Sunday, 19 April 2015

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akihudhuria Mkutano wa pamoja kati ya Uongozi wa Kampuni inayohusika na masuala ya Teknolojia ya Kisasa ya mawasiliano ya Baharini { SRT } na watendaji wa sekta ya Habarini hapo Zanzibar Ocean View.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kati Kati akishindikizwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mh. Said Mohd Dimwa Kulia yake mara baada ya kuhudhuria Mkutano wa pamoja  kati ya Uongozi wa Kampuni inayohusika na masuala ya Teknolojia ya Kisasa ya mawasiliano ya Baharini  { SRT } na watendaji wa sekta ya Habarini hapo Zanzibar Ocean View. Picha Hassan Issa - OMPR – ZNZ.
Afisa Mkuu wa Mradi wa Teknolojia ya Kisasa ya mawasiliano ya Baharini  wa Kampuni ya { SRT } kutoka Nchini Uingereza  Bwana Simon Tucker akielezea umuhimu wa kifaa cha mawasiliano kinachotumika katika vyombo vya usafiri Majini kwenye Mkutano wa pamoja na watendaji wa Sekta ya Baharini hapa Zanzibar.
Picha Hassan Issa - OMPR – ZNZ.





















Balozi Seif akizungumza na Wanahabari   mara baada ya kuhudhuria Mkutano wa pamoja kati ya Uongozi wa Kampuni inayohusika na masuala ya Teknolojia ya Kisasa ya mawasiliano ya Baharini  { SRT } ya Nchini Uingereza na  watendaji wa Taasisi zinazohusika na sekta hiyo hapo Zanzibar. Picha Hassan Issa - OMPR – ZNZ.

 
Press Release:-

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Zanzibar ikiwa ni sehemu ya Dunia hii  inahitaji kuendelea kuwa salama na tulivu kutokana na mazingira yake yaliyozunguukwa na Bahari pembe zote.
Alisema mfumo wa kisasa wa mawasiliano unaotumika katika mataifa mbali mbali Duniani uliolenga zaidi katika maeneo ya bahari  yenye kutoa utajiri mkubwa kwa   asilimia 90% ya Uchumi wa Dunia unafaa kutumika ili kuondoa shaka katika udhibiti wa uvamizi wa vitendo vya kiharamia.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akizungumza na Wanahabari wa Vyombo mbali mbali hapa Nchini mara baada ya kuhudhuria Mkutano wa pamoja kati ya Uongozi wa Kampuni inayohusika na masuala ya Teknolojia ya Kisasa ya mawasiliano ya Baharini  { SRT } ya Nchini Uingereza na  watendaji wa Taasisi zinazohusika na sekta hiyo hapo Zanzibar Ocean View Kilimani Mjini Zanzibar.
Alisema yapo matukio kadhaa ya uvamizi wa vyombo vya Baharini yaliyowahi kuibuka  na kuripotiwa katika ukanda wa Pembe ya Afrika ambayo yalikuwa yakitekelezwa na maharamia kutokana na udhaifu wa mawasiliano uliokuwepo wakati huo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliridhika na kukubaliana na Mfumo wa kisasa waTeknolojia ya mawasiliano ya Baharini  unaotumiwa na Kampuni ya          { SRT } ya Nchini Uingereza katika Mataifa mbali mbali Duniani ambao umesaidia kupunguza wimbi la uharamia katika maeneo ya Baharini.
Akiwasilisha mada ya mfumo wa utendaji kazi wa Kampuni hiyo kwenye  Mkutano huo Afisa Mkuu wa Mradi wa Teknolojia ya Kisasa ya mawasiliano ya Baharini  wa { SRT }  Bwana Simon Tucker alisema  kifaa maalum cha Mawasiliano huwekwa kwenye chombo cha Baharini ambacho husaidia kutoa taarifa za mawasiliano.
Bw. Simon alisema chombo hicho kidogo kinachoweza kuwekwa kwenye boti au hata meli za uvuvi na abiria kinauwezo wa kusafirisha mawimbi ya mawasiliano kwa zidi ya meli 40.
Alisema mradi huo maalum wa mawasiliano ulioanzishwa mwaka 2008 tayari umekuwa ukitoa huduma katika Mataifa mbali mbali ulimwenguni ikiwemo Marekani, India na Ungereza yenyewe.
“  Asilimia 70% ya eneo lote la Dunia limezunguukwa na maji na kulifanya kuwa tegemezi kwa uchumi ulimwenguni kwa zaidi ya asilimia 90% kutokana na rasilmali ya mazao ya baharini kama samaki pamoja na usafirishaji wa mizigo pamoja na abiria “. Alifafanua Bwana Simon Tucker.
Mapema  Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Maharini Zanzibar { ZMA } Nd. Abdi Omar alisema Uongozi na watendaji wa Mamlaka hiyo wanajitahidi kumarisha huduma za mawasiliano baharini ili kuijengea mazingira bora sekta hiyo iendelee kutoa huduma kwa ufanisi.
Nd. Abdi alisema hatua hiyo imezingatiwa kutokana na mabadiliko ya Dunia ya Teknolojia yaliyoibua matukio ya kiharamia ambayo yameleta hasara kubwa ya kupotea kwa mali na hata maisha ya watu katika ukanda wa Pembe ya Afrika.
“ Mkutano wetu wa hivi karibu kati yetu ZMA wenzetu wa SUMATRA  ambapo tulishirikisha watendaji wa taasisi za ulinzi wa majini na na polisi bara na Zanzibar ulilenga katika kutafuta mbinu za kujiweka tayari kukabiliana na changamoto yoyote itayojitokeza katika eneo letu “. Alisema Mkurugenzi Abdi.
Mkutano huo mfupi ulihudhuriwa na watendaji kutoka mamlaka ya usafiri wa baharini,  Mamlaka ya Uwekezaji vitege uchumi Zanzibar { ZIPA }, Mamlaka ya Mapato Tanzania { TRA }, Kodi ya Mapato Zanzibar { ZRB }, Wizara ya Fedha, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Ardhi pamoja na Tume ya Mipango.