Mwanamichezo Maarufu Nchini ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la
Uzini Moh’d Raza Hassanali aliyesimama akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kabla ya kukabidhi vifaa vya michezo kwa Timu ya Soka
ya Ofisi ya Makamu wa Pili. Wa kwanza
kulia ni Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Dr. Khalid
Salum Moh’d, wa mwanzo kushoto ni
Mjumbe wa Kamati ya Ufundi ya Timu ya Ofisi ya Makamu wa Pili Tajo
Hassan na Mwenyekiti wa Timu Haroub Gharib Bilal.
Balozi Seif akiziwashilisha Jezi kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar mara baada ya kukabilidhiwa na Mwanamichezo Maarufu Nchini Moh’d Raza.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Dr. Khalid Salum Moh’d akipokea soksi na mipira kutoka kwa Balozi Seif iliyotolewa na Moh’d Raza kwa ajili ya Tmu ya Soka ya Wizara yake.
Press Release:-
Mwanamichezo
Maarufu Nchini ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Moh’d Raza Hassanali
alisema Kampuni yake ya Hassan and Son’s
inakusudia kuanzisha mpango maalum wa kuzisaidia timu za Maskuli Unguja
na Pemba ili ile ari na vugu vugu la michezo lirejee kama zamani.
Raza alisema
hayo wakati wa hafla fupi ya kumkabidhi Seti za jezi, soksi na mipira Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwa ajili ya Timu ya Wizara ya
Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Hafla hiyo
fupi iliyofanyika Ofisini kwa Balozi Seif Vuga Mjini Zanzibar pia ilihudhuriwa
na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Dr. Khalid Salum
Moh’d pamoja na Viongozi wa Timu ya Wizara hiyo.
Raza alisema
wakati umefika kwa washirika wa michezo Nchini kuunga mkono mpango huo wa
kurejesha mashindano ya mara kwa mara katika maskuli ya Zanzibar kwa lengo la
kuwaandaa vijana kuwa na timu imara zitakazokuwa na uwezo wa Kimataifa.
Akipokea
msaada huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alimpongeza
Mwanamichezo huyo Maarufu wa Zanzibar Moh’d Raza kwa jitihada zake za kuunga
mkono sekta ya Michezo hapa Nchini.
Alisema
kitendo cha Mwanamichezo huyo ni miongoni mwa uzalendo aliouonyesha ambao
unastahiki kuigwa na washirika pamoja na wanamichezo wengine.
Balozi Seif
alisema juhudi za Mwanamichezo huyo zilipelekea kuteuliwa kuwa mshauri wa Rais
anayesimamia michezo pamoja na kuwa Mwenyekiti wa Saidia Zanzibar Ishinde { SAZI
} katika awamu zilizopita.
Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba lengo la Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar ambalo limo ndani ya Ilani ya chama cha Mapinduzi ni kukuza michezo hapa Nchini.
Alishauri
Taasisi zinazosimamia michezo Nchini kwa
kushirikiana na Ofisi yake ziandae utaratibu wa kuanzisha Ligi Maalum za
Mawizara ya Serikali na tayari Mwanamichezo Moh’d Raza ameonyesha nia shauku ya
kuzisaidia Timu hizo kwa kuzipatia vifaa endapo ligi hiyo itaasisiwa rasmi.