Sunday, 3 August 2014

Wananchi watahadharishwa kuwa na macho na baadhi ya wanasiasa wasiotaka maendeleo

 Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seiof Ali Iddi akibadilishana mawazo na Uongozi wa Kamati ya Skuli ya Sekondari ya Fujoni mara baada ya kukaguwa majengo ya Maabara na Maktaba na kukabidhi mbao kwa ajili ya uwezekaji majengo hayo.
 Balozi Seif akimkabidhi Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Sekondari ya Fujoni kulia yake Maalim Mabrouk Ishaq Daima Mbao pamoja na mitwiko yake kwa ajili ya uwezekaji majengo mapya ya Maktaba na Maabara ya Skuli hiyo.
 Balozi Seif akikabidhi Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Fujoni Maalim Mabrouk Ishaq Daima fedha za fundi wa uwezekaji wa mapaa ya majengo ya Maabara na Maktaba ya Skuli hiyo.
Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif akizungumza na Uongozi wa Kamati ya Skuli ya Sekondari ya Fujoni ndani ya Ofisi ya Mwalimu Mkuu mara baada ya kukabidhi vifaa kwa ajili ya uwezekaji wa majengo ya Maabara na Maktaba ya Skuli hiyo.

Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
 
Wananchi wameendelea kutahadharishwa kuwa macho na tabia ya baadhi ya wanasiasa wenye hulka ya kushawishi jamii kutoshiriki harakati za maendeleo na ustawi wa jamii kwenye maeneo yao kwa sababu tu ya itikadi ya kisiasa.
 
Tahadhari hiyo imetolewa na Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi wakati akikabidhi vifaa mbali mbali vya uwezekaji wa majengo ya Maabara na Maktaba ya Skuli ya Sekondari ya Fujoni iliyomo ndani ya Jimbo la Kitope Wilaya ya Kaskazini “ B”.
 
Balozi Seif ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema ipo miradi mingi ya maendeleo ya wananchi katika maeneo tofauti mengine ikipata usaidizi wa ufadhili wa wawekezaji waliomo katika maeneo hayo, lakini cha kushangaza ni kuona baadhi ya wanasiasa walafi hushawishi wananchi hao wasijihusishe kushiriki katika miradi hiyo.
 
“ Upo mradi wa uwekezaji wa Kitalii uliomo ndani ya jimbo langu ambao uongozi wake umeonyesha nia safi ya kutaka kusaidia maendeleo ya wananchi wanaouzunguuka mradi huo. Lakini cha kusikitisha ni kuona baadhi ya wanachi wake wamesusia kwa sababu tu za ushawishi wa Kisiasa uliochochewa kwa makusudi “. Alisema Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope.


Balozi Seif aliushukuru na kuupongeza Uongozi  mzima wa Kamati ya Skuli ya sekondari ya Fujoni kwa umahiri wake wa kuwajengea hatma njema ya kielimu watoto wao.
 
Alisema juhudi hizo ndizo zilizozaa matunda bora ya kielimu kwa kutoa fursa kubwa kwa wanafunzi wa skuli hiyo kuendelea na masomo yao ya kidato cha tano na sita baada ya kufaulu katika kiwango kinachokubalika Kitaifa.
 
“ Pongezi Maalum zimfikie mwalimu Mkuu wa Skuli yetu ya Fujoni  kwa kazi kubwa ya kusimamia maamuzi ya Kamati ya Uongozi wa skuli. Napata faraja kuona umoja wenu ndio onaofanikisha malengo mliojipangia “ Alifafanua Balozi Seif.
 
Akiwathibitishia Wananchi wa Jimbo la Kitope kuendelea kuliongoza Jimbo hilo endapo watampa ridhaa tena katika uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2015 Balozi Seif alisema yeye pamoja na Viongozi wenzake watahakikisha wanaongeza nguvu zao za kiuwezeshaji katika miradi mbali mbali wanayoianzisha wananchi hao.
 
Alisema kazi ya Uongozi ni kuhakikisha inaendelea kuwajengea  mazingira  makubwa zaidi wananchi wake hasa wanafunzi wa skuli zilizomo kwenye Jimbo hilo ili wawe na uwezo wa kuingia vyuo vikuu na kufikia daraja la utaalamu utakaokuja wasaidia wazazi na jamii inayowazunguuka hapo baadaye.
 
Mapema Mke wa Mbunge wa Jimbo la Kitope Mama Asha Suleiman Iddi alisema maendeleo ya kielimu yaliyopatikana ndani ya skuli ya Fujoni wapo wapo baadhi ya watu waharidhiki nayo kutokana na choyo cha roho walichokuwa nacho.
 
Mama Asha alieleza kwamba maendeleo hayo ambayo ni ya kupigiwa mfano yanastahiki kuigwa na vijiji vyengine vyenye malengo ya kujipatia maendeleo yanayotokana na nguvu zao wenyewe.
 
Mama Asha lielezea masikitiko yake na kulaani kitendo  kilichofanywa na baadhi ya watu kumsingiziwa kwamba aliahidi kujenga madrasa moja iliyomo ndani ya Kijiji cha Fujoni jambo ambalo niuzushi unaotaka kumuharibia kisiasa.
Alieleza kwamba tabia aliyojijengea ndani ya jamii ni kwamba anapo ahidi jambo tayari ameshajiandaa na kamwe hachukui muda mrefu kuitekeleza ahadi hiyo akielewa kwamba asipotekeleza tayari ameshabeba dhima kwa mwenyezi mungu.
 
Akitoa shukrani kwa niaba ya Uongozi  wa Kamati ya Skuli Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Sekondari ya Fujon i Mwalimu Mbrouk Ishaq Daima alimuhakikishia Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope kwamba Kamati hiyo itakuwa tayari wakati wote kutekeleza malengo yanayopangwa katika skuli hiyo.
 
Mwalimu Mabrouk Ishaq alimpongeza Mbunge huyo kwa jitihada zake anazochukuwa katika kuona maendeleo ya elimu ya skuli hiyo pamoja na Jimbo zima yanafikiwa.