebadilika na kutoa fursa ya kuendelea na Tamasha hilo kama kawaida.
Akimkaribisha
Mgeni rasmi kuzindua Tamasha hilo la Utamaduni wa Mzanzibar Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na
Michezo Zanzibar Mh. Said Ali Mbarouk alisema Tamasha hilo ni muhimu katika
kukirithisha kizazi kipya kuelewa Utamaduni wao wa asili.
Mh. Mbarouk
alisema Taifa lisilo na Utamaduni mara nyingi kizazi chake hutumbukia katika matatizo
makubwa ya mmong’onyoko wa maadili, upotevu wa mila na silka zao.
Waziri wa
Habari alifahamisha kwamba Tamasha la Utamaduni wa Mzanzibar lengo lake kuu ni
kuwakumbusha wazazi kurejesha malezi ya heshima kwa kikazi chao kama
walivyofanikiwa wao pamoja na mafunzo ya lugha sanifu ya Kiswahili inayokubalika
katika jamii pahali popote.
Ujumbe wa
Mwaka huu wa Tamasha la 20 la Utamaduni wa Mzanzibar ni:- “ Tudumishe Utamaduni wetu
katika hali ya amani, utulivu na Umoja “.