Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Afisa Mkuu wa Kampuni ya Huawei ya China Bwana Bruce Zhang Ofisini kwake ndani ya Jengo la Msekwa katika Viunga vya Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mjini Dodoma.
Afisa Mkuu wa Kampuni ya Huawei Bwana Bruce Zhang akimuonyesha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif michoro ya mradi wao wa Umeme wa kutumia jua waliopanga kuuanzisha Visiwani Zanzibar.
Nyuma ya Bwana Bruce ni Mkurugenzi Fedha wa Huawei Bwana Peter Jiang pamoja na Meneja wa mradi wa Solution Bwana Briyan Peng.
Mkurugenzi Fedha wa Huawei Bwana Peter Jiang kati kati akitoa maelezo mbele ya Balozi Seif hayupo pichani ya jinsi mradi wa umeme wa kutumia jua utakavyoweza kufanya kazi kwa kiwango kinachokubalika.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akibadilishana mawazo na Ujumbe wa Kampuni ya Huawei mara baada ya mazungumzo yao yaliyofanyika kwenye Ofisi yake iliyopo Bungeni Mjini Dodoma.
Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ
Na Othman Khamis Ame, OMPR
Kampuni ya Mitandao ya Teknolojia ya Kisasa ya Nchini Jamuhuri ya Watu wa China ya Huawei inayoendesha na kusimamia mradi wa Umeme unaotumia jua { Solar Power Solution } imeonyesha nia ya kutaka kuwekeza mradi wa umeme unaotumia jua Visiwani Zanzibar kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Zanzibar { ZECCO }.
Ujumbe wa Kampuni Huawei ulioongozwa na Afisa Mkuu wa Kampuni hiyo Bw.Bruce Zhang ulieleza hayo wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini kwake iliyopo katika Jengo la Msekwa ndani ya Viunga vya Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mjini Dodoma.
Akitoa maelezo na ufafanuzi wa kina wa mradi huo Mkurugeni Fedha wa Huawei Bwana Peter Jiang alimueleza Balozi Seif kwamba mradi huo umepangwa kuwa na awamu tatu zitakazojitegemea zenyewe kulingana na mahitaji ya sehemu husika zitazofanikiwa kuwekwa mradi huo.
Bwana Peter alizitaja awamu hizo kuwa ni pamoja na ile ya mwanzo itakaolengwa katika miradi ya Skuli, Hospitali wakati ile ya pili itaelekezwa katika maeneo ya utalii pamoja na bara bara za maeneo ya mji.
Mkurugenzi huyo Fedha wa Kampuni ya Huawei aliitaja awamu ya tatu ya mradi huo itahusisha maeneo ya visima vya maji itakayokwenda sambamba na uimarishaji wa sekta ya kilimo kwa vile lengo kuu la mradi huo linategemewa kufaidisha jamii iliyopo vijijini ambayo kwa mazingira ya maisha ya kila siku hukosa huduma za umeme na kudumaza kwa mahitajio yao ya kijamii.
“ Mradi huu wa Solar Power umelenga kuangalia zaidi maeneo ya vijijini ambayo mara nyingi hukosa au kukumbwa na upungufu wa huduma za umeme “. Alisema Bwana Peter Jiang.
Alieleza kwamba uongozi wa Kampuni hiyo katika azma ya utekelezaji wa mradi huo imetoa fursa kwa wahandisi na baadhi ya watendaji wa shirika la umeme Zanzibar { ZECCO } kwenda kujifunza utendaji wa mradi wa solar ulioanzishwa na Huawei ulioko Makao Makuu ya Kampuni hiyo Nchini China.
Alifahamisha kwamba jitihada za msingi zitaendelea kuchukuliwa na Uongozi wa Kampuni hiyo katika kuona mradi huo unafanikiwa kuanzishwa Visiwani Zanzibar ili kusaidia wananchi walioko vijijini.
Naye Afisa Mkuu wa Kampuni hiyo ya Huawei Bwana Bruce Zhang alisema mradi huo unaweza kuanza rasmi Januari mwaka ujao endapo pande mbili kati ya Shirika la Umeme Zanzibar na Kampuni yake zitafikia makubaliano ya mafanikio.
“ Tunategemea kuweka saini mkataba wa kuanzishwa kwa mradi huo baadaye mwaka huu baada ya taratibu zote zinazohusika za uwekezaji wa mradi huo kufikiwa na kukubalika rasmi na Serikali kupitia taasisi inayohusika na masuala ya huduma za Umeme “. Alisema Bwana Bruce Zhang.
Afisa Mkuu huyo wa Kampuni ya Huawei alieleza kwamba miradi inayoanzishwa na Kampuni hiyo hupata Baraka na ruzuku kutoka Serikali Kuu ya Jamuhuri ya Watu wa China kupitia Benki yao maarufu ya Exim Bank.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba mradi wa Umeme wa kutumia jua ni muhimu sana kwa vile unaweza kuwa hakiba hasa wakati inapotokea hitilafu ya umeme unaotumika hivi sasa ambao ni chanzo kimoja tuu.
Balozi Seif aliuambia Uongozi wa Kampuni hiyo ya Huawei kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar bado inahitaji uwekezaji katika sekta tofauti nchini ili kusaidia kunyanyua uchumi wa Taifana kustawisha jamii.
Alisema uanzishwaji wa mradi kama huo Visiwani Zanzibar unaweza kusaidia kasi ya ongezeko la uwekezaji katika sekta ya viwanda vidogo vidogo vitakavyotoa pia ajira kwa wananchi hasa Vijana.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliutaka Uongozi huo wa Kampuni ya Huawei kuwasilisha maombi yake kwa wakati ili Serikali kupitia Taasisi husika zipate fursa ya kuangalia njia ya kufanikisha kuanzishwa kwa mradi huo.
Mradi wa Umeme unaotumia jua { Solar Power Solution } unaosimamiwa na Kampuni ya Huawei ya China na ambao tayari umeshavifaidisha Vijiji vipatavyo elfu moja Nchini Cameroun hutumia eneo la Square Metre Moja kwa kuzalisha umeme unaokadiriwa kufikia Mega wats 15.4.