Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akilifungua
Tamasha la Pili la Biashara Zanzibar linalofanyika katika uwanja wa michezo wa
Maisara Mjini Zanzibar. Kulia ya
Balozi Seif ni Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Mh. Nasso Ahmed Mazrui na
kushoto yake ni Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Baisra
Tanzania { Tantrade } Bibi Jackline na Naibu Waziri wa Biashara Zanzibar Mh.
Thuwaiba Kisasi. Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
Kikundi cha Sarakasi cha Young
Brother Acrobatic kutoka Kijiji cha Muyuni kikifanya vitu vyake wakati wa hafla
ya ufunguzi wa Tamasha la Biashara Zanzibar Hapo Maisara Suleiman. Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.Ofisa Kutoka Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bibi Robi Bwire akimpatia maelezo Balozi Seif wakati akikagua mabanda ya maonyesho kwenye Tamasha la Biashara. Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
Balozi Seif akifurahia bidhaa zinazouzwa na Kampuni ya Pakiza General Traders kwe nye Tamasha la Pili la Biashara Zanzibar. Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Baisra Tanzania { Tantrade } Bibi Jackline na Waziri wa Biashara Zannzibar Mh. Mazrui wakifurahia bidhaa za Miti shamba kwenye banda la Maonyesho la Uganda. Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
Press Release:-
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi ametoa wito kwa Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko Zanzibar kuanzisha eneo maalum kwa maonyesho ya
biashara kwa lengo la kutanua zaidi uhusiano wa kibiashara kati ya Zanzibar na
Mataifa mengine Duniani.
Alisema maonyesho ya Kibiashara siyo tu yanavutia na
kushawishi wawekezaji lakini pia huongeza ushirikiano karibu baina ya wafanyabiashara
wenyewe kwa wenyewe .
Balozi Seif alitoa wito huo wakati akilifungua
tamasha la Pili la Biashara la mwaka 2015 la maadhimisho ya kutimia miaka 51 ya
Mapinduzi ya Zanzibar linalofanyika katika uwanja wa mishezo wa Maisara Mjini
Zanzibar.
Alisema lengo kuu la Tamasha la biashara Zanzibar ni kushajiisha ukuaji wa biashara kwa azma ya
kuirejeshea Zanzibar hadhi yake ya kuwa kituo cha biashara katika mwambao wa
Afrika Mashariki kwa karne kadhaa zilizopita.
Balozi Seif alifahamisha kwamba uwepo wa matamasha
kama haya Zanzibar hutoa fursa kwa wageni kujipangia muda wa kutembelea
Zanzibar kwa mapumziko pamoja na kujipatia mahitaji yao ya bidhaa tofauti
zinazozalishwa ndani na hata kwa zile Taasisi za nje zinazoshiriki maonyesho
hayo.
Alisema wafanyabiashara pamoja na wajasiri amali wanapaswa kuitumia
vyema fursa hiyo adhimu ya tamasha la biashara ili wakuze biashara zao kwa vile
ni moja kati ya sekta muhimu ya kukuza uchumi na kutoa ajira kwa wananchi walio
wengi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Serikali
itaendelea kushirikiana na wafanyabiashara wa pande zote mbili za Jamuhuri ya
Muungano wa Tanzania na Afrika Mashariki katika kuhakikisha sekta ya biashara
inazidi kukua sambamba na matamasha ya
biashara ili kuongeza idadi ya wageni.
Balozi Seif
alisisitiza umuhimu wa matamasha kama haya ya biashara kujumuishwa pia
maonyesho ya utamaduni wa Mzanzibari kama kazi za sanaa ya mkononi, vyakula vya
mwambao wa pwani ya Afrika Mashariki na Muziki ambao unaonekana kutoweka katika
Historia kutokana na mabadiliko ya utandawazi.
Aliwaomba wafanyabiashara kuziepuka bidhaa zilizo
chini ya kiwango kwani kufanya hivyo kutamfanya mnunuzi wa bidhaa zao kupoteza
fedha bure pamoja na kuharibiwa mipango yake.
Balozi Seif alieleza kwamba Serikali imeanzisha
Taasisi inayosimamia viwango kwa lengo la kukuza ubora wa bidhaa zinazozalishwa
pamoja na zile zinazoagiziwa nje ya nchi masuala ambayo yanakwenda sambamba na
mikakati ya kuwasaidia wjasiri amali wa Zanzibar katika kufikia viwango
vinavyokubalika katika masoko ya Kimataifa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameipongeza
Wizara ya Biashara Zanzibar kwa kushirikiana na mamlaka ya Maendeleo ya
Biashara Tanzania { Tantrade } pamoja na Jumuiya ya Wafanyabiashara Zanzibar
kwa wazo lao la pamoja la kuanzisha na kuendeleza Tamasha la Biashara hapa Zanzibar.
“ Na hili ni tamasha la Pili huku tukisherehekea
miaka 51 ya Mapinduzi ya Januari mwaka 1964 lengo likiwa kushajiisha ukuaji wa
biashara kwa azma ya kuirejeshea Zanzibar hadhi yake ya kuwa kituio cha
Biashara Mwambao wa Afrika Mashariki “. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliipongeza
Mamlaka ya Maendeleo ya Baisra Tanzania { Tanzania Trade Development Authority
– Trade } kwa uamuzi wake wa kuisaidia
Wizara ya Biashara Viwanda na Masoko Zanzibar katika taaluma ya Maonyesho na matamasha
ya Baishara.
Balozi Seif aliitaka Mamlaka hiyo kuendelea kuiunga
mkono Zanzibar katika sekta hiyo ili ifikie hatua ya kujiendesha yenyewe katika
sekta hiyo muhimu ya Uchumi wa Taifa.
Aliwashukuru washiriki wa wa tamasha hili la
Biashara Zanzibar kutoka ndani na nje ya Nchi, Taasisi za Umma na zile Binafsi,
Mapampuni kwa kushiriki kwenye tamasha
la mwaka huu na kuwaomba washiriki kwenye matamasha yanayokuwa yanaandaliwa
hapa Zanzibar.
Mapema Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko
Zanzibar Mh. Nassor Ahmed Mazrui alisema ukuaji wa sekta ya B iashara hapa
Nchini umeongeza mapato ya nchi sambamba na huduma za fedha.
Waziri Mazrui alisema Tamasha la Biashara la Mwaka
huu limeshirikisha zaidi ya Makampuni 160 katika ya 200 yaliyoomba kushiriki
katika Tamasha hili kutoka Tanzania Bara
na wenyeji Zanzibar yakiwemo Makapumi
mawili ya Kigeni.
Alifahamisha kwamba mbali ya bidhaa mbali mbali
zitakazouzwa na kuonyeshwa kwenye Tamasha hilo la bishara lakini pia huduma za
Michezo ya Watoto itakuwepo ili kuwapa fursa watoto watakaotembelea Tamasha
hilo kupata burdani.
Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko aliwapongeza
washiriki wa Tamasha la kwanza la mwaka
J ana lililofanikiwa vyema kutokana na kukusanya mapato zaidi hya shilingi
Milioni 220,630,150/- kutokana na bishara za papo kwa papo.
Alisema Tamasha la mwaka pia lilipokea maombi ya
wateja kutoka makampuni na watu binafsi kwa ajili ya kupata huduma zenye
gharama ya zaidi ya shilingi Milioni 90,000,00o/-.
Tamasha la Pili la Biashara la mwaka 2015 la
maadhimisho ya kutimia miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar limeanza Tarehe 7
Januari mwaka huu wa 2015 na kuendelea hadi Tarahe 13 Mwezi huu.