Ofisa wa Tawi la Kampuni ya Kimataifa ya Mtandao wa Mawasiliano ya
Kisasa ya ZTE hapa Zanzibar yenye Makao Makuu yake Nchini Jamuhuri ya Watu wa China Bibi Coco Wang
akimpatia maelezo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kabla
ya kumkabidhi msaada wa Kompyuta 10 kwa ajili ya wanafunzi wa Skuli zilizomo
ndani ya Jimbo lake. Kulia ya
Bibi Coco Wang ni Ofisa mwenzake wa Kampuni hiyo Roy Chen Hafla iliyofanyika Ofisini kwa
Balozi Seif hapo Mtaa wa Vuga Mjini
Zanzibar. Picha na Hassan Issa –
OMPR
Baadhi ya Kompyuta zilizotolewa msaada na Kampuni ya Kimataifa ya
Mtandao wa Mawasiliano ya Kisasa ya ZTE Tawi la Zanzibar kwa ajili ya wanafunzi
wa Skuli za Jimbo la Balozi Seif. Picha na Hassan Issa –
OMPR
Press Release:-
Kampuni ya
Kimataifa ya Mtandao wa Mawasiliano ya Kisasa ya ZTE yenye Makao Makuu yake
Nchini Jamuhuri ya Watu wa China
imeahidi kuendelea kuunga mkono harakati za kiuchumi za Zanzibar katika kuona
wananchi wake wanafaidika na mfumo wa kisasa wa mtandao wa mawasiliano.
Ofisa wa
Tawi la Kampuni hiyo ya ZTE liliopo hapa Zanzibar Bibi Coco Wang alisema hayo
wakati wa hafla fupi ya kumkabidhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi
Seif Ali Iddi msaada wa Kompyuta Kumi
kwa ajili ya wanafunzi wa skuli zilizomo ndani ya Jimbo lake.
Akikabidhi
msaada huo wa Kompyuta wenye thamani ya zaidi ya shilingi za Kitanzania Milioni
12,000,000/- Ofisini kwa Balozi Seif Vuga Mjini Zanzibar Bibi Coco Wang alisema
Kampuni ya ZTE imejipanga kusaidia zaidi sekta ya elimu ambayo ndio msingi mkuu
wa maisha ya mwanaadamu.
Bibi Coco
alisema mfumo wa mafunzo katika vyuo na hata baadhi ya skuli za sekondari
unaotumika katika Mataifa mbali mbali yaliyoendelea unaweza kutumika hapa
Zanzibar endapo itaimarisha zaidi miundo mbinu ya mtandao wake wa mawasiliano ya Compyuta.
Akipokea
msaada huo wa Kampyuta Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
aliupongeza Uongozi wa Kampuni hiyo kwa moyo wake wa kujitolea katika kusaidia
mtandao wa mawasiliano ya kisasa hapa Zanzibar.
Balozi Seif
alisema Kampuni ya ZTE imeonyesha uungwana mkubwa kwa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar kiasi ambacho unafaa kuigwa na Makampuni mengine makubwa katika kusaidia
jamii.
Kampuni ya
Kimataifa ya Mtandao wa Mawasiliano ya Kisasa ya ZTE yenye Makao Makuu yake
Nchini Jamuhuri ya Watu wa China ndiyo
iliyofadhili mradi wa ufungaji Kamera za
kurikodi matukio mbali mbali ya kila siku { CCTV CAMERA } katika eneo la
Mji Mkongwe wa Zanzibar.
Ufadhili huo
umekuja Zanzibar kufuatia ziara ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi
Seif Ali Iddi aliyoifanya Nchini Jamuhuri ya Watu wa China mwishoni mwa mwaka uliopita.