Monday, 12 January 2015

Mwenyekiti wa Kamati ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiambatana na baadhi ya Viongozi wa Kamati 10 zilizopewa jukumu la kusimamia maandalizi ya sherehe za Miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

 Makamanda  shupavu Wanawake wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania  { JWTZ } wakionyesha umahiri wao katika kulichapa gwaride wakijiandaa na Kilele cha maadhimisho ya kutimia miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar hapo Uwanja wa Amani Mjini Zanzibar.  Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.

 Mwenyekiti wa Kamati ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa Balozi Seif akiwa pamoja na Viongozi wa Kitaifa na Makamanda wa Vikosi vya ulinzi wakiangalia hatua za matayarisho ya mwisho ya Gwaride litakalopamba kilele cha maadhimisho ya miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar hapo Uwanja wa Amani Mjini Zanzibar. Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.



 Vijana wa Muziki wa Kikazi Kipya Zanzibar wakiimba wimbo maalum utakaoburudisha  kwenye sherehe za maadhimisho ya Kutimia miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar Januari 12 Uwanja wa Amani.  Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
























Mwenyekiti wa Kamati ya Sherehe na maadhimisho ya Kitaifa Balozi Seif akizungumza na wajumbe wa Kamati hiyo walipokuwa wakitathmini matayarisho ya kwisho ya kilele cha sherehe za Mapinduzi zinazofikia ukingoni Januari 12 2015 uwanjani Aamani.  Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.

   Press Release:-

Matayarisho ya mwisho kwa ajili ya kilele cha maadhimisho ya kusherehekea kutimia miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 yamefikia hatua ya mafanikio makubwa  katika kukamilika kwake.

Maadhimisho hayo yaliyoanza Tarehe  Pili Januari 2015 kwa usafi wa mazingira, uzinduzi pamoja na  uwekaji wa mawe ya msingi ya miradi mbali mbali ya Taasisi za Umma na zile binafsi yakiwemo mashindano ya michezo na burdani tofauti yanafikia kilele chake Januari 12 siku ambayo wakwezi na Wakulima walijikomboa kutoka katika makucha ya wakoloni.

Vikosi vya ulinzi na usalama vya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na vile vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar vilikamilisha matayarisho ya mwisho ya Gwaride  rasmi hapo Uwanja wa Amani Mjini Zanzibar linalotarajiwa kupamba maadhimisho hayo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiambatana na baadhi ya Viongozi wa Kamati 10 zilizopewa jukumu la kusimamia maandalizi ya sherehe hizo walishuhudia gwaride la vikosi hivyo vinavyoonekana kuwiva katika kiwango kilichokusudiwa.

Vikosi vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania { JWTZ }, Polisi, Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo { KMKM }, Mafunzo,Jeshi la Kujenga Uchimi { JKU }, Kikosi cha Zimamoto na Uokozi na Valantia vilionekana kuupamba uwanja wa amani kwenye matayarisho hayo vikiwa tayari kwa ajili ya Kilele cha maadhimisho hayo.

Gwaride hilo lililoongozwa na Luteni Kanali Moh’d Khamis Adam liliambatanisha pia na matayarisho mengine ya mwisho ya ngoma za utaduni pamoja na muziki wa Kizazi kipya watakaopata fursa ya kutoa burdani kwenye kilele cha maadhimisho hayo ya kutimia miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa katika Ukumbi wa Watu mashuhuri { VIP } uliopo Uwanja wa Amani Mjini Zanzibar mara baada ya kuangalia  matayarisho hayo Mwenyekiti wa Kamati hiyo Balozi Seif aliyapongeza majeshi yote kwa hatua yaliyochukuwa ya kushiriki vyema kwenye maandalizi ya sherehe hizo.

Balozi Seif alisema juhudi zilizoonyeshwa na wapiganaji hao katika kulichapa gwaride  zimeonyesha wazi umahiri wao katika kutekeleza vyema majukumu wanayopangia na Taifa.

“ Nimeridhika na maandlizi yote yaliyochukuliwa  na  Kamati  zote zilizoshiriki kikamilifu katika matukio mbali mbali tokea sherehe zetu zilipoanza Mapema mwezi huu. Mambo mazuri sana licha ya kasoro ndogo ndogo zilizojitokeza ambazo uwezo wa kuzikamilisha upo “. Alisema Balozi Seif.

Mapema Katibu wa Kamati ya Sherehe na Maadshimisho ya Kitaifa  Dr. Khalid Salum Moh’d alisema Kamati imeandaa utaratibu kwa Wananchi watakaokosa kuingia ndani ya Uwanja  wa Amani kuziona sherehe hizo kupitia TV maalum zitakazowekwa upande wa jukwa la mashariki  { Maarufu jukwaa la Urusi }.

Dr. Khalid alisema TV hizo zimeandaliwa kwa lengo la kupunguza msongamano mkubwa unaoweza kutokea endapo wananchi watajitokeza kwa wingi kuhudhuria sherehe hizo za Mapinduzi ya Zanzibar kutimia miaka 51.

Wageni wa Kimataifa wapatao 120  miongoni mwao  wakiwemo Mabalozi  80 wa Nchi za Nje waliopo Tanzania wamethibitisha kuhudhuria sherehe hizo, waandishi wa Habari 160 wataripoti  matukio ya sherehe hizo wakati vituo vya TV Vinne na Redio 6 vinatarajiwa kutangaza moja kwa moja sherehe hiyo.