Balozi Mteule wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Balozi John
Michael Haule akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif
Ali Iddi alipofika Ofisini kwake kujitambulisha na kuaga rasmi baada ya
kuteuliwa kushika wadhifa huo wa Kidiplomasia. Picha na Hassan Issa–
OMPR
Balozi Mteule wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Balozi John
Michael Haule akibadilishana mawazo na Balozi Seif Ali Iddi Ofisini kwake Vuga
Mjini Zanzibar.
Picha na Hassan Issa– OMPR
Picha na Hassan Issa– OMPR
Press Release:-
Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba uendelezaji wa
Sekta ya Biashara kati ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamuhuri ya Watu
wa Kenya chini ya mwamvuli wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki utafungua njia ya
kuimarisha ustawi wa Wananchi wa pande hizo mbili.
Alisema
Kenya na Tanzania zina uhusiano wa muda mrefu wa Kihistoria licha ya changamoto
ndogo ndogo zinazojitokeza katika baadhi ya wakati ambazo uwezo wa kuzitatua
upo kwa kushirikisha mazungumzo ya pamoja baina ya Viongozi wa Nchi hizo mbili.
Balozi Seif
Ali Iddi alisema hayo wakati akizungumza na Balozi Mteule wa Jamuhuri ya
Muungano wa Tanzania Nchini Kenya Balozi John Michael Haule aliyefika Ofisini
kwake Vuga Mjini Zanzibar kujitambulisha sambamba na kuaga rasmi.
Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar alimuomba Balozi John Michael kusimamia vyema uhusiano
huo wa Kenya na Tanzania katika kuangalia fursa zilizopo kwenye Sekta ya Utalii
inayoonekana kushika kasi hivi sasa katika uchumi wa Mataifa mengi Duniani kwa.
Alisema
kutokana na kuimarika vyema kwa miundombinu kwenye Sekta ya Utalii hapa Zanzibar Ofisi ya Ubalozi
wa Tanzania Nchini Kenya inastahiki kuandaa utaratibu maalum wa kuitangaza
Zanzibar ili kuhamasisha wawekezaji wa Kenya kuanzisha Miradi yao ya kiuchumi.
Balozi Seif
alifahamisha kwamba uhamasishaji huo pia ungefanywa katika kuwashawishi
hata wageni na watalii wanaoingia Nchini
Kenya kutenga muda wao wa kuitembelea Zanzibar ili kujionea miundo mbinu na
rasilmali za utalii zinazopatikana Zanzibar.
Mapema
Balozi Mteule wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Balozi John Michael Haule alimueleza
Balozi Seif kwamba Ofisi ya Ubalozi huo itajipanga kutoa huduma muda wote wa
wiki kwa wageni na watalii watakaokuwa tayari kutaka kuitembelea Tanzania.
Balozi John alisema
maafisa wa Ubalozi huo watakutana na watembezaji utalii Nchini Kenya kwa lengo
la kuwaeleza nia ya Tanzania katika kutoa huduma za viza hata siku za mapumziko
wakati inapobidi.
Balozi
Mteule huyo wa Tanzania Nchini Kenya alimuhakikishia Balozi Seif kwamba
atasimamia kwa nguvu zake uwamuzi wa
wawekezaji wa Kenya watakaoonyesha nia ya kutaka kuwekeza Vitega uchumi vyao katika
Visiwa vya Zanzibar.
Alifahamisha
kwamba vielelezo alivyovipata wakati wa mazungumzo yake na Viongozi wa
Kamisheni ya Utalii Zanzibar na Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar {
ZIPA } vitamrahisishia kazi yake kuifanya
kwa ufanisi katika kuzitangaza fursa za Utalii zilizopo Visiwani Zanzibar.