Tuesday, 6 January 2015

Balozi Seif afungua jengo la skuli la Faraja


 Jengo la Skuli ya Secondary ya  Faraja lililofunguliwa na Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idi Kwamtipura Mjini Zanzibar ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra za Maadhimisho ya miaka 51ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idi kushoto akisalimiana na Muwakilishi wa Jimbo la Kwamtipura Hamza Hassan katika ufunguzi wa Skuli ya Secondary ya Faraja Kwamtipura Mjini Zanzibar ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra za Maadhimisho ya miaka 51ya Mapinduzi ya Zanzibar.
 Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idi akikunjuwa Kitambaa ikiwa ni ishara ya Ufunguzi wa Skuli ya Secondary ya Faraja Kwamtipura Mjini Zanzibar ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra za Maadhimisho ya miaka 51ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Wanafunzi wa Madrasa ya Kamaria wakileta burudani ya Kasida katika ufunguzi wa Skuli ya Secondary ya Faraja Kwamtipura Mjini Zanzibar ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra za Maadhimisho ya miaka 51ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Ali Juma Shamhuna akitoa maelezo kuhusiana na Skuli ya Secondary ya Faraja iliofunguliwa na  Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idi Kwamtipura Mjini Zanzibar ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra za Maadhimisho ya miaka 51ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Na Othman Khamis Ame, OMPR
 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba hakuna hakiba, utajiri au urithi wenye thamani kubwa ambao mzazi anaweza kumuachia mtoto wake isipokuwa elimu.
 
Alisema ukweli ni kwamba mtoto akipata elimu tayari anakuwa na rasilmali ya maisha yake yote ambayo ndio inayompa utajiri wa kudumu usioweza kuibiwa au kuharibiwa.
 
Balozi Seif alisema hayo wakati akiifungua rasmi Skuli ya Sekondari ya Faraja iliyopo katika mtaa wa Kwamtipura Mjini Zanzibar ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra za kusherehekea maadhimisho ya kutimia miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.
 
Alisema wazazi wana wajibu wa kushirikiana na walimu na kamati za skuli katika kuwahimiza watoto kwenda kutafuta elimu ili kuungana na Serikali katika dhana nzima ya kuwajengea mazingira mazuri ya miundo mbinu ya kielimu watoto wote hapa nchini.
 
Balozi Seif alieleza kwamba Serikali itaendelea kuchukuwa hatua mbali mbali katika kuhakikisha kuwa ujenzi wa skuli na huduma nyengine muhimu za Kijamii zinapelekwa katika na maeneo wanayoishi wananchi waliowengi  wengi ili kuwapunguzia usumbufu wa kufuata huduma hizo masafa marefu.
 
Alisema Taifa limeamua kuwekeza katika sekta ya elimu ikielewa kwamba  nchi itapiga hatua kubwa za maendeleo iwapo wananchi wake wataelimika. Hivyo aliwaasa wanafunzi  kutumia fursa walizozipata ili baadaye waweze kulitumikia Taifa lao katika nafasi tofauti za kitaalamu na hata za uongozi.

“Kujengwa kwa Skuli hii hapa kumelengwa kuwaondoshea usumbufu wanafunzi wa kufuata skuli maeneo mengine ya mbali “. Alisema Balozi Seif.
 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba jamii imekuwa ikishuhudia juhudi kubwa za Serikali ilizochukuwa katika kujenga Skuli za Sekondari 19 katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba ikiwa inatekeleza Ilani ya CCM  ya mwaka 2010.
 
Alisema Serikali ya Awamu ya Saba inayoongozwa na Mheshimiwa Dr. Ali Mohammed Shein tokea kuingia madarakani miwaka mine iliyopita imeamua kuongeza uwekezaji katika upanuzi wa elimu kuanzia ngazi ya msingi hadi elimu ya sekondari na vyuo Vikuu.
 
Balozi Seif alisema kwamba Serikali imeamuwa kufanya hivyo ikilenga kutekeleza kwa vitendo maamuzi yaliyofikiwa  tokea mwaka 1964 chini ya Rais wa Kwanza wa ZXanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume ya kutoa elimu bila ya malipo kwa watoto wote bila ya ubaguzi.
 
Alifahamisha kwamba lipo ongezeko la wanafunzi kutokana na juhudi hizo ambapo takwimu zikionyesha kwamba mwaka 2010 kulikuwa na wanafunzi 346,377 katika ngazi zote za elimu hapa Zanzibar ikilinganishwa na mwaka 2014 uliobeba jumla ya wanafunzi Laki 388,719.
 
Alisema takwimu hizi zinaonyesha kuwepo kwa ongezeko la wanafunzi katika kipindi  hicho cha miaka minne ikiwa ni kielelezo cha wazi cha nia ya Serikali katika kuimarisha sekta ya elimu na kuweza kupambana na umaskini.
 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliwanasihi wananchi wanaoishi pembezoni mwa maeneo ya skuli  za Umma pamoja na wanafunzi wanaoitumia skuli hizo hawana budi kuzitunza vyema ili ziendelee kutoa huduma kwa muda mrefu zaidi.
 
Alisema Serikali imetumia fedha nyingi katika ujenzi wa miundombinu ya ujenzi wa skuli mbali mbali, hivyo Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali inapaswa kuandaa utaratibu maalum wa utunzaji wa majengo ya skuli ili kuhakikisha yanaendelea kuwa katika hali nzuri kila wakati.
 
Akisoma Risala ya Walimu na wanafunzi wa Skuli ya Sekondari ya Faraja Mwalimu Takadiri  Omar Bakar alisema skuli hiyo iliyojengwa kwa Mkopo wa Benki ya Dunia ilianza na wanafunzi 838 mwaka 2013.
 
Mwalimu Takadir alisema hivi sasa skuli hiyo yenye walimu 71 imeongeza idadi ya wanafunzi wanaofikia 1674 na kuifanya kuwa na upungufu wa walimu wa masomo ya Sayansi.
 
Alisema ujenzi wa skuli hiyo umesaidia kupunguza ongezeko kubwa la wanafunzi katika skuli za Rahaleo na Muembe Ladu pamoja na kuwaondoshea usumbufu wa masafa marefu wanafunzi wa maeneo ya Ng’ambo.
 
Hata hivyo Mwalimu Takadiri alielezea changamoto zinazoikabili skuli ya Faraja akazitaja baadhi yake kuwa ni pamoja na ukosefu wa huduma za maji safi, uhaba wa compyuta pamoja na walimu wa sayansi kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi pamoja na ukosefu wa uzio unaoizunguuka skuli hiyo.
 
Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Bibi Khadija Saleh  alisema Skuli ya Faraja iliyojengwa Kwa Mkopo wa Benki ya Dunia wa gharama ya Shilingi Bilioni 1.8 ina mazingira rafiki ya wanafunzi wote wakiwemo watoto wale wenye mahitaji Maalum.
 
Bibi Khadija alisema katika kuijengea mazingira mazuri ya utoaji wa elimu inayokwenda na wakati Skuli hiyo ya Faraja Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar  itajitahidi kuzichukulia hatua inayofaa changamoto zote  zinazoikabili skuli hiyo ambazo zimo ndani ya uwezo wa Wizara hiyo.