Mkurugenzi wa Idara ya Mafa Zanzibar Ali Juma Hamadi akionyesha dole kufurahia mlo akiwa pamoja na Mkurugenzi Uratibu wa Shughuli za Serikali Nd. Issa I. Mahmoud kwenye tafrija ya mkesha wa mwaka Mpya iliyoandaliwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Nyumbani kwake Mazizini nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Sei Ali Iddi na Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi wakiserebuka wakatiu wimbo maalum wa Baba na Mwana wakiimba na chucheza ulipopigwa kwenye tafrija ya mkesha wa mwaka mpya.Watendaji wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar pamoja na waalikwa mbali mbali wakisakata rumba wakati wa mkesha wa mwaka mpya hapo mazizini knyumbani kwa Balozi Seif.
watendaji wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar pamoja na waalikwa mbali mbali wakisakata rumba wakati wa mkesha wa mwaka mpya hapo mazizini knyumbani kwa Balozi Seif.
Balozi Seif akiagana na Mwakilishi wa Jimbo la Kwamtipura Mh. Hamza Hassan Juma mara baada ya kukamilika kwa tafrija ya mkesha wa mwaka mpya wa 2015 hapo nyumbani kwake Mazizini. Nyuma ya Mhe. Hamza ni Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Dr. Khalid Salum Mohamed.
press release
Balozi Seif: Mashirikiano katika kutekeleza majukumu huleta ufanisi
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba maombi aliyoyatoa ya kuwataka wafanyakazi wa Ofisi yake kufanya kazi kwa ushirikiano na upendo ndani ya kipindi cha miaka minne iliyopita ndio yaliyoleta ufanisi mkubwa katika utekelezaji wa majukumu ya Ofisi hiyo.
Balozi Seif alimpongeza Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud Mohamed kwa kuwa kiungo kikubwa cha ufanisi kati ya wafanyakazi na Viongozi pamoja na Kumshukuru Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo Dr. Khalid Salum Moh’d kwa kusimamia vyema udhibiti mzuri wa matumizi ya fedha za Wizara hiyo.
Akizungumza katika hafla maalum aliyowaandalia watendaji wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar iliyojumuisha wawakilishi wa taasisi zote zilizo chini ya Ofisi hiyo hapo nyumbani kwake Mazizini nje kidogo ya Mji wa Zanzibar Balozi Seif alisema kwamba mwaka 2014 umeleta faraja iliyoleta mafanikio makubwa.
Alisema usimamizi makini ulioonyeshwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo hasa katika masuala ya matumizi ya Fedha umeiwezesha Wizara hiyo kujilinda na kwiri ambazo zingehitaji maelezo ya kina jambo ambalo halipendezi kwa watendaji wenye akili na maarifa wakati wanapotekeleza majukumu waliyopangiwa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwataka watendaji hao kuendelea kutekeleza kazi zao kwa bidii na maarifa wakikumbuka kwamba mwaka 2015 ni muhimu kwa vile umebeba mambo mengi muhimu kwa Kitaifa.
Alisema Wananchi wanatarajiwa kushiriki katika upigaji kura ya maoni ya Katiba Mpya ya Tanzania mwishoni mwa mwezi wa Aprili ikifuatiwa na uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba mambo ambayo watendaji wa Taasisi za Umma watalazimika kuwajibika ipasavyo kwenye majukumu watayopangiwa ili kufanikisha mambo yote mawili.
Balozi Seif aliomba radhi kwa mtendaji au Mtu ye yote pamoja na jamii yote kwa ujumla hapa nchini kama alimkosea wakati akitekeleza jukumu lake akiwa kama mtendaji Mkuu wa Serikali na ichukuliwe kuwa hizo ni kasoro zinazoweza kumpata Binaadamu ye yote na yeye alithibitisha kwamba amewasamehe wale wote waliomkosea iwe kwa makusudi au bahati mbaya.
Aliiombea dua jamii na wananchi wote kuuanza mwaka mpya wa 2015 kwa mshikamano, ushirikiano na uwajibikaji ili kupata mafanikio yatakayoleta faida kwao na Taifa kwa jumla.
Mapema Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Dr. Khalid Salum Mohamed alisema watendaji wa Ofisi hiyo wamefanya kazi kubwa ndani ya mwaka 2014 na kuiwezesha Wizara kufikia zaidi ya asilimia 90% ya utekelezaji wa majukumu yake licha ya baadhi ya changamoto zilizojitokeza.
Dr. Khalid alisema watendaji hao wanaingia mwaka 2015 na matumaini makubwa yakibeba nguvu za kuendeleza kasi ile ile ya uwajibikaji utakaoongeza tija mara dufu na kuweka rikodi nzuri.
“ Tunaingia mwaka mpya wa 2015 sote tukiwa wamoja, tunaopendana , kushikamana na kushirikiana tukiwa na lengo moja la kufanikisha jukumu tulilopangiwa kulisimamia “. Alisema Dr. Khalid.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif amekuwa na kawaida ya kuandaa Tafrija kwa kuwaalika wafanyakazi wa Ofisi yake pamoja na Familia zao tokea ashike wadhifa huo ambapo hujumuika nao pamoja katika kusherehekea mkesha wa mwaka mpya unaoambatana na burdani mbali mbali.