Monday, 11 August 2014

Zanzibar ingependa kuona wawekezaji wengi zaidi kutoka Ujerumani wanawekeza Zanzibar


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akisalimiana na Balozi Mpya wa Ujerumani Nchini Tanzania Mhe,Egon Kochanke,alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo kujitambulisha.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akifuatana na Balozi Mpya wa Ujerumani Nchini Tanzania Mhe,Egon Kochanke,baada ya mazungumzo yao alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo kujitambulisha


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akibadilishana mawazo na Balozi Mpya wa Ujerumani Nchini Tanzania Mhe,Egon Kochanke,alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo kujitambulisha.[Picha na Ramadhan Othman,Ikulu.]

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ingependa kuona wawekezaji wengi zaidi kutoka Ujerumani wanawekeza Zanzibar ikiwa ni njia mojawapo ya kukuza uhusiano mzuri na wa kihistoria uliopo kati ya Zanzibar na Ujerumani.Amesema kuimarisha uhusiano kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ujerumani ni suala linalopewa kipambele katika maudhui ya ushirikiano kati ya pande mbili hizo hivyo kupanua maeneo mapya ya ushirikiano kama katika uwekezaji ni hatua moja muhimu katika kutekeleza maudhui hayo.
Dk. Shein amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kila wakati imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kuimarisha mazingira bora ya uwekezaji ili kuvutia na kuongeza kasi ya uwekezaji katika sekta mbalimbali za uchumi na huduma ambapo alisisitiza kuwa fursa za uwekezaji Zanzibar hazina ukomo.
Akizungumza na Balozi Mpya wa Ujerumani nchini, Mheshimiwa Egon Kochanke, Ikulu leo, Dk. Shein ameeleza kuwa, historia inaonesha kuwa uhusiano kati ya Zanzibar na Ujerumani umeanza katikati ya karne ya 19 pale Ujerumani ikiwa kati ya nchi chache za mwanzo kuanzisha ofisi zake mjini Zanzibar.Kwa hiyo alimueleza Balozi huyo kuwa Zanzibar na Tanzania kwa jumla inajivunia uhusiano wake huo na Ujerumani kwa kuwa wakati wote umekuwa wa manufaa kwa Serikali na wananchi wa pande hizo mbili.
Aliongeza kuwa ni jambo la fahari kuona wakati wote Serikali na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ujerumani wamekuwa wakionesha dhamira na ari ya kuimarisha uhusiano huo.Alifafanua kuwa chini ya uhusiano huo, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Zanzibar ikiwemo, imeweza kufaidika na misaada mbalimbali kuanzia ya kiufundi hadi ya usaidizi katika bajeti ambapo sekta mbalimbali zikiwemo za jamii kama elimu, afya na maji zimekuwa zikinufaika na misaada hiyo.
Dk. Shein alitoa mfano wa msaada mkubwa wa ujenzi na ukarabati wa hospitali ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania, huko Bububu nje kidogo ya mji wa Zanzibar ambayo hivi sasa inatoa huduma muhimu sio tu kwa wanajeshi bali kwa wananchi wote hivyo kusaidia uimarishaji wa utoaji wa huduma za afya humu nchini.
Kwa hivyo alimuhakikishia Balozi Kochanke kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kama ilivyokuwa kwa mtangulizi wake, itampa ushirikiano wakati wote atakapokuwa nchini na kueleza matarajio yake ni kuona ushirikiano kati ya Zanzibar na Ujerumani unazidi kuimarika.
Wakati huo huo Balozi huyo mpya wa Ujerumani Mheshimiwa Egon Kochanke amesema Ujerumani itaendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wananchi wake katika kufanikisha malengo ya maendeleo waliyojiwekea.Balozi Kochanke ameleeza kufurahishwa kwake kupata fursa ya kuitumikia nchi yake katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchi ambayo alisema ni rafiki wa miaka mingi wa nchi yake.
Alimueleza Mhe Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kuwa amejionea mazingira mazuri ya kisiwa cha Zanzibar na kufurahishwa kuona wageni wengi wakiwemo wananchi wa Ujerumani wanatembelea visiwa hivi mara kwa mara.
Balozi Kochanke alibainisha kuwa Zanzibar inaweza kutumia fursa ya kushiriki matamasha ya muziki na sanaa yanayofanyika kila mwaka nchini Ujerumani kutangaza utamaduni wake kwa mfano muziki, sanaa na filamu kama njia ya kuvutia watalii na wawekezaji.