Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Kiwengwa Mwalimu Ali Mtumwa Ussi akipokea msaada
wa Vikalio 30 kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi. Kushoto ya
Balozi Seif ni Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi. Picha Hassan
–OMPR
Mkurugenzi Idara ya Elimu Sekondari Bibi Asya Iddi Issa akimpongeza Mbunge
wa Jimbo la Kitope Balozi Seif kwa jitihada zake za kuiunga mkono Wizara ya
Elimu katika kusaidia michango tofauti kwenye sekta ya Elimu. Aliyepo kati
kati yao ni Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Upenja Mwalimu Jaffar Ali Haji. Picha Hassan
–OMPR
Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif akimkabidhi Kiongozi wa Timu ya Soka ya New Star ya Kiwengwa Mcheni Abdulla shilingi Milioni 1,000,000/- zitakazosaidia matengenezo ya Uwanja wao wa michezo. Picha Hassan –OMPR
Balozi Seif akikabidhi mchango wa shilingi Laki 500,000/- kwa Kepteni wa Timu ya Soka ya Cairo Kiwengwa Ame Abdulla Ali zitakazosaidia timu hiyo katika harakati zao za kujiandaa na ligi.
Press Release:-
Mbunge wa
Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba karne iliyopo hivi sasa ya
21 ambayo imebeba Sayansi na Teknolojia ulimwenguni haistahiki watoto wa kizazi
chake kuendelea kupata elimu katika mazingira duni.
Alisema
juhudi za ziada kwa wazazi, wazee pamoja na Viongozi kwa kushirikiana na Kamati
za Maskuli zinapaswa kuchukuliwa ili kuona watoto wote Nchini wanaendelea
kujengewa mazingira yanayokwenda na karne hiyo.
Balozi Seif
Ali Iddi ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza hayo kwa
nyakati tofauti wakati akikabidhi vikalio 75 kwa ajili ya Skuli za Upenja na
Pwani Kiwengwa akitekeleza ahadi alizotoa kwa Walimu, Wanafunzi na Kamati za
Skuli hizo.
Vikalio 45 viligaiwa kwa Skuli ya Msingi na Sekondari
ya Upenja wakati vyengine 30 vikakabidhiwa kukamilisha Madarasa yote ya Skuli
ya Kiwengwa yakiwa na vikalio kamili vyote vikiwa na thamani ya Shilingi
Milioni Kumi na Mbili na Laki Tano {
12,500,000 }.
Balozi Seif
alisema ipo haja kwa viongozi wa Majimbo kuongeza nguvu zao katika kusaidia
huduma za Elimu ili kuiunga Mkono Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali ambayo
kwa sasa ina majukumu mengi ya kukamilisha majengo yaliyoanzishwa kwa michango
na nguvu za Wananchi wenyewe.
Alitoa mfano
wa jukumu kubwa linaloikabili Wizara ya elimu ya kuzipatia vikalio Skuli zote
za Unguja na Pemba ambapo bado kwa sasa upo upungufu mkubwa wa vikalio
vipatavyo 25 elfu Zanzibar nzima.
Alisema
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali
haijawa na nguvu kamili ya kuzipatia skuli zote za Zanzibar Vikalio kwani
Wizara hiyo hivi sasa ina mambo mengi ya kufanya likiwemo changamoto la
uwezekaji wa majengo yaliyoanzishwa na wananchi katika maeneo yao.
Alieleza
kwamba Taifa linahitaji kuwa na viongozi wengi wenye sifa zinazokubalika
Kitaaluma, lakini hilo halitapatikana endapo juhudi za makusudi hazitachukuliwa
na kuanzishwa na Viongozi katika kukabiliana na changamoto zinazowakabili
wanafunzi na Walimu katika skuli mbali mbali hapa Nchini.
“ Mimi kama
Mbunge wa Jimbo hili sitasita kuendelea kusaidia maendeleo ya Kielimu hata nje
ya Jimbo langu kutokana na wadhifa niliyokuwa nao hivi sasa wa Umakamu wa Pili
wa Rais wa Zanzibar “. Alisema Balozi Seif.
Aliahidi
kuendelea kuunga mkono juhudi kubwa zinazochukuliwa na Wananchi wa Jimbo la
Kitope kwa muamko wao wa kuanzishwa majengo mapya ya Madarasa kwenye skuli
mbali mbali za Jimbo hilo
Balozi Seif
alisema katika kuunga mkono juhudi za Wananchi pamoja na walimu atajitahidi ili
kuona nyumba za Walimu zilizojengwa katika skuli za Upenja na Kiwengwa
zinakamilika ili kuwaondoshea usumbufu walimu wa skuli hizo.
Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar alilipongeza Wazo la Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Amali Zanzibar la kuitaka Jamii inapojenga majengo mapya ya madarasa katika
maeneo yao yakaenda sambamba na ujenzi wa nyumba za Walimu.
Balozi Seif
alifahamisha kwamba hatua hiyo muhimu kwa kiasi kikubwa itawapa fursa na wasaa
mpana walimu kuweza kuwapatia taaluma wanafunzi wao kwa nyakati zote ukiwemo ule
muda wa ziada.
Mapema
Mkurugenzi wa Idara ya Elimu Sekondari Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Bibi
Asya Iddi Issa alisema msaada huo wa Vikalio kwa Skuli za Upenja na Kiwengwa
uliotolewa na Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi umeipa msukumo
Wizara hiyo katika kupunguza uhaba wa vikalio kwa skuli mbali mbali hapa
Nchini.
Bibi Asya
ameitahadharisha Jamii kujiepusha na wizi wa vifaa vya Maskuli ambao hurejesha
nyuma juhudi za wahisani pamoja na viongozi wanaoamua kusaidia vifaa hivyo kwa
lengo la kupunguza changamoto zinazojitokeza ndani ya sekta ya Elimu.
Alisema upo
ushahidi na baadhi ya matukio yaliyojichomoza kwa baadhi ya watu kuiba vifaa
hivyo hasa vikalio kwa kutengeneza vifaa vyengine na baadaye kuuza jambo ambalo
si utu wala uungwana kuendeleza tabia hiyo mbaya.
Wakitoa
shukrani kwa niaba ya wazazi, Walimu na
Wanafunzi wa Skuli za Upenja na Kiwengwa Walimu Wakuu wa Skuli hizo Mwalimu
Jaffar Ali Haji wa Upenja na Mwalimu Ali
Mtumwa Ussi wa Kiwengwa walielezea faraja yao kutokana na juhudi zinazoendelea
kuchukuliwa na Mbunge wa Jimbo lao Balozi Seif Ali Iddi.
Maalim
Jaffar Ali aliiomba Serikali ifanye utaratibu wa kuushawishi Uongozi wa Benki
ya Wananchi wa Zanzibar { PBZ } kufungua Tawi la Benki hiyo ndani ya Mkoa wa
Kaskazini ili kuwapunguzia usumbufu wa kukatisha vipindi Walimu wao wakati
Mwalimu Ali Mtumwa wa Kiwenga akaeleza kwamba Skuli hiyo imejipanga kutoa elimu
ya maandalizi katika kiwango kitakachokuwa mfano ndani ya Mkoa huo.
Katika kuchangia
juhudi za Walimu, Kamati ya Skuli na Wanafunzi wa Skuli ya Kiwengwa Mke wa
Mbunge wa Jimbo la Kitope Mama Asha Suleiman Iddi alikabidhi mchango wa
shilingi Milioni moja { 1,000,000/- } kusaidia uendelezaji wa Nyumba Walimu wa
skuli hiyo.