Tuesday, 3 March 2015

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Waandishi wa Habari Nchini wana nafasi kubwa ya kuitumia Taaluma yao katika kusaidia Wananchi kufanikisha vyema kura ya maoni inayotarajiwa kufanyika mnamo mwezi wa Aprili pamoja na uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba mwaka huu.

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyevaa joho rangi ya zambarau aliyesimama pembeni kushoto akiambatana na Waziri wa Habari,Utamaduni, Utalii na Michezo Mh. Said Ali Mbarouk kulia yake pamoja na Mkuu wa Taaluma wakiyapokea maandamano ya wahitimu 105 wa cheti na Stashahada wa Chuo cha Uandishi wa Habari Zanzibar waliomaliza mafunzo yao mkupuo wa sita. Picha na Hassan Issa –OMPR – ZNZ.
 Baadhi ya wahitimu wa chuo cha Uandishi wa Habari Zanzibar ngazi ya cheti na stashahada wakiwa katika mahafali ya sita ya kumaliza mafunzo yao yaliyofanyika katika viwanja vya Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Kikwajuni Mjini Zanzibar. Picha na Hassan Issa–OMPR – ZNZ.
 Mhitimu wa Chuo cha Uandishi wa Habari Zanzibar Aboubakar Harith Bakari akisoma Risala ya wanachuo wenzake katika mahafali ya Sita ya chuo cha uandishi wa Habari Zanzibar. Picha na Hassan Issa–OMPR – ZNZ.
 Wahitimu wa Chuo cha Uandishi wa Habari Zanzibar ngazi ya Stashahada wakihudhurishwa kupatiwa Stashahada zao baada ya kumaliza mafunzo yao.
Picha na Hassan Issa –OMPR – ZNZ.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akimpatia tuzo mwanafunzi Tabia Abdi Amour aliyefanya vizuri zaidi katika somo la Uandishi wa Magazeti { Print in Journalism } ngazi ya Diploma. Kushoto ya Balozi Seif ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mh. Said Ali Mbarouk. Picha na Hassan Issa –OMPR – ZNZ.
Balozi Seif aliyevaa joho la rangi na zambarau akiagwa na Mwenyekiti wake Waziri wa Habari Mh. Said Ali Mbarouk kushoto yake mara baada ya kumaliza kwa mahafali ya Chuo cha Uandishi wa Habari. Picha na Hassan Issa–OMPR – ZNZ.























Balozi Seif  huo cha akimpongeza Mkuu wa Chuo cha Uandishi wa Habari Zanzibar Dr. Aboubakar Sheikh Rajab mara baada ya kumalizika kwa mahafali ya sita ya chuo cha Uandishi wa Habari Zanzibar yaliyofanyika katika Viwanja vya Wizara ya Habari Kikwajuni Mjini Zanzibar.  Picha na Hassan Issa –OMPR – ZNZ.


