Thursday, 14 August 2014

Taasisi ya Milele ya Zanzibar Foundation Yataliana saini ya Makubaliano ya Ujenzi wa Vituo vya Afya Pemba na Unguja.


Mjumbe wa bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Milele Zanzibar Foundation Bi. Sharifa Saif akieleza malengo ya tasisi yao kwa wandishi wa habari wa vyombo mbalimbali juu ya kusaidia jamii ya wazanzibari. 
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Mohamed Saleh Jidawi na Bi Sharifa Saif ambaye ni Mjumbe wa bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Milele  wakitia Saini Mkataba wa Makubaliano wenye lengo la kujenga na kumalizia Vituo vya Afya 27 katika Visiwa vya Unguja na Pemba. 
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Mohamed Saleh Jidawi na Bi. Sharifa Saif wakikabidhia hati za makubalino ya ujenzi wa Cliniki 27 Unguja na Pemba, hafla hiyo imafanyika katika ukumbi wa mikutano wa Wizara ya Afya Zanzibar.(Picha na Jamila Abdalla-maelezo Zanzibar)

Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar    
                      
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetiliana Saini Mkataba wa Makubaliano na Taasisi ya Milele Zanzibar kwa lengo la kujenga na kumalizia Vituo vya Afya 27 katika Visiwa vya Unguja na Pemba.

   Taasisi hiyo inayoundwa na Wazanzibari wanaoishi nje ya Nchi(WanaDiaspora) inatarajia kutumia zaidi ya Bilioni 4 katika kufanikisha ujenzi wa Vituo hivyo.

Akizungumza katika hafla hiyo Katibu wa Wizara ya Afya Mohamed Saleh Jidawi amesema Vituo 16 vitajengwa Unguja ambapo kwa Pemba watajenga Vituo 11.

   Amefahamisha kuwa Mradi huo utawezesha kujengwa Vituo vipya vya Afya katika baadhi ya Maeneo ambapo kwa maeneo mengine vitamaliziwa vituo ambavyo havijakamilika ujenzi wake.

Aidha Katibu Jidawi amewashukuru Wazalendo hao kwa kuthamini Afya kwa jamii yao na kuwaahidi mashirikiano yote yatakayohitajika.

Kwa upande wake Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Milele Sharifa Saif amesema Taasisi yao si ya kiserikali wala haifungamani na Itikadi yoyote ya kisiasa wala Kidini bali inajikita zaidi katika misaada ya kiutu.Amesema msukumo wao mkubwa umetokana na kujua kwamba Zanzibar ni nyumbani kwao hivyo hawana budi kusaidia pale ambapo wanauwezo wa kufanya hivyo.

 Amebainisha kuwa upande wa Kisiwa cha Unguja watajikita zaidi kusaidia katika Maeneo ya Shamba lakini kwa upande wa Pemba watajikita katika maeneo yote.

    Katika utiaji huo wa Saini ya Makubaliano Katibu Mkuu wa Afya Mohamed Saleh Jidawi aliiwakilisha Serikali ambapo kwa Upande wa Taasisi ya Milele iliwakilishwa na Bi Sharifa Saif.
    Taaisisi ya Milele ilisajiliwa rasmi Zanzibar Februari 2014 ambapo malengo yake ni kuleta maendeleo katika sehemu za Afya, Elimu, Kilimo na kuongeza kipato na kupunguza umasikini Vijijini.