Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na Mkuu wa Mafunzo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Zanzibar Nd. Abdullah Othman Ali wakati wa hafla ya kuyafunga mafunzo hayo hapo Skuli ya Sekondari Donge Mkoa wa Kaskazini Unguja. Kati kati yao ni Mbunge wa Jimbo la Donge Mheshimiwa Sadifa Juma Khamis, na nyuma ya Balozi Seif ni Mratibu wa Mradi unaoondesha mafunzo hayo Nd.Abdi Hamid Abeid. Picha Hassan Issa – OMPR
Mkuu wa Mafunzo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Zanzibar Nd. Abdullah Othman Ali akimpatia maelezo Balozi Seif wakati alipotembelea Darasa la mafunzo hayo hapo Skuli ya Sekondari Donge. Picha Hassan Issa – OMPRBaadhi ya Wanafuzi wa Darasa la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Zanzibar wakishuhudiwa na Balozi Seif wakiendelea kufanya mazoezi ya vitendo katika kukabiliana na matatizo madogo madogo yanayojichomoza wakati wa matumizi wa kompyuta zao. Picha Hassan Issa – OMPR
Mmoja wa Wanafunzi wa Darasa la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Zanzibar akiperuzi kuangalia nini kimejiri duniani kupitia mtandao wa Internet akishuhudiwa na Balozi Seif. Picha Hassan Issa – OMPR
Baadhi ya Wananchi na Wanafunzi wakisikiliza Hotuba ya Mgeni rasmi Balozi Seif hayupo pichani wakati akiyafunga mafunzo ya miezi mitatu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Zanzibar hapo Skuli ya Sekondari Donge. Picha Hassan Issa – OMPR
Balozi Seif akimkabidhi Cheti Mwenyekiti wa Jumuiya Kupambana na changamoto na kuwaendeleza Vijana Zanzibar Bibi Umukulthum kwa kusaidia uendeshaji wa mafunzo ya Teknolijia ya Habari na Mawasiliano. Kati kati yao ni Mwenyekiti wa Umoja wa Madereva na Utingo Zanzibar Maalim Khamis Mussa, na kushoto ya Balozi Seif ni Mratibu wa Mradi wa Mafunzo ya Teknolijia ya Habari na Mawasiliano Abdi Hamid Abeid na Mkuu wa Mafunzo hayo Nd. Abdulla Othman Ali. Picha Hassan Issa – OMPR
Balozi Seif akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Jimbo la Donge, walimu na wanafunzi wa mafunzo ya Teknolijia ya Habari na Mawasiliano yaliyokuwa yakifanyika katika skuli ya Sekondari ya Donge. Kushoto ya Balozi Seif ni Mwakilishi wa Jimbo la Donge ambae pia ni Waziri wa Elimu Mh. Ali Juma Shamuhuna, Mratibu wa Mradi wa Mafunzo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Abdi Hamid Abeid na Mwenyekiti wa Jumuiya ya ZAFAYCO Bibi Umukulthum. Kulia ya Balozi Seif ni Mbunge wa Jimbo la Donge Mh. Sadifa Juma Khamis, Mkuu wa Mafunzo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Zanzibar Nd. Abdullah Othman Ali pamoja na Mwenyekiti wa Umoja wa Madereva na Utingo Zanzibar Maalim Khamis Mussa. Picha Hassan Issa – OMPR
Press Release:-
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewaasa Vijana wanaojifunza Taaluma ya Mitandao ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kuwa makini katika matumizi bora ya mfumo huo mpya ili kulinda mila na Tamaduni zao za asili.
Alisema si vyema kuthubutu kufanya matumizi maovu way mfumo huo akijua kwamba yatawashawishi kujiingiza katika matendo yatakayowapelekea kuwa na maamuzi ya kufanya vitendo vilivyo nje ya utamaduni wao.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa nasaha hizo wakati akiyafunga Mafunzo ya Miezi Mitatu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Zanzibar { TEKNOHAMA } yaliyoendeshwa kwa pamoja kati ya Umoja wa Madereva na Utingo Zanzibar { UMUZA } na Jumuiya ya kupambana na changamoto na kuwaendeleza Vijana Zanzibar { ZAFAYCO } hapo katika Majengo ya Skuli ya Sekondari Donge Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Alisema Dunia imekuwa na Mabadiliko makubwa ya Teknolojia ya Kisasa ya Mawasiliano inayokwenda kwa haraka kiasi kwamba Jamii za Kimataifa popote pale zilipo hupata fursa za kuwasiliana, kushirikiana na hata kupashana taarifa kupitia mfumo huo.
Hata hivyo Balozi Seif alifahamisha kwamba upo upotoshaji wa makusudi unaoendelea kufanywa na baadhi ya Watu ikiwemo pia mitandao ya Kijamii katika matumizi mabaya ya Mitandao hiyo jambo ambalo vijana hao wanapaswa kujiepusha nalo.
Alisema Jamii imekuwa ikishuhudia kashfa na matusi yaliyosheheni kwenye baadhi ya Mitandao hiyo tabia ambayo inadhalilisha watu wanaokusidia kuwachafulia wakiwa hawana hatia na pia kwenda kinyume na Haki za Kibinadamu.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameipongeza Jumuiya ya kupambana na changamoto na kuwaendeleza Vijana Zanzibar { ZAFAYCO } pamoja na Umoja wa Madereva na Utingo Zanzibar { UMUZA } kwa jitihada zao za kuwanoa vijana katika masuala yanayowagusa moja kwa moja.
Alisema kazi zinazoendeshwa na Taasisi hizo za Kiraia zimekuwa zikiisaidia Serikali Kuu katika azma yake ya kuwapatia taaluma hasa ile inayokwenda na wakati wa sasa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Wananchi wake katika maeneo mbali mbali Nchini Mjini na Vijini.
Balozi Seif alifahamisha kwamba Serikali katika kuziunga Mkono Taasisi hizo za Kiraia itajitahidi katika kuona inaunga mkono kazi za Taasisi hizo kwa watendaji na wakufunzi wake kuwawezesha kutoa mafunzo kama hayo kwa Vijana wa Kisiwa cha Pemba.
Katika kuunga mkono jitihada za Jumuiya ya kupambana na changamoto na kuwaendeleza Vijana Zanzibar pamoja na Umoja wa Madereva na Utingo Zanzibar amehidi kuchangia nguvu katika upatikanaji wa Mashine ya Projector pamoja na ile ya Fotokopi ili kuwarahisishia watendaji wa Taasisi hizo kuendesha vyema mradi wao wa mafunzo kwa Vijana.
Akisoma Risala Mkuu wa Mafunzo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Nd. Abdullah Othman Ali alisema zaidi ya vijana 368 wa Wilaya Tano za Unguja tayari wameshaptiwa mafunzo hayo yanayochukuwa muda wa miezi mitatu.
Nd. Abdullah alisema kwa kuelewa matatizo na changamoto zinazowakabili vijana katika maeneo mbali mbali Nchini Taasisi hizo zimebuni mradi huo kwa kuwakusanya pamoja vijana ili kuwapatia mafunzo yanayowawezesha kujiepuisha na makundi maovu.
Hata hivyo Nd. Abdullah alitaja baadhi ya changamoto zinazojichomoza katika mafunzo hayo akizitaja kuwa ni pamoja na muitiko mdogo wa washiriki wa mafunzo hayo hasa katika sehemu za Vijijini pamoja na uhaba wa vifaa vya kujifunzia kama Kompyuta.
Naye Mratibu wa Mradi wa mafunzo hayo wa Jumuiya ya kupambana na changamoto na kuwaendeleza Vijana Zanzibar { ZAFAYCO } Nd. Abdi Hamid Abeid alisema Jamii inaweza kupunguza uchafuzi wa mazingira endapo itakijika katika katumizi zaidi ya Kompyuta.
Alisema Wanafunzi wa Skuli za Sekondari na Vyuo Vikuu hivi sasa wamekuwa wakitumia kumbu kumbu za vitabu na baadhi ya maandisi na machapisho kupitia mtandao huo badala ya mfumo wa zamani wa kutumia vitabu vilivyokuwa vikitengenezwa kwa karatasi zinazotokana na kukatwa kwa miti.
Mratibu Abdi Hamid alifafanua kwamba upo mfano hai wa matangazo ya matokeo ya mtihani wa Darasa la Saba mwaka huu yaliyochapishwa katika mtandao wa Kompyuta mfumo ambao umeisaidia Serikali Kuu kuwepuka kutoka matangazo ya Redio ambayo yangegharimu mamilioni ya Fedha.
Alieleza kwamba Jamii lazima ikubali kwamba Kompyuta ni rafiki mzuri kwa mtumiaji ambapo hali hii iko wazi kutokana na mfumo wa watumiaji wa simu za mkono hivi sasa kupata huduma za vocha kwa njia ya kurusha.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif katika ufungaji wa mafunzo hayo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano alikabidhi vyeti kwa wahitimu wa mafunzo hayo pamoja na Skuli zilizotoa wanafunzi hao.