Sunday, 28 June 2015

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiifungua Semina ya Siku moja juu ya mwenendo wa sarafu ya Tanzania dhidi ya Dola ya Kimarekani kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Hapo Ukumbi wa Baraza hilo Mbweni Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiifungua Semina ya Siku moja juu ya mwenendo wa sarafu ya Tanzania dhidi ya Dola ya Kimarekani kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Hapo Ukumbi wa Baraza hilo Mbweni Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar. Picha na Hassan Issa – OMPR – ZNZ.
Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Bwana Juma Hassan Reli akitoa ufafanuzi kabla ya kuanza kwa semina ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar juu ya mwenendo wa sarafu ya Tanzania dhidi ya Dola ya Kimarekani. Picha na Hassan Issa – OMPR – ZNZ.
Mkurugenzi wa Sera za Kiuchumi na Utafiti wa Benki Kuu ya Tanzania Dr. Masawe Joseph akitoa Mada kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi juu ya mwenendo wa sarafu ya Tanzania. Picha na Hassan Issa – OMPR – ZNZ.
Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mh. Pandu Ameir Kificho  wa pili kutoka kushoto akichangia pamoja na kuliza maswali kwenye semina ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar juu ya mwenendo wa sarafu ya Tanzania dhidi ya Dola ya Kimarekani. Picha na Hassan Issa – OMPR – ZNZ.





















Baadhi ya Watendaji wa Benki Kuu ya Tanzania { BOT } pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakifuatilia michango na maswali mbali mbali yaliyokuwa yakiulizwa na  baadhi ya Wajumbe hao kwenye kwenye semina hiyo. Picha na Hassan Issa – OMPR – ZNZ.

Press Release:-

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya Dola ya Kimarekani huathirika mara kwa mara kutokana na Taifa kutegemea kuagiza bidhaa zaidi kutoka nje badala ya bidhaa hizo kuzalishwa na makampuni ya hapa nchini
Alisema nyingi ya biadhaa zinazoingizwa Nchini huagizwa kwa fedha za kigeni, hususan Dola za Kimarekani na kuuzwa kwa fedha za Kitanzania jambo ambalo hushajiisha uingizaji zaidi wa bidhaa na huduma kutoka nje.
Balozi Seif Ali Iddid alisema hayo wakati akiifungua Semina ya siku moja ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi juu ya mwenendo wa Sarafu ya Tanzania dhidi ya Dola ya Marekani iliyofanyika katika Ukumbi wa juu wa Baraza la Wawakilishi Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Alisema athari ya kuteremka kwa thamani ya sarafu ya Shilingi ya Tanzania hasa katika kipindi cha hivi karibuni imekuwa kubwa zaidi kuliko  faida yake na kupelekea kuzuka kwa malalamiko kwa Wananchi waliowengi hasa wafanyabiashara kutokana na kubadilika sana kiwango cha sarafu hiyo dhidi ya Dola.
Balozi Seif alieleza kwamba kiwango cha ubadilishaji wa fedha kimekuwa ni mojawapo ya kubebea mfuko wa bei nchini ikishuhudiwa kupanda kwa bei za bidhaa zikiwemo zile  zinazotengenezwa hapa nchini ikitwaja sababu kubwa ni mwenendo wa thamani ya shilingi dhidi ya dola.
“ Hivi karibuni tumeshuhudia kupanda kwa bei za bidhaa, zikikwemo zinazotengenezwa na kuzalishwa humu humu nchini sababu inayotajwakuwa  ni mwenendo wa thamani ya shilingi dhidi ya Dola ya Kimarekani “. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alishauri kwamba ili kukabiliana na changamoto hiyo ya kuyumba kwa Thamani ya Shilingi ya Kitanzania umefika wakati kwa Wafanyabiashara na wawekezaji wa sekta ya Viwanda wajitahidi kuongeza uzalishaji kwa kutumia rasilmali za ndani ili kudhibiti mfumko huo.
Mapema Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Bwana Juma Hassan Reli alisema Fedha za Kigeni ziliadimika Nchini Tanzania katika miaka ya 80 kutokana na udhibiti wa fedha hizo kusimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania chini ya Sheria ya kudhibiti fedha za kigeni ya mwaka 1965.
Bwana Juma Reli alisema hali hiyo ilifungua mianya ya rushwa hasa kwa wale waliopewa dhamana ya kusimamia upatikanaji wa fedha za kigeni  kwa bei rasmi ambayo katika miaka ya kati ya 1967 - 1984 Dola moja ya Kimarekani ilibadilishwa kati ya shilingi 7.14 hadi shilingi 8.13 za Kitanzania.
Alisema mfumo huo pia ulichochea utoroshwaji wa mitaji kupelekwa nje ya nchi kwani Watanzani walio wengi wakipata fedha za kigeni kwa kutumia  njia mbali mbali walishawishika kuzitunza fedha hizo katika Mabenki ya nje ya nchi ili kukwepa sheria.    
Ili kuondokana na changamoto hizo Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania alieleza kwamba Serikali ilifanya mageuzi kupitia sheria ya fedha za Kigeni iliyopitishwa na Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1992 ambayo inamruhusu mtu yeyote kumiliki kiasi chochote cha fedha za kigeni au dhahabu ghafi hapa Nchini.
Alisema Wananchi hivi sasa wana haki ya kununua na kuuza fedha za kigeni kwenye maduka ya kubadilishia fedha pamoja na kuwa na akaunti ya fedha hizo katika mabenki ya Biashara, jukumu la Benki Kuu likibakia kuhakikisha kuwa soko la fedha linaanzishwa na kuendeshwa kwa nguvu za soko.
Bwana Reli alifafanua wazi kwamba soko liliopo sasa la fedha za kigeni linaendelea kukua  ambapo ndio msingi mkuu wa kuweka thamani ya shilingi ya Tanzania  baada ya kuanzishwa na Benki Kuu ya Tanzania mwaka 1994.
Akitoa Mada kwenye Semina juu ya mwenendo wa Sarafu ya Tanzania dhidi ya Dola ya Marekani Mkurugenzi wa Sera za Kiuchumi na Utafiti wa Benki Kuu ya Tanzania Dr. Masawe Joseph alisema sarafu ya Fedha ya Tanzania  imeachwa kwenye soko  ili kuiwezesha iende sambamba na masoko mengine ya Sarafu Ulimwenguni.
Dr. Masawe alisema mwenendo wa Shilingi ya Tanzania imeshuka thamani na kuufanya mfumko wa Bei Nchini kufikia asilimia 5.4% ikilinganishwa na Mataifa mengine Duniani zikiwemo baadhi ya Nchi za Bara la Afrika ambazo mfumko wao uko chini ya asilimia 3%.
Mkurugenzi wa Sera za Kiuchumi na Utafiti wa Benki Kuu ya Tanzania            alifafanua kwamba upungufu wa mapato yanayotokana na bidhaa ya dhahabu na bidhaa nyengine asilia umefidiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na kuongezeka kwa bidhaa za viwanda zinazozalishwa na kusafirishwa nje ya Nchi.
Alisema fidia hiyo imeifanya sekta ya Viwanda kukua na kukusanya mapato ya zaidi ya Dola za Kimarekani Elfu Moja kwa sasa kutoka Dola Mia Nane mwaka uliopita ikitanguliwa na Sekta ya Utalii ambayo kwa sasa inashikilia nambari Moja katika kuchangia pato la Taifa.
“ Lazima tuangalie hiyo shilingi ilipo kwa wakati husika ni mahala pake pazuri bila ya kuathiri pande zote zinazohusika kati ya wakusanyaji, wauzaji na watumiaji “. Alifafanua Mkurugenzi huyo wa Sera za Kiuchumi na Utafiti wa Benki Kuu ya Tanzania.
Dr. Masawe alieleza kwamba ni vyema ukawepo uwiano baina ya kushuka na kupanda kwa sarafu ya shilingi kwa vile pande zote husika zina hasara na kunufaika pia,  lakini cha kuzingatia zaidi ni udhibiti makini wa mambo hayo ya kupanda na kushuka.
Wakichangia mada ya mwenendo wa thamani ya shilingi ya Tanzania iliyotolewa na Mkurugenzi wa Sera za Kiuchumi na Utafiti wa Benki Kuu ya Tanzania Dr. Masawe Joseph, baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi  walisema uchumi wa Zanzibar unastahiki kuangaliwa kwa makini kulingana na mazingira yake ili kujieusha na matatizo yanayotokana na kushuka kwa sarafu ya Tanzania.
Wajumbe hao walisema mazingira ya Zanzibar yanategemea uchumi wa bidhaa chache ikilinganishwa na ule wa Tanzania Bara kiasi kwamba maisha ya wananchi walio wengi  Visiwani yanategemea Kilimo ambacho bado hakijawa na nguvu za kuwafanya wawe na uwezo wa kusafirisha kwa lengo la kupata uchumi imara.
Waliushauri Uongozi wa Benki Kuu ya Tanzania kuyaangalia mashirikia na Taasisi za Kiuchumi Nchini katika kuziwezesha wakati inapotokea hali au mazingira ya kuporomoka kwa sarafu ya shilingi ya Tanzania kwenye soko la Dunia.
Walifahamisha kwamba yao mashirika na Taasisi zisizopungua 90 Tanzania Bara ambazo ziliwahi kupewa nguvu ya uwezeshaji na Benki Kuu ya Tanzania katika kujiendesha wakati wa kuporomoka kwa soko la Sarafu Ulimwenguni miaka michache iliyoita.
Walieleza kwamba uimarishaji wa Mashirika na Taasisi za ndani ya Nchi utaongeza ufanisi sambamba na kuwapunguzia ukali wa maisha wafanyakazi wa Taasisi za umma na hata binafsi ambao ndani ya miezi mitatu iliyopita wameshindwa kukidhi mahitaji yao kutokana na kushuka kwa thamani ya shilingi.
Wawakilishi hao wameishauri Benki Kuu ya Tanzania kuangalia mazingira ya matumizi ya fedha ya kigeni  kama Yuan ya Jamuhuri ya Watu wa china kutokana na wafanyabiasha wengi wa Tanzania kwa zaidi ya asilimia 75% kuendesha biashara zao katika soko la China.