Mhandisi wa Kiwanda cha Matrekta Mbweni Haji Wa Haji Makame akimpatia
Maelezo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi moja ya Mashine
zinazotumika Kiwandani hapo. Picha Hassan Issa –
OMPR – ZNZ.
Balozi Seif akiangalia Mashine inayotumika katika uburugaji wa mashamba ya Mpunga. Picha Hassan Issa – OMPR – ZNZ.
Mkuu wa Kitengo cha Ufundi katika Kiwanda cha Matrekta Mbweni Mhandisi Moh’d Omar Moh’d WA Pili kutoka Kulia alimueleza Balozi Seif juhudi za Kiwanda hicho licha ya utengenezaji wa vyombo vya moto lakini pia hutoa mafunzo ya Ufundi kwa vijana wanaomaliza masomo ya sekondari. Wa mwanzo kutoka Kulia ni Mhandisi mwenzake wa Kiwanda hicho Haji Wa Haji Makame. Picha Hassan Issa – OMPR – ZNZ.
Balozi Seif akiangalia Mashine inayotumika katika uburugaji wa mashamba ya Mpunga. Picha Hassan Issa – OMPR – ZNZ.
Mkuu wa Kitengo cha Ufundi katika Kiwanda cha Matrekta Mbweni Mhandisi Moh’d Omar Moh’d WA Pili kutoka Kulia alimueleza Balozi Seif juhudi za Kiwanda hicho licha ya utengenezaji wa vyombo vya moto lakini pia hutoa mafunzo ya Ufundi kwa vijana wanaomaliza masomo ya sekondari. Wa mwanzo kutoka Kulia ni Mhandisi mwenzake wa Kiwanda hicho Haji Wa Haji Makame. Picha Hassan Issa – OMPR – ZNZ.
Press Release:-
Ukosefu wa
fungu maalum la matumizi pamoja na upungufu wa vipuri vya utengenezaji wa vyombo vya moto katika Kiwanda cha Matrekta
Mbweni ndio changamoto ya msingi inayosababisha
watendaji wa Kiwanda hicho kufanya kazi katika kiwango kisichoridhisha.
Mkuu wa
Kitengo cha ufundi katika kiwanda hicho Mhandisi Moh’d Omar Moh’d alieleza hayo
mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyefanya
ziara ya ghafla kwenye karakana ya Kiwanda hicho kuangalia uwajibikaji wa
watendaji hao hapo Mbweni Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Mhandisi
Moh’d Omar Moh’d alisema changamoto hiyo
kubwa wakati mwengine hupelekea baadhi ya Taasisi za Umma na hata
zile binafsi husita kupelekea vyombo vyao vya moto kwa ajili ya kupata huduma
za matengenezo ya kiufundi.
Alisema
Kitengo hicho licha ya kwamba hakina kifungu cha fedha lakini watendaji wake
hulazimika kufanya kazi wakati wote
kutegemea huduma wanazozipokea kituoni hapo hasa zile za Matrekta ya
Wizara ya Kilimo na Mali Asili.
Alieleza
kwamba Kiwanda hicho hivi sasa kimepokea Matrekta kadhaa kutoka Wizara ya Kilimo na Mali Asili ambayo
yanahitaji marekebisho ya kiufundi ili
yawahi kurejea kutoa huduma za kilimo mashambani Unguja na Pemba.
Mkuu huyo wa
Kitengo cha Ufundi Kiwanda cha Matrekta Mbweni alifahamisha kwamba Kitengo
hicho hivi sasa kinaendelea na mpango wa kushirikiana na Kampuni ya ufundi ya
Mahindra ya Nchini India kwa lengo la kujiimarisha kiufundi ili kiendelee kutoa
huduma za Kimataifa.
Mhandisi
Moh’d alifafanua kuwa wataalamu wa Kiwanda hicho wako katika hatua ya
kukamilisha mapendekezo yatayopelekwa kwenye Uongozi wa Kampuni
hiyo ya Mahindra kwa hatua zaidi.
Alieleza
kwamba Mpango huo wa maombi umeainisha pia namna Kiwanda hicho kinavyotaka
kujiimarisha zaidi katika utoaji wa mafunzo ya ufundi ngazi ya cheti kwa vijana
wanaoamua kuchukuwa fani hiyo.
“
Tunaendelea kufundisha vijana wetu wanaomaliza masomo yao ya sekondari kwa vile
tayari tumeshapata idhini ya Nacte na tunafarajika zaidi kwa vile masomo ya vijana
hao huambatana na mazoezi ya vitendo hapa hapa Kiwandani “. Alisema Mhandisi
Moh’d.
Naye Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliwapongeza watendaji wa Kiwanda cha
Matrekta Mbweni kwa juhudi wanazoendelea kuchukuwa katika utekelezaji wa
majukumu yao licha ya changamoto zinazowakabili kila siku.
Balozi Seif alielezea
faraja yake kutokana kwamba vifaa na
mashine nyingi zilizopo Kiwandani hapo bado zinaendelea kutumika tokea kuanzishwa
kwa Kiwanda hicho mwaka 1967.
“ Kazi
mnazozifanya mnastahiki kupongezwa hasa ikizingatiwa kwamba mashine zenu ni
zile zile mnazozitumia za mwaka 1967 “. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar aliufahamisha Uongozi wa Kiwanda hicho pamoja na
watendaji wake kwamba Serikali Kuu itaangalia namna itakavyoweza kusaidia
kukwamua changamoto zinazokikabili Kiwanda hicho.