Press Release:-


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Waandishi wa Habari Nchini wana nafasi kubwa ya kuitumia Taaluma yao katika kusaidia Wananchi kufanikisha vyema  kura ya maoni inayotarajiwa kufanyika mnamo mwezi wa Aprili pamoja na uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba mwaka huu.
Alisema suala la amani na utulivu ambalo ni hazina kubwa inayojivunia Tanzania hasa ikazingatiwa kipindi hichi cha Taifa kuingia katika kura na uchaguzi huo Wanahabari wanapaswa ku jitahidi kuitumia vizuri kalamu yao katika kulinda amani iliyopo ili isije chezewa.
Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo kwenye mahafali ya Tano ya kuwatunuku Vyeti na Stashahada wahitimu 105 wa Chuo cha Uandishi wa Habari Zanzibar yaliyofanyika katika Viwanja vya Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Alisema wanahabari watapojikita vizuri kufanya kazi zao kwa kuzingatia maadili ya Taaluma yao pamoja na uzalendo ni dhahiri kwamba wataisaidia jamii katika kulinda amani iliyopo na kulifanya Taifa hili lipige hatua kubwa ya maendeleo.
Balozi Seif aliwaomba wahitimu hao wa Tasnia ya Habari kuwa wanahabari wema watakaoisaidia Nchi kuingia kwenye neema badala ya kuiingiza Nchi  katika nakama ambayo kwa njia ye yote ikitokea madhara yake yatamgusa kila mtu.
Alielezea matumaini ya Serikali kwamba taaluma waliyopipata wahitimu hao itakuwa chachu ya kuchapuza kasi ya maendeleo miongoni mwa jamii na Taifa kupitia kalamu zao.
Balozi Seif alielezea faraja yake kutokana na Maendeleo makubwa yaliyopatikana tokea kuanzishwa kwa Chuo cha Habari Zanzibar ambapo jumla ya wanachuo mia 628 wamehitimu ngazi mbali mbali tokea mwaka 2010.
Alisema Wahitimu hao tayari wanafanyakazi katika vyombo mbali mbali vya Habari vikiwemo vya Serikali zote mbili na hata vile binafsi wakiwemo baadhi yao kuamua kujitegemea na kuuza Habari zao kwenye Taasisi za Habari Bara na Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaelewa changamoto kubwa zinazokikabili chuo cha Habari Zanzibar likiwemo eneo la ujenzi wa majengo mapya ya kudumu ambapo tayari imeshatenga eneo la ukubwa wa Mita 180 kwa 150 litakalojengwa majengo hayo.
Alisema Serikali itatenga fungu maalum la fedha mwaka huu wa 2015/2016 kwa ajili ya kuendeleza mradi wa ujenzi wa majengo mapya  likiwemo la ghorofa mbili pamoja na kuyafanyia matengenezo makubwa majengo mawili yatakayotumika kama ofisi za chuo.
Balozi Seif alieleza kwamba Chuo hicho kimepatiwa eneo lililokuwa Kilimani Bar kwa ajili ya kuanzisha makazi ya kudumu kazi itakayogharimu Shilingi Bilioni Moja na Nusu mwaka huu zikitengwa shilingi Milioni 200 zitazotumika  kwa ujenzi wa Madarasa.
“ Hivi sasa Serikali tayari imekipatia chuo cha Habari jumla ya shilingi Milioni 90 na kazi za ujenzi zinaendelea na shilingi Milioni 110 zilizobakia zitatolewa wakati wowote kwa mujibu wa mkataba wa ujenzi uliopo “. Alisema Balozi Seif.
Alifahamisha kwamba Serikali inaamini kwamba ndani ya kipindi kifupi kijacho juhudi hizo zitaondosha changamoto inazokikabili chuo hicho ukiwemo uhaba wa madarasa .
Alieleza kwa hatua hiyo itaipa  fursa Serikali kuelekeza nguvu na macho yake katika upatikanaji wa vifaa vya kufundishia kama vbile kamera za kisasa, ujenzi wa studio zinazokwenda na wakati pamoja na ununuzi wa Kompyuta.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Serikali inatambua na kuthamini kwamba Taifa hupiga hatua kubwa ya maendeleo iwapo  watakuwepo wataalamu wa kutosha wa kada mbali mbali.
Alisema kuanzishwa kwa Chuo cha Habari Zanzibar kulilengwa na Serikali kutoa fursa kwa  vijana kupata taaluma itakayowawezesha hapo baadaye kulisaidia Taifa lao katika kusukuma  harakati za maendeleo, Uchumi na ustawi wa jamii.
Akisoma Risala ya wahitimu hao Chuo cha Waandishi wa Habari  Muhitimu Aboubakar Harith Bakari alisema wahitimu hao wameahidi kutumia vizuri kalamu zao ili lengo la taaluma waliyoipata liweze kufanikiwa.
Aboubakar Harith alisema yapo mafanikio yanayojichomoza kwa wanafunzi wa chuo hicho wakati wanapokuwa kwenye mazoezi ya vitendo ambapo baadhi ya vituo vya Habari huonyesha ishara ya kutaka kuwaajiri kuendelea na kazi kwenye vituo hivyo.
Hata hivyo alisema baadhi ya watendaji katika vituo wanavyofanyia mazoezi wamekuwa wakionyesha dharau kwa wanafunzi hao kiasi cha kuwakatisha tamaa ya kuendelea na mazoezi yao.
Akizungumzia suala la ajira Aboubakar alitanabahisha kwamba ongezeko la  vijana wasio na ajira litazidi kukuwa kutokana na mfumo wa sasa Taasisi za umma na hata zile binafsi kutangaza nafasi za kazi zikiainisha muhusika lazima awe na uzoefu wa kazi usiopunguwa miaka miwili.
Alisema kuna haja ya kuzingatiwa  kwa mabadiliko ya mfumo huo unanyima fursa  ambayo kwao ni kikwazo kwa vile ndio kwanza wanajiandaa kuingia katika soko la ajira baada ya kumaliza mafunzo yao.
Mapema Mkuu wa Chuo cha Habari Zanzibar Dr. Aboubakar Sheikh Rajab alisema juhudi za Uongozi wa Chuo hicho zimepelekea kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa kila mwaka.
Dr. Aboubakar alisema hatua hiyo imechangia ongezeko la  wanafunzi kwenye chuo hicho kwa zaidi ya mara mbili kwa mwaka jam bo ambalo limetoa faraja kwa walimu na Baraza la Chuo.
Akitoa salamu Mwenyekiti wa Baraza la chuo cha Uandishi wa Habari Zanzibar Ndugu Chande Omar Omar ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa jitihada inazochukuwa katika kuimarisha Chuo hicho.
Nd. Chande alisema kitendo cha Serikali cha kukipatia eneo la ujenzi wa majengo ya kudumu ya chuo hicho kimeleta faraja kwa wanataaluma wa tasnia ya Habari hapa Nchini.
Akimkaribisha mgeni rasmi kwenye mahafali hayo Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mh. Said Ali Mbarouk alisema mikakati imara imewekwa na Serikali kupitia Wizara hiyo ya kukijengea mazingira bora ya kutoa taaluma chuo hicho.
Waziri Mbarouk alisema vifaa kamili vya mafunzo kama kamera, studio za kisasa za utangazaji na kurikodi vitawekwa ili kuwapa fursa nzuri wanafunzi wa chuo hicho kukamilisha mazoezi yao ya kivitendo chuoni hapo.
Alisema hatua hiyo itawapa nguvu na uzoefu wanafunzi hao ili wakati wanapomba ajira waendelee na utumishi wao moja kwa moja badala ya kupatiwa mafunzo mengine ya ziada katika taasisi watazofanyia kazi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi katika Mahafali hayo pia alikabidhi zawadi kwa wanafunzi bora waliofanya vizuri katika masomo yao ya cheti na stashahada.
Mwanafunzi bora wa somo la uandishi wa magazeti { Print in Journalism } ni Tabia Abdi Amour, somo la Uhusiano wa Umma{ Public Reletions } ni Kassim Ali Hamad na  somo la Utangazaji { Broadcasting } Ibrahim Moh’d  Juma.
Mwanafunzi wa Darasa la cheti ambae amefanya vizuri masomo yote ni Asha Fum Khamis ambae anakuwa mwanafunzo bora kwa mwaka 2013/2014.