Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi akimkabidhi msaada
wa Kompyuta Tatu na Printa yake Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Sekondari ya Kitope
Mwalimu Suleiman Juma Makame kwa ajili ya matumizi ya skuli hiyo. Picha na Hassan Issa –
OMPR
Balozi Seif Ali Iddi akimkabidhi Msaada wa Kompyuta Moja Katibu wa
Madrasat Jamiiya Islamic ya Kijiji cha Mahonda akitekeleza ahadi aliyoupa
Uongozi wa Madrasa hiyo hivi karibuni. Picha na Hassan Issa –
OMPR
Baadhi ya Wazazi na wajumbe wa Kamati ya Skuli ya Sekondari ya
Fujoni wakifuatilia mambo mbali mbali wakati wa hafla fupi ya kukabidhiwa Skuli
hiyo msaada wa Kompyuta na Prita yake kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Kitope
Balozi Seif Ali Iddi hayupo pichani. Picha na Hassan Issa –
OMPR
Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Sekondari ya Fujoni Mwalimi Mabrouk Ishaq Daima
akipokea msaada wa Kompyuta Tatu na Printa Moja kutoka kwa Mbunge wa Jimbo lao
Balozi Seif Ali Iddi. Picha na Hassan Issa –
OMPR
Press Release:-
Mbunge wa
Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba Walimu Nchini bado
wataendelea kuwa na dhamana kubwa ya kuwafinyanga wanafunzi katika kuelekea
kwenye maadili mema yatakayowavua kutumbukia katika majanga ya migogoro na
uvunjivu wa amani.
Alisema
walimu ndio wahimili wakubwa wa amani kwa kuwaongoza wanafunzi wao kushinda
mitego iliyoelekezwa kwao ambayo mara nyingi kuwashawishi kutumbukia katika
matendo maovu.
Balozi Seif
ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema hayo wakati akikabidhi
Kompyuta Tatu na Printa Moja kwa Uongozi wa Skuli ya Sekondari ya Kitope pamoja
na Skuli ya Sekondari ya Fujoni alizopewa msaada na Kampuni ya Kimataifa ya
Mtandao wa Mawasiliano ya Kisasa ya ZTE ya Nchini China kwa ajili ya Skuli
zilizomo ndani ya Jimbo lake.
Hafla hiyo
fupi iliyofanyika katika skuli hizo mbili iliambatana pia na Balozi Seif
kukabidhi Kompyuta Moja kwa Uongozi wa Madrasat Jamiiya Islamic ya Kijiji cha
Mahonda kutekeleza ahadi aliyoupa wakati akizungumza nao.
Balozi Seif alisema suala la amani ambalo linamuhusu
kila mwana Jamii halina mbadala hasa katika kipindi hichi Taifa linakoelekea
katika uchaguzi Mkuu wa Mwezi Oktoba mwaka huu.
Mbunge huyo
wa Jimbo la Kitope aliahidi kwamba ataendelea kuchangia maendeleo ya Wananchi
hasa katika sekta ya elimu kadri fursa na uwezo utakavyomruhu.
Aliwahimiza
Wanafunzi wa Skuli hizo kujitahidi kusoma kwa bidii kwa kuongeza nguvu zaidi
katika masomo ya Sayansi na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano yanayoonekana
kuwa na soko kubwa la ajira katika karne hii ya sayansi na Teknolojia.
Alizipongeza
juhudi kubwa zinazoendelea kuchukuliwa na Walimu, Wazazi na Kamati za Skuli za
Kitope na Fujoni ambazo zimesaidia kuzibadilisha Skuli hizo na kufikia katika
kiwango kinachokubalika kimasomo.
“ Kitope ni
moja ya Skuli inayofanya vyema kipindi hichi baada ya mikakati imara iliyochukuliwa na Walimu na Kamati ya
Skuli na mimi nikalazimika kuweka nguvu kufuatia matokeo ya wanafunzi wake
kuzorota katika kipindi cha nyuma “. Alisema Balozi Seif.
“ Sekondari
ya Fujoni kwa hivi sasa inatunavya uso kutokana na matokeo mazuri ya wanafunzi
wake yaliyopelekea kwa sasa kuwa na madarasa ya Kidato cha Tano na Cha Sita.
Hongereni Walimu na Wazazi “. Alifafanua Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope.
Akitoa
Shukrani kwa niaba ya Walimu Wanafunzi, Wazazi wa Skuli hizo Mwenyekiti wa
Kamati ya Skuli ya Kitope Bwana Makame Ali Mussa alisema Balozi Seif ataendelea
kupata baraka za Wananachi wa Jimbo lake kutokana na moyo wake wa Kizalendo anaouchukuwa
wa kuwasimamia Kimaendeleo.
Bwana Mussa
alisema Jimbo la Kitope limepata mafanikio makubwa ya Maendeleo ndani ya Kipindi cha miaka kumi ya
Uongozi wa Balozi Seif hasa katika Sekta ya Mama ya Elimu ambayo ndio Mkombozi
wa Jamii mahali popote pale.
Naye Mwalimu
Mkuu wa Skuli ya Sekondari ya Fujoni Mwalimu Mabrouk Ishaq Daima alisema Msaada huo wa Kompyuta umefika wakati
muwafaka kwa vile nusu ya zile zilizokuwa zikitumiwa na Wanafunzi zimechakaa
baada ya kutoa huduma kwa muda mrefu.
Mwalimu
Mabrouk alimpongeza Balozi Seif kwa
umakini wake wa kuongeza nguvu za michango na misaada katika Sekta ya Elimu inayofunza
na kulea wataalamu wa fani mbali mbali.
Katika hafla
hizo fupi zilizofanyika kwa nyakati tofauti kati ya Skuli ya Kitope na Skuli ya
Fujoni Balozi Seif alipata fursa ya kulikagua Jengo la Darasa moja lililkojengwakwa nguvu za Wananchi wenyewe
katika Skuli ya Sekondari ya Kitope.
Akikagua Darasa
na Vyoo vyake Balozi Seif Ali Iddi aliahidi kusaidia nguvu kwa kuchangia
milango, madirisha, Dari pamoja na rangi
ili kukamilisha rasmi ujenzi wa
Darasa hilo.