Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na
wanachama wa Kikundi cha Ufundi wa vyombo vya Moto cha Wagodo Gereji cha
Wete Pemba hapo katika Ukumbi wa Hoteli ya Hifadhi Tibirinzi Chake
chake Pemba. Picha Hassan Issa –OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akimkabidhi Fundi Mkuu wa Wadogo Gereji Bwana Hussein Moh’d Said Zana za Ufundi akitekeleza ahadi aliyowapa wanachama wa kikundi hicho cha ufundi zitakazowasaidia katikia harakati zao za kujitafutia mapato. Picha Hassan Issa –OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akimkabidhi Fundi Mkuu wa Wadogo Gereji Bwana Hussein Moh’d Said Zana za Ufundi akitekeleza ahadi aliyowapa wanachama wa kikundi hicho cha ufundi zitakazowasaidia katikia harakati zao za kujitafutia mapato. Picha Hassan Issa –OMPR
Press Release:-
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema licha ya
Serikali kujitahidi kutafua mbinu za kukabiliana na tatizo la ajira
lakini wananchi wenyewe hasa Vijana waliomaliza masomo yao wana fursa na
wajibu wa kuunda vikundi vya ujasiri amali vitakavyoweza kusaidia
kukabiliana na tatizo hilo.
Alisema suala la ajira hivi sasa limekuwa changamoto kubwa inayoikabili Dunia ambapo hata Mataifa
yaliyoendelea kiuchumi yanaguswa na changamoto hiyo inayoweza kupungua
iwapo jitihada kati ya Serikali ya taasisi Binafsi zitashirikiana katika
kuunganisha nguvu za pamoja.
Balozi
Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati akikabidhi zana za Kiufundi { Tools
Box } kwa Kikundi cha Vijana wajasiri amali cha Wadogo Garage hapo
Hoteli ya Hifadhi Tibirinzi Mjini Chake chake kufuatia ziara yake ya
hivi karibuni aliyoifanya Kisiwani Pemba.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar alikuwa akitekeleza ahadi aliyowapa Vijana
hao wenye mastakimu yao katika Mtaa wa Wete mkabala ya Jengo la Posta
ambao wanaojishughulisha na shughuli za ufundi wa Magari, Vespa, Piki
piki pamoja na Mashine zinazotumia umeme.
Alisema juhudi mbali mbali zitachukuliwa
na Serikali Kuu katika kuona vijana hao wanapata zana kamili
zitakazokidhi mahitaji yao ya kiufundi na kuwataka kuhakikisha kwamba
wateja wanaowahudumia wanalipa fedha za matengenezo kutokana na vyombo wanavyopeleka ili fedha zinazokusanya zisasaidie kuendesha maisha yao ya kila siku.
Aliwapongeza
vijana hao wa Kikundi cha ufundi cha Wadogo Gereji kwa uamuzi wao wa
kujikusanya pamoja na kuanzisha miradi itakayotowa mwanga katika
kukabiliana na ukali wa maisha hapo baadaye.
Balozi
Seif amekuwa akisisitiza kwamba Serikali imeanzisha mfuko wa Uwezeshaji
kupitia Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana Wanawake na
Watoto ambao umelenga kuwasaidia wananchi waliojikusanya pamoja kwa
kupatiwa mikopo ya kuendesha miradi yao ya Kiuchumi.
Nao Vijana hao wa Wadogo Gereji Wete
Pemba walimshukuru na kumpongeza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif kwa jitihada zake anazoendelea kuzichukuwa kila kukicha
katika kujaribu kusaidia kuunga mkono jitihada za wananachi mbali mbali
walioamua kujiletea maendeleo kupitia vikundi vya wajasiri amali.
Walisema
juhudi za Balozi Seif ziko wazi na kushuhudiwa na Wananchi waliowengi
Nchini na zinapaswa kuungwa mkono sambamba na kuigwa na Viongozi wengine
wa Taasisi za umma na hata zile za kiraia zinazotoa huduma za maendeleo
na kiuchumi hjapa Nchini.
Wakizungumzia
changamoto wanazopambana nazo vijana hao wa Wadogo Gereji walisema kuwa
ni pamoja na ukosefu wa sehemu maalum ya kufanyia shughuli zao za
kiufundi, umuhali walionao kwa wateja wao pamoja na ukosefu wa fursa za
masomo kwa nia ya kuongeza ujuzi waliokuwa nao.
Kikundi cha wajasiri amali cha Wadogo Gereji kilichoanzishwa miaka kadhaa iliyopita Chini ya Fundi Mkuu Nd. Hussein Moh’d Said kikiwa na wanachama 29 hivi sasa tayari kimeshafungua Tawi jengine la Kiufundi katika Kijiji cha Tumbe.