Sunday, 10 August 2014

Mama Asha: Vijana waungwe mkono kwenye harakati zao za kijamii


Mke wa Mbunge wa Jimbo la Kitope Mama Asha Suleiman Iddi akimkabidhi Vifaa vya Michezo Nahodha wa Timu ya Soka ya Jimbo la Donge Ussi Ali-Haji Bakar Juma ambayo imepiga kambi ikijiandaa na mashindano ya Kombe la Majimbo Taifa yaliyoanza rasmi Tarehe 6 mwezi huu.

Mwenyekiti wa Kambi ya mazoezi ya Timu za Soka za Majimbo la Donge na Kitope Mwinyi Mahfoudh Muhsin akipokea vifaa na vyakula kutoka kwa Mama Asha Suleiman Iddi kwa ajili ya wachezaji wa Timu za Majimbo ya Donge na Kitope waliopiga kambi kwenye Ofisi ya CCM Jimbo la Kitope hapo Kinduni.
Baadhi ya wachezaji wa Timu za Soka za Majimbo ya Kitope na Donge waliopiga kambi kwa ajili ya mashindano ya Kombe la Majimbo Taifa wakimsikiliza Mke wa Mbunge wa Jimbo la Kitope Mama Asha Suleiman Iddi hayupo pichani wkati wa uzinduzi wa kambi hiyo hapo Ofisi ys CCM Jimbo la Kitope iliyopo Kinduni.

Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ

Na Othman Khamis Ame, OMPR
Viongozi wa ngazi mbali mbali Nchini wanapaswa muda wao mwingi kuutumia katika kuendelea kuwaunga mkono Vijana kwenye harakati zao za kijamii ili wapate muongozo sahihi utakaowapa njia ya kufanikiwa vyema katika malengo wanayojipangia ya hapo baadae.
Mke wa Mbunge wa Jimbo la Kitope Mama Asha Suleiman Iddi alitoa kauli hiyo wakati akizindua rasmi Kambi ya Timu za Soka za Majimbo ya Donge na Kitope zinazojiandaa kwa mashindano ya Kombe la Majimbo Taifa yaliyoanza rasmi Tarehe 6 Mwezi huu.
Hafla hiyo fupi iliyofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya CCM Jimbo la Kitope iliyopo Kinduni Wilaya ya Kaskazini “B “ ilishuhudiwa pia Mama Asha akikabidhi Vifaa vya  michezo kama Jezi Seti mbili kwa kila Timu, Mipira,Track Suits kwa ajili ya Viongozi wao pamoja na vyakula mbali mbali vyote vikigharimu zaidi ya shilingi Milioni Tano Nukta Tatu { 5,300,000/- }.


Mama Asha alisema ukaribu wa wazazi kwa watoto na Vijana  wao ndio jambo la msingi litakalotoa fursa nzuri kwa Watoto hao kuwa na maadili na utamaduni sahihi unaokubalika katika Jamii.
Mke huyo wa Mbunge wa Jimbo la Kitope alisema wachezaji hao wa  Timu zote mbili za Majimbo ya  Kitope na Donge wanapaswa kucheza kwa bidii na nidhamu ili kuleta ushindi ndani ya Wilaya yao ya Kaskazini “ B “.
Mama Asha aliwataka wachezaji hao wajiepushe mbali na vitendo vya udanganyifu vinavyotumiwa na baadhi ya watu hasa wanasiasa vya kuwashawishi vijana kujiingiza katika vitendo viovu.
Alisema Watu na Viongozi hao matapeli hutumia muda wao mwingi kuwavurugia vijana mwenendo wao na baadae huwasababishia hata kukosa muda wa kuendeleza michezo yao ambayo kwa hivi sasa imeonyesha mwanga wa kutoa ajira.
Katika kuwahamasisha wachezao hao wa Timu zote mbili za Majimbo ya Donge na Kitope Mke huyo wa Mbunge wa Jimbo la Kitope alisema kwamba endapo wachezaji hao wataleta ushindi ndani ya Wilaya yao ya Kaskazini “ B “ amehidi kutoa shilingi Milioni Moja na Nusu kwa Timu itakayopeleka kikombe cha ushindi wa mashindano hayo ya Kombe la Majimbo Taifa na shilingi Laki mbili na Nusu kwa Kila Mchezaji.
Akitos shukrani kwa niaba ya wachezaji wa timu zote Mbili za Majimbo hayo ya Donge na Kitope mwakilishi wa wachezaji hao Omar Ali Khamis alimuhakikishia Mama Asha kwamba vifaa vyote hivyo walivyopatiwa watavitumia kama inavyotarajiwa.
Omar Ali Khamis alisema wachezaji hao wana kila sababu ya kufanya vyema katika mashindano hayo ya kombe la Majimbo Taifa na kuahidi kwamba Timu hizo zitaingia mbili bora na kuweka rikodi nzuri ya Wilaya na Majimbo hayo.
Mapema Mbunge wa Jimbo la Donge ambae pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM Taifa Mh. Sadifa Juma Khamis alisema bahati iliyoje kwa Wananchi wa Jimbo la Kitope kupata Mbunge anayejali shida na changamoto zinazowakabili Wananchi wake hasa wanamichezo wa Jimbo hilo.
Mh. Sadifa ambae aliahidi kuwapatia Seti ya TV na King’amuzi chake Wanakambi hao ili kujua kinachojiri Duniani hasa katika ulimwengu wa Soka aliwataka Wananchi hao kuendelea kumpa fursa ya kuongoza Jimbo lao la Kitope Mbunge wao Balozi Seif Ali Iddi katika kipindi kijacho ili akamilishe malengo aliyojiwekea.
Mbunge huyo wa Jimbo la Donge aliwaasa Wananchi na Viongozi wa Majimbo hayo pamoja  na Wilaya nzima kujenga utamaduni wa kuwaandaa viongozi wa baadae ili kuwa na uhakika wa safu ya Uongozi ndani ya Majimbo na Wilaya hiyo.