Wednesday, 1 April 2015

Kufungwa kwa Mkutano wa 19 wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

HOTUBA YA MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR,
MHE. BALOZI SEIF ALI IDDI KATIKA UFUNGAJI
WA MKUTANO WA 19 WA BARAZA LA WAWAKILISHI
ZANZIBAR, TAREHE 31 MACHI, 2015
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe Balozi Seif Ali Iddi Akihutubia wakati wa kufunga mkutano wa 19 wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar. 

1.0     Mheshimiwa Spika, naomba kuchukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu Mwingi wa Rehema kwa kutujaalia uzima na afya njema na kutuwezesha kumaliza Mkutano huu wa 19 wa Baraza la Wawakilishi kwa salama na amani. Pia, naomba kuchukua nafasi hii kukushukuru wewe Mheshimiwa Spika kwa kuliendesha Baraza letu hili kwa hekima, busara na ustahamilivu mkubwa.  Uwezo wako wa kuliongoza Baraza hili  ndio uliotuletea mafanikio makubwa katika  mkutano huu. Aidha, napenda kumshukuru Mheshimiwa Naibu Spika pamoja na Waheshimiwa Wenyeviti kwa kukusaidia kuuendesha Mkutano huu wa 19 kwa umakini na ufanisi mkubwa.

2.0     Mheshimiwa Spika, kwa aina ya kipekee naomba kumshukuru na kumpongeza kwa dhati Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein kwa namna anavyoiongoza nchi yetu kwa umahiri, hekima na busara kubwa hali ambayo imeiwezesha nchi yetu kupiga hatua kubwa ya maendeleo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii na kudumisha amani na utulivu. Vile vile, natoa shukurani kwa Makamu wa Kwanza wa Rais Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad kwa kumsaidia Mheshimiwa Rais katika kuiongoza nchi yetu.

3.0     Mheshimiwa Spika, nachukuwa fursa hii pia kuwashukuru Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri kwa kazi zao nzuri katika kuwasilisha taarifa za utekelezaji wa maagizo ya Kamati mbali mbali za Kudumu za Baraza hili Tukufu zinazohusu sekta zao na kutoa majibu kwa hoja mbali mbali zinazotolewa na Waheshimiwa Wawakilishi.

4.0     Mheshimiwa Spika, nawashukuru na kuwapongeza sana Waheshimiwa Wajumbe wote wa Baraza lako Tukufu kwa maswali waliyouliza juu ya utendaji wa Serikali na michango, mapendekezo na maelekezo yao waliyotoa wakati wa kujadili Miswada na hoja mbali mbali zilizowasilishwa hapa Barazani. Ni dhahiri kwamba, michango iliyotolewa na Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi inasaidia sana katika kuimarisha utendaji wa Serikali.

5.0     Mheshimiwa Spika, kabla ya kuelezea mafanikio tulioyapata katika Mkutano huu wa 19 kwa masikitiko makubwa naomba kuchukua nafasi hii kumkumbuka mwenzetu ambaye alikuwa Mjumbe wa Baraza hili Marehemu Salmin Awadh Salmin aliekuwa Mwakilishi wa Jimbo la Magomeni aliyefariki tarehe 19 Februari, 2015. Marehemu alikuwa ni kiongozi hodari, mwenye msimamo thabit, makini na shupavu na aliejitolea kuwatumikia wananchi kwa kipindi chote cha uhai wake. Hatuna budi kuyaenzi na kuyaendeleza yale yote mazuri ambayo ametuachia kwa manufaa ya nchi yetu.  Kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, naendelea kuwapa pole Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza, wanafamilia na wananchi wote kwa ujumla. Sisi sote ni waja wake Mwenyezi Mungu na bila ya shaka marejeo yetu ni kwake.   Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema peponi. Amin.

6.0     Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu wa 19 jumla ya maswali ya msingi 62 na maswali ya nyongeza 147 yaliulizwa na Waheshimiwa Wajumbe na kujibiwa na Waheshimiwa Mawaziri.  Aidha, jumla ya Miswada minne (4) imewasilishwa, kujadiliwa na kupitishwa na Baraza lako Tukufu.

Miswada hiyo ni:
a.      Mswada wa Sheria ya Kuweka Masharti ya Usajili na Usimamizi wa Wathamini na Mambo Mengine Yanayohusiana na Hayo.
b.      Mswada wa Sheria ya Kuanzisha Kamisheni ya Ardhi na Mambo Mengine Yanayohusiana na Hayo.
c.      Mswada wa Sheria ya Kufuta Sheria Namba 6 ya 1983 ya Baraza la Sanaa na Muziki na Sheria ya Bodi ya Sensa ya Filamu na Sanaa za Maonyesho Namba 1 ya 2009 na kutunga Sheria mpya ya Baraza la Sanaa na Sensa ya Filamu na Utamaduni Zanzibar  na Mambo Mengine Yanayohusiana na Hayo.
d.      Mswada wa Sheria ya Kufuta Sheria ya Miradi ya Maridhiano Namba 1 ya 1999 na kutunga Sheria mpya kwa ajili ya kuanzishwa na kuendesha mashirikiano baina ya Sekta ya Umma na Binafsi na Mambo Mengine Yanayohusiana na Hayo.

7.0     Mheshimiwa Spika, Baraza limejadili na kupitisha Sheria ya Kuweka Masharti ya Usajili na Usimamizi wa Wathamini na Mambo Mengine Yanayohusiana na Hayo kwa madhumuni ya kuweka utaratibu wa kisheria wa kusajili na kusimamia wathamini. Pia, sheria hii inapendekeza mfumo mpya wa kuanzisha bodi ya wathamini ambayo itakuwa na utendaji na ufanisi na yenye kukubaliana na mabadiliko ya kitaaluma na fani ya uthamini.

8.0     Mheshimiwa Spika, Serikali inawashukuru sana Waheshimiwa Wajumbe wote kwa mapendekezo yao waliyoyatoa ambayo yametoa mchango mkubwa katika kupatikana sheria hii.

9.0     Mheshimiwa Spika, mswada wa pili uliowasilishwa Barazani ni Mswada wa Sheria ya Kuanzisha Kamisheni ya Ardhi na Mambo Mengine Yanayohusiana na Hayo. Lengo kuu la mswada huu ni kuanzisha sheria itakayosimamia masuala ya ardhi katika kujenga uimara wa uongozi na usimamizi wa ardhi kwa ajili ya matumizi bora na maendeleo ya taifa.  Aidha, mswada huu unapendekeza kuanzishwa kwa Kamisheni ya Ardhi kwa ajili ya kuongoza na kusimamia masharti ya sheria hii pamoja na sheria nyengine zinazohusiana na masuala ya ardhi.

10.0    Mheshimiwa Spika, Serikali inawashukuru sana
Waheshimiwa Wajumbe wote kwa michango na maoni yao yaliyopelekea kupatikana kwa sheria hii ambayo itasaidia sana katika kuweka utaratibu wa matumizi bora ya ardhi na kupunguza migogoro ya ardhi nchini.

11.0    Mheshimiwa Spika, mswada mwengine uliowasilishwa ni Mswada wa Sheria ya Kufuta Sheria Namba 6 ya mwaka 1983 ya Baraza la Sanaa na Muziki na Sheria ya Bodi ya Sensa ya Filamu na Sanaa za Maonesho Namba 1 ya mwaka 2009 na kutunga Sheria mpya ya Baraza la Sanaa na Sensa ya Filamu na Utamaduni Zanzibar na Mambo Mengine Yanayohusiana na Hayo.  Madhumuni ya kufuta sheria hizo na kuanzisha sheria mpya ni kuimarisha utendaji wa kazi na kusimamia majukumu ya kulinda na kuhifadhi mila, silka na maadili mema ya Wazanzibari na kutumia utamaduni katika kupunguza umasikini kwa jamii.

12.0    Mheshimiwa Spika, kwa mara nyengine tena Serikali inawashukuru Waheshimiwa Wajumbe kwa michango yao ambayo ilisisitiza zaidi katika kulinda na kudumisha mila, silka na maadili mema. Ni mategemeo yetu kwamba, tutapata mashirikiano makubwa kutoka kwa wananchi katika utekelezaji wa sheria hii.

13.0    Mheshimiwa Spika, mswada wa mwisho uliowasilishwa katika mkutano huu wa 19 wa Baraza lako Tukufu ni Mswada wa Sheria ya Kufuta Sheria ya Miradi ya Maridhiano Namba 1 ya 1999 na kutunga Sheria mpya kwa ajili ya kuanzishwa na kuendesha mashirikiano baina ya Sekta ya Umma na Binafsi na Mambo Mengine Yanayohusiana na Hayo. Madhumuni makubwa ya mswada huu ni kuweka vipaumbele katika kuendeleza miundombinu ya kitaifa kwa mashirikiano baina ya Sekta ya Umma na Sekta binafsi katika kukuza uchumi endelevu na mendeleo.

14.0    Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wajumbe pia walipata muda mzuri wa kuchangia na kutoa maoni juu ya kuimarisha mswada huo. Ni imani yangu kwamba kupitishwa kwa mswada huu utasaidia kuimarisha uwazi na ushindani usiofungamana na mgongano wa kimaslahi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

15.0    Mheshimiwa Spika, kwa ujumla, Miswada yote hiyo ilikuwa na lengo la kutunga Sheria zenye kuimarisha, kukuza na kuendeleza uchumi wetu, kujenga mazingira mazuri ya utawala bora na uwajibikaji pamoja na kuongeza ufanisi katika utoaji na upatikanaji wa huduma za kijamii. Ni imani yangu kwamba, kupitishwa kwa sheria hizo kutarahisisha utekelezaji na usimamiaji wa mipango ya Serikali kwa watendaji wake na wananchi kwa ujumla.

16.0    Mheshimiwa Spika, pamoja na Miswada hiyo, katika Mkutano huu wa 19 Serikali pia iliwasilisha mbele ya Baraza lako Sheria ya Kura ya Maoni Namba 11 ya 2013 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mujibu wa Kifungu 132 (2) cha Katiba ya Zanzibar ya 1984 kwa ajili ya kuridhiwa na Baraza ambapo sheria hiyo ilipata ridhaa ya Baraza.

17.0    Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu pia Baraza lilipokea na kujadili Ripoti za Utekelezaji wa Maagizo ya Kamati za Kudumu za Baraza kwa mwaka 2013/2014. Taarifa hizo zilichangiwa kwa kina na Waheshimiwa Wajumbe na Waheshimiwa Mawaziri walitoa ufafanuzi wa hoja zote zilizotolewa. Nachukua nafasi hii kuwapongeza na kuwashukuru Wenyeviti wa Kamati na Wajumbe wao kwa kazi kubwa walioifanya ya kuihoji, kuishauri na kuielekeza Serikali katika kutekeleza majukumu yake. Naamini haya yote yalifanyika kwa nia njema kuisaidia Serikali kutekeleza wajibu wake kwa ufanisi.

18.0    Mheshimiwa Spika, nawahakikishia Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako Tukufu kwamba, Serikali imezipokea Taarifa za Kamati za Kudumu za Baraza na itayafanyia kazi mapendekezo yote yaliyotolewa kwa mujibu wa taratibu zilizopo.

19.0    Mheshimiwa Spika, vile vile katika Mkutano huu wa 19 Baraza lako Tukufu lilipata nafasi ya kupokea taarifa ya Kamati Teule ya Kuchunguza Upotevu wa Nyaraka. Namshukuru na kumpongeza Mwenyekiti wa Kamati Teule Mheshimiwa Mahmoud Mohammed Mussa na Wajumbe wake wote kwa taarifa yao kwa Baraza na nawashukuru Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi waliochangia hoja hii. Aidha, nawashukuru Waheshimiwa Mawaziri walioitolea ufafanuzi hoja.

20.0    Mheshimiwa Spika, napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako Tukufu kwamba, Serikali imepokea Taarifa ya Kamati Teule na kupokea michango yote iliyotolewa katika Baraza. Serikali itayafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa katika Taarifa na kutokana na michango ya Wajumbe na hatua muafaka zitachukuliwa kwa wale wote waliohusika na kadhia.  Ni kweli kabisa kuwa tukio hili lilikuwa la kusikitisha sana.

21.0       Mheshimiwa Spika, Baraza pia lilipokea na kujadili hoja binafsi ya Mheshimiwa Hamad Masoud Hamad inayohusu ucheleweshaji wa upatikanaji wa Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi. Kuhusu suala hili, kwanza napenda kuwanasihi Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako Tukufu kuepuka jazba na utashi wa kisiasa wakati tunapojadili hoja mbali mbali hapa Barazani na pia tukumbuke kwamba, masuala mengine ni ya kisheria, sheria ambazo tumezitunga sisi wenyewe. Suala la kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi ni suala la kisheria na kila Mzanzibari anastahiki kupata kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi baada ya kutimiza masharti yaliyowekwa kisheria.

22.0    Mheshimiwa Spika, nawaomba Waheshimiwa Wajumbe na wananchi kwa ujumla wakaelewa kwamba, Serikali hii haitamnyima haki Mzanzibari yeyote aliyetimiza masharti ya kupata kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi. Ni wajibu wetu Viongozi kuwaelimisha wananchi wetu juu ya utaratibu wa kisheria uliopo na kuwataka kuufuata utaratibu huo bila ya kuweka shindikizo za kisiasa.

TAARIFA ZA KISEKTA

23.0    Mheshimiwa Spika, kilimo bado kinaendelea kuwa ni mhimili mkuu wa uchumi wetu na ndicho kinachotoa ajira kwa wananchi walio wengi, kwa kutambua hilo Serikali inaendelea kutekeleza programu na miradi mbali mbali ya kilimo.  Juhudi hizi zimepelekea kuimarika utoaji wa elimu kwa wakulima wa mazao ya chakula, biashara, viungo na matunda,  matumizi ya pembejeo, matumizi ya zana za kisasa za kilimo ikiwemo matrekta na miundo mbinu ya umwagiliaji maji mashambani.

24.0    Mheshimiwa Spika, kwa mwaka huu 2014/2015, matayarisho  ya msimu wa kilimo cha mpunga yanaendelea ambapo jumla ya matrekta 32 yamekuwa yakitoa huduma kwa wakulima. Kazi hii imekuwa ikifanyika kwa mafanikio makubwa ambapo hadi sasa jumla ya ekari 16,197 kwa Unguja na Pemba zimeshatayarishwa. Aidha, Serikali imenunua na kusambaza kwa wakulima jumla ya tani 225 za mbolea ya TSP, Urea tani 600, dawa za kuulia magugu lita 15,000. Pia, tani 146 za mbegu zimenunuliwa na kusambazwa. Napenda kutoa wito kwa wakulima wote kukamilisha shughuli zao za kilimo ili kuzitumia vizuri mvua zinazoendelea.

25.0    Mheshimiwa Spika, katika kuendeleza matumizi bora ya ardhi nchini  (Land Use Planning), Serikali imekamilisha Mpango Mkuu wa Kitaifa wa Matumizi Bora ya Ardhi wa Zanzibar. Utekelezaji wa Mpango huu utasaidia kupunguza matumizi holela ya ardhi. Sambamba na Mpango huo, Serikali imetayarisha Sheria ya kuanzisha Kamisheni ya Ardhi itakayosimamia matumizi yote ya ardhi nchini. Aidha, Serikali imeendelea kuziimarisha Mahakama za Ardhi kwa kuzipatia vitendea kazi na kuziongezea idadi ya Mahakimu. Juhudi zote hizi zimelenga katika kupunguza tatizo la migogoro ya ardhi lililodumu kwa muda mrefu.

26.0    Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Washirika wa Maendeleo inaendelea na jitihada zake za kuwapatia wananchi wake huduma bora ya maji safi na salama. Katika kutimiza azma hiyo, Serikali imeendelea kutekeleza Miradi na Programu mbali mbali za kuwapatia wananchi wake maji safi na salama pamoja na kuendeleza Mpango wa Kulinda Vyanzo vya Maji Unguja na Pemba. Vile vile, Serikali imeifanyia matengenezo makubwa miundombinu ya usambazaji maji katika maeneo mbali mbali mjini na vijijini ili kuhakikisha kuwa  huduma ya maji inapatikana kwa wananchi wakati wote bila ya usumbufu. Aidha, Serikali imechukua hatua maalumu ya kuziondosha mita 41 za TUKUZA zilizokuwepo katika visima mbali mbali vya miradi ya maji ili kuwaondoshea kero wananchi na kuhakikisha wanapata huduma ya maji safi na salama bila ya usumbufu.  Lakini hapo hapo ningependa kuwanasihi wananchi kwamba waache kuvichafua vianzio vya maji kwa kujenga katika vianzio hivyo.

27.0    Mheshimiwa Spika, Sekta ya Utalii imeendelea kuimarika. Idadi ya watalii walioingia nchini imeendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka na kufikia  watalii 274,619 mwaka 2014.  Ongezeko hili linatokana na kuimarika kwa miundombinu ya utalii pamoja na hali ya amani na utulivu uliopo nchini. Nawaomba viongozi na wananchi wote kuendelea kudumisha amani katika nchi yetu hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu ili utalii wetu uzidi kuimarika na uchumi wetu uzidi kukua.  Nawasihi sana wananchi wawe wakarimu kwa wageni wetu wanapokuja kututembelea ili isadifu ile kauli mbiu yetu ya “UNGUJA NI NJEMA ATAKAE AJE”.  Ukarimu wa Wazanzibari unajulikana duniani kote.

MAMBO MENGINEYO:
28.0    Mheshimiwa Spika, katika kipindi kifupi kijacho wananchi wote wa Tanzania watapata nafasi ya kuipigia Kura ya Maoni Katiba Inayopendekezwa, Katiba ambayo kama itakubalika ndio itakayoliongoza Taifa letu katika kipindi cha miaka 50 ijayo. Kufanyika kwa kura hiyo kutakamilisha awamu ya tatu ya mchakato wa uandikaji wa Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ili kuhakikisha kuwa Watanzania wanafanya maamuzi sahihi siku ya tarehe 30 Aprili, 2015, nawasihi wananchi kuisoma kwa makini na kuielewa Katiba hiyo inayaopendekezwa na maamuzi yao yatokane na matakwa na ridhaa zao binafsi na siyo kushawishiwa  na watu, vikundi au vyama vya siasa.  Katika kufanikisha hilo Serikali imegawa nakala za Katiba Inayopendekezwa kwa wananchi  Tanzania nzima ili waisome, waielewe na kuifahamu. Ni imani yangu kuwa Watanzania wote wataitumia fursa hii adhimu na adimu kuhakikisha nchi yetu inapata Katiba kwa kwenda kupiga kura ya maoni kwa amani, utulivu na usalama.

29.0    Mheshimiwa Spika, vile vile mwaka huu wa 2015 ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu hapa nchini. Wananchi watafanya maamuzi ya kuwachagua viongozi watakaowaongoza ikiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Zanzibar, Wabunge, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani katika kipindi cha miaka mitano ijayo.  Ni imani yangu kwamba, wananchi watajitokeza kwa wingi katika kuitumia nafasi hiyo ili kuwachagua viongozi wao pamoja na kujitokeza kugombea nafasi za uongozi kwa wale wenye sifa za kufanya hivyo.  Aidha, Serikali kwa upande wake inaendelea na maandalizi ya uchaguzi huo ikiwemo uboreshaji wa Daftari la Wapiga Kura, kutoa elimu ya uraia na upatikanaji wa vifaa vya upigaji kura.  Sambamba na hayo Serikali itahakikisha kwamba chaguzi zote hizo zinafanyika katika hali ya usalama na amani kwa kutovifumbia macho vitendo vyote vinavyoashiria uvunjifu wa amani.

30.0    Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii nitoe wito maalum kwa viongozi wote wa kisiasa na wa kijamii pamoja na wananchi kwa ujumla tushirikiane na Serikali katika kuendeleza na kudumisha amani na utulivu uliopo katika nchi yetu.

31.0    Mheshimiwa Spika, kwa masikitiko makubwa hivi karibuni nchi yetu ya Tanzania imeingia katika wimbi la utekaji na  mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino).  Mengi yamesemwa kuhusu sababu za matokeo haya. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inalaani kwa nguvu zote suala hili na iko pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hatua inazoendelea kuchukuwa katika kukabiliana na tatizo hili. Kwa mnasaba huu nachukua nafasi hii kutoa wito maalumu kwa wananchi kuongeza mapenzi na huruma baina yetu katika kuwalinda na kuwathamini wenzetu hawa.

32.0    Mheshimiwa Spika, kama tunavyoelewa kuwa hivi sasa tuko katika kipindi cha Msimu wa Mvua za Masika. Mwanzoni mwa Machi, 2015 Mamlaka ya Hali ya Hewa ya Tanzania kanda ya Zanzibar ilitoa taarifa  ya muelekeo wa mvua za masika kwa kipindi cha Machi hadi Mei 2015. Mvua hizo tayari zimeshaanza na zinaendelea.  Ili kujikinga na majanga na maafa yanayoweza kutokea katika kipindi hichi yakiwemo maradhi ya mripuko na mafuriko, nachukua nafasi hii kuwakumbusha wananchi kudumisha hali ya usafi wa mazingira yetu yanayotuzunguka na kushirikiana na Baraza la Manispaa, Mabaraza ya Miji na Halmashauri zote za Unguja na Pemba katika kuchukua hatua madhubuti  za kuweka maeneo yetu katika hali ya usafi ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza. Aidha, Serikali kupitia Wizara ya Afya itaendelea kuielimisha jamii  juu ya madhara yanayoweza kutokea pamoja na hatua madhubuti za kujikinga na maradhi mbali mbali yanayoweza kutokea katika kipindi hiki.

33.0    Mheshimiwa Spika, vile vile naomba kuchukua nafasi hii  kuwakumbusha wananchi hasa wakulima kukitumia vizuri kipindi hiki cha  mvua za masika tunachoendelea nacho katika harakati za kilimo cha mazao ya chakula na biashara. Aidha, Serikali itaendelea kushirikiana na wananchi katika upandaji wa miti ya kudumu ili kuweza kuongeza uhakika wa upatikanaji wa chakula na matunda na kuinua hali ya kiuchumi ya nchi yetu.

34.0    Mheshimiwa Spika, napenda kuwatanabahisha Waheshimiwa Wawakilishi wote kwamba mambo yaliyotokea ndani ya Baraza letu Tukufu tarehe 11 Machi, 2015 wakati wa kuwasilisha mbele ya Baraza Sheria ya Kura ya Maoni Na: 11 ya mwaka 2013 ya Jamhuri ya Muungano kwa mujibu wa kifungu 131(2) cha Katiba ya Zanzibar mwaka 1984 yamewasikitisha wananchi wetu wengi.  Yaliyotokea mnayajua, sina haja ya kuyaeleza kwa kirefu lakini mambo hayo hayakuwakilisha vizuri Baraza letu mbele ya macho ya wananchi wetu tunaowawakilisha. Wananchi wetu wengi wametuona kama tumekuja kucheza badala ya kufanya kazi waliyotutuma.  Kuhitilafiana kwenye Baraza ni jambo la kawaida lakini ni vyema busara ikatumika badala ya jazba.

Nasaha zangu kwenu tunaposhughulikia mambo ya Kitaifa tuweke kando jazba zetu.  Nawaombeni siku zote tufanye kazi tukielewa kuwa wananchi wetu wanatufuatilia matendo yetu ndani ya Baraza na watatuhukumu.

35.0    Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa, kwa mara nyengine tena naomba kukushukuru kwa dhati kabisa wewe binafsi kwa kazi kubwa unayoifanya ya kuliendesha Baraza letu kwa umakini mkubwa.  Vile vile, nawashukuru Naibu Spika, Wenyeviti wa Baraza na Wenyeviti wa Kamati za Kudumu kwa kutekeleza majukumu yao vyema kwa mashirikiano makubwa na kukusaidia vyema katika kutekeleza shughuli za Baraza. Aidha, nawashukuru Waheshimiwa Mawaziri, Naibu Mawaziri na Waheshimiwa Wajumbe wote wa Baraza la Wawakilishi kwa ushiriki wao katika mkutano huu wa 19 ambao umemalizika salama na kwa mafanikio makubwa.

36.0    Mheshimiwa Spika, nawashukuru watendaji wote wa Serikali wakiongozwa na Makatibu Wakuu kwa juhudi zao zilizoliwezesha Baraza kuendesha shughuli zake kwa ufanisi katika kipindi hiki.  Pia, namshukuru Katibu wa Baraza la Wawakilishi na wafanyakazi wote wa Baraza hili kwa maandalizi mazuri ya Mkutano huu.  Aidha, nawashukuru Wanahabari wote na Wakalimani wa lugha ya alama kwa kazi nzuri wanazoendelea kuzifanya za kuwaelewesha wananchi wetu  yanayotokea katika Baraza hili.

37.0    Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, sasa kwa heshima na kwa ruhusa yako naomba kutoa hoja ya kuliakhirisha Baraza lako Tukufu hadi siku ya Jumatano tarehe 13 Mei, 2015 saa 3.00 barabara za asubuhi panapo majaaliwa.

38.0    Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.