Friday, 22 August 2014

Balozi Seif akutana na Uongozi wa Wanafunzi wa Wanaosoma Korea.


Uongozi wa Jumuiya Watanzania wanaosoma Nchini Korea ya Kusini { KOIKA } ukiongozwa na Rais wake Nd. Steven Katemba ukijitambulisha rasmi kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Nyumbani kwake Mazizini Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar mara baada ya kucgauliwa rasmi mwezi Mei Mwaka huu.Nyuma ya Ndugu Steven ni Makamu wa Rais wa Jumuiya hiyo kwa upande wa Zanzibar NduguBukheit Juma.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kati kati akiwa katika picha ya pamoja na uongozi wa Jumuiya ya Watanzania wanaosoma Nchini Korea ya Kusini { KOIKA } uliofika nyumbani kwake kujitambulisha rasmi baada ya kushika wadhifa huo.Kushoito ya Balozi Seif ni Rais wa Jumuiya hiyo ya KOIKA Nd. Steven Katemba na Makamu wa Rais wake Nd. Bukheit Juma.
Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.


Jumuiya ya Wanafunzi wa Kitanzania wanaosoma Nchini Korea ya Kusini { KOIKA } imejipanga kuwa kiunganishi kizuri cha wanataaluma wa Korea ya Kusini na wale wa Kitanzania kwa lengo la kudumisha uhusiano uliopo kati ya nchi mbili hizo.

Rais wa KOIKA  aliyekuwa kinara wa Ujumbe wa Viongozi Wanne wa Jumuiya  hiyo Ndugu Steven Katemba alieleza hayo wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Nyumbani kwake Mazizini Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Nd. Steven na ujumbe wake ambao wapo Nchini Tanzania kujitambulisha rasmi baada ya kuchaguliwa kwao kushika dhamana hiyo ya Uongozi wa Jumuiya mnamo Mwezi Mei mwaka huu alisema zipo fursa nyingi za kimasomo na uhusiano Nchini Korea Kusini ambazo Vijana wa Kitanzania wanaweza kuzichangamkia.

Alieleza kwamba Korea ya Kusini iliyopo Bara la Asia ni miongoni mwa Nchi chache za Bara hilo ziliyopiga hatua kubwa za maendeleo na kiuchumi kiasi kwamba Tanzania inaweza kujifunza kupitia maendeleo hayo.

Alisema Jumuiya yao mbali ya kuanzishwa kwa lengo la kusaidiana kupambana na matatizo yanayowakabili katika mafunzo yao lakini pia imejipanga kushiriki katika shughuli za Kijamii hapa Tanzania.

Rais huyo wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Kitanzania wanaosoma Nchini Korea ya Kusini alifahamisha kwamba wanachama wa jumuiya hiyo tayari wameshajipanga kufanya kazi za Kijamii hivi karfibuni katika Nyumba za Wazee ziliopo Mtaa wa Sebleni Mjini Zanzibar.


Alisema kazi hizo zitakuwa ni pamoja na kufanya usafi utakaoambatana na kubadilishana mawazo na wazee hao  ambao tayari wameshatumia muda wao mwingi wa maisha katika Kujenga Taifa la Tanzania.
Akitoa Shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliipongeza Jumuiya hiyo ya Wanafunzi wa Kitanzania wanaosoma Nchini Korea Kusini kwa uamuzi wao wa kuunda Jumuiya itakayowasaidia kukabiliana na changa moto zozote zitakazojitokeza mbele yao.

Balozi Seif alisema kitendo cha vijana hao kuamua kujishirikisha katika shughuli za Kijamii kinaweza kuamsha ari na chachu kwa vijana wengine nchini na hata wale wanaosoma mataifa wengine kuunda vikundi kama hivyo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliueleza Uongozi wa Jumuiya hiyo ya Koika kwamba uhusiano uliopo kati ya Korea ya Kusini na Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ni mkubwa na Vijana hao wana haki na wajibu wa kusaidia kuudumisha uhusiano huo muhimu kwa ustawi wa pande zote mbili.

Zaidi ya Wanafunzi mia Tisa na Kumi wa Kitanzania wanasoma Nchini Korea ya Kusini ambao kati ya hao Mia Moja na Mbili wanatoka Visiwani Zanzibar